SERIKALI YAWAPIGA MKWARA WAMILIKI WA KUMBI ZA BURUDANI


 . Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari,Utamaduni na Michezo,Bw.Ceth Kamuhanda akitoa tamko la serikali kuhusu wamiliki wa kumbi ambao wanaziendesha kinyume cha sheria, kanuni na taratibu za nchi.Kulia kwake ni Mkurugenzi wa Idara ya Utamaduni, Profesa Hermas Mwansoko.

   
Wizara ya Habari, Utamaduni na Michezo imetoa miezi mitatu hadi Desemba 31 mwaka huu kwa wamiliki wa kumbi kuhakikisha wanafuata kanuni, taratibu na sheria za kuendesha kumbi zao ikiwa ni pamoja na kuzisajili Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) vinginevyo hatua kali za kisheria zitachukuliwa.
Akizungumza kwenye Jukwaa la Sanaa linalofanyika kila Jumatatu BASATA, Katibu Mkuu wa wizara hiyo,Bw.Ceth Kamuhanda alisema kwamba, kumekuwa na ukiukwaji wa makusudi wa sheria,kanuni na taratibu za kuendesha kumbi hali ambayo imekuwa ikisababisha maafa makubwa yakiwemo yale yaliyotokea Tabora mwaka jana na yale ya Sherehe za Idd El Fetri kwenye Ukumbi wa Luxury wilayani Temeke,Dar es Salaam.
“Tatizo kubwa la watanzania, ni kufanya mambo kiholela, kutokufuata sheria, kanuni na taratibu.Hili limekuwa kwenye mazoea na kwa kiasi kikubwa limekuwa likisababisha matatizo mengi yakiwemo majanga kama yale ya Tabora na Temeke kwenye Ukumbi wa Luxury” alisema.
Alisisitiza kwamba, serikali kamwe haiwezi kuendelea kufumbia macho vitendo visivyozingatia sheria hivyo wamiliki wa kumbi lazima wahakikishe wanafanya marekebisho kwenye kumbi zao na kuhakikisha kufikia Desemba mwaka huu zinakuwa ziko kwenye kiwango kinachokubalika kisheria na zimesajiliwa Baraza la Sanaa la Taifa.
“Serikali inasikitishwa sana na vifo ambavyo vimekuwa vikitokea kwenye kumbi za burudani hasa vya watoto na vijana na inaagiza wadau wote wa burudani hasa wamiliki wa kumbi kuzingatia sheria, kanuni na taratibu zilizopo zinazosimamiwa na BASATA”, aliongeza.
Awali Katibu Mtendaji wa BASATA,Ghonche Materego alizitaja sifa za kumbi zinazokubalika kisheria kuwa ni pamoja na kuwa na milango ya kutosha inayofungukia nje,vyoo nadhifu vya wanawake na wanaume, miundombinu kwa walemavu, vifaa vya kuzimia moto, maegesho ya vyombo vya usafiri na ulinzi kamili.
Aidha, alisema kuwa kumbi zote lazima zisajiliwe Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) lakini changamoto kubwa ni kasi ndogo ya wamiliki kusajili kumbi zao.Katika hili Katibu Mkuu,Bw.Kamuhanda alisema kwamba, ifikapo Desemba mwaka huu kama kutakuwa na kumbi zitakuwa hazijasajiliwa basi hatua kali za kisheria zichukuliwe.
Kwa upande wake,Mkurugenzi wa Idara ya Utamaduni Bw.Profesa Hermas Mwansoko alisisitiza kwamba, muda uliotolewa kwa wamiliki wa kumbi kurekebisha kumbi zao ili ziendeshwe kwa mujibu wa sheria, kanuni na taratibu ni wa mwisho na baada ya hapo hakutakuwa na huruma yoyote.
“Nafasi hii ni ya mwisho kwa wamiliki wa kumbi,BASATA wameshatoa maelekezo yote kuhusu sifa za kumbi.Hatutakuja kukumbushana tena suala hili lazima wamiliki wa kumbi watumie fursa hii iliyotolewa na serikali kufanya marekebisho” aliongeza Profesa Mwansoko.
Pamoja na Jukwaa la Sanaa wiki hii kujikita kwenye suala la kumbi masuala mbalimbali yaliibuka ikiwemo mada ya Soko la Sanaa ya Ubunifu wa Mavazi Tanzania na Changamoto zinazowakabili iliyowasilishwa na mbunifu maarufu wa mavazi Mustapha Hassanaly na kuvuta hisia za wadau wengi.
Wiki ijayo katika Jukwaa la Sanaa, Katibu Mtendaji wa Baraza la Habari nchini (MCT) Bw.Kajubi Mkajanga atazungumzia mada ya Vyombo vya Habari na Utandawazi Katika Tasnia ya Sanaa.

Comments