SERA YA UBUNIFU WA MAVAZI NCHINI INAHITAJIKA -HASSANALI

MMUNIFU WA MAVAZI NCHINI MUSTAFA HASSANALI AKITOA MADA KATIKA JUKWAA LA SANAA JANA.


Historia na utafiti kwa sanaa ya ubunifu ni muhimu kwa watanzania.
Imeelezwa kuwa ipo haja ya kufanyika utafiti wa kina na kuandika historia ya sanaa ya ubunifu wa mavazi hapa nchi, ili kuifahamisha jamii sanaa ya ubunifu ilikuwaje hapo nyuma, hivi sasa na mueleko wake wa baadae.
Ushauri huo umetolewa na mbunifu maarufu wa mavazi Tanzania Ndugu Mustafa Hassanali alipoluwa akiwasilisha mada ya hali ya sanaa ya ubunifu na changamoto wanazokabiliana nazo wasanii mbalimbali ambao wamejikita katika fani hiyo katika mkutano wa jukwaa la sanaa linalowakutanish wadau wa sanaa kutoka fani tofauti katika ukumbi wa BASATA, Ilala Sharifu Shamba jijini Dar es salaam.
“Ni vizuri tukajua kwa miaka iliyopita jamii ya watanzania walikuwa wakivaa mavazi ya aina gani? na kwa staili ipi?walikuwa wakifungaje vilemba, ni vazi la aina gani lilikuwa likipendwa zaidi, na mambo kama hayo ili kujua kama khanga, kitenge au vazi gani lilikuwa bora kwa wakati ule” Alisema Mustafa Hassanali.
Amesema BASATA iwapo itafanya hivyo itaisaidia jamii kupata taarifa hizo muhimu ambazo zitasaidia kujenga ufahamu wa kutosha wapi fani hii ilianzia, kwa sasa upo vipi na wasanii wafanye kuikuza na kunufaika nayo kama kazi nyingine.
Sambamba na hayo, aliishauri serikali kupitia wizara ya utamaduni na michezo, kuandaa sera ya sanaa ya ubunifu wa mavazi itakayosaidia kutoa muongozo katika sekta hiyo na ya sanaa ya ubunifu ambayo inakuwa siku hadi siku hapa nchini.
Hassanali amesema sambamba na sekta hiyo kukua bado haijatoa ajira tosha kwa wasanii kwani haijafikia uwezo wa kuuza na kufikiwa kwa malengo ya wasanii ambao siku zote wamekuwa mstari wa mbele katika ubunifu.
Aidha Mustafa amesema kuwa itakuwa ni jambo la busara iwapo itaandaliwa siku maalumu ya sanaa hapa nchini, siku itakayoakutanisha wasanii wa fani mbalimbali na kukaa pamoja kuweza kuangalia wapi wametoka, walipo na changamoto mbalimbali zinazowakabli na jinsi ya kukabiliana nazo.
“Siku zote umoja ni nguvu, na itapendeza iwapo wasanii watakutana pamoja na kupata fursa ya kujadili na kuzungumza mambo mbalimbali, pamoja na kuibua mbinu mpya za kuleta mafanikio katika fani ya sanaa hapa nchini.
Aidha mbunifu huyo wa mavazi aliongeza kuwa wasanii wa fani ya ubunifu wa mavazi wapatiwe fursa za kushiriki katika matukio mbailimbali yanayoandaliwa na serikali na taasisi mbalimbali kwani wanaowezo wa kutoa mchango mkubwa kufanikisha matukio hayo kupitia kazi zao.

Comments