ROCK CITY MARATHON 2010 YAFANA

BAADHI ya washiriki wa mashindano ya riadha ya kilometa 21 yanayojulikana kama Rock City Marathon wakichuana katika mashindano hayo yaliyofanyika jijini Mwanza Jumapili na kushuhudia Daudi joseph alishinda kwa upande wa wanaume na Polnes Chach akiwa kinara kwa upande wa Wanawake.Mashindano hayo yaliandaliwa na Capital Plus International ya Dar es Salaam

MWANARIADHA Daudi Joseph na Polnes Chacha wameibuka vinara katika mashindano ya

riadha kilometa 21 yanayojulikana kama ‘Rock City Marathon 2010’ yaliyofanyika Jijini Mwanza Jumapili.
Joseph alishinda mbio hizo kwa upande wa wanaume baada ya kuchukua saa 1:03:40
huku mwanadada Chacha akishinda kwa upande wa wanawake baada ya kutumia saa
1:13:10.Zaidi ya wanariadha 200 walijitokeza kushiriki mashindano hayo.
Wanaume walionekana kuwa na mchuano mkali kutokana na kutopishana sana kumaliza
mbio hizo ambapo Eliya Sidame alishika nafasi ya pili baada ya kupishana na
mshindi kwa sekunde 10 ambapo yeye alitumia saa 1:03:50.
Nafasi ya tatu kwa wanaume ilikwenda kwa Ezekiel Japhet aliyetumia saa 1:04:05
ikiwa ni tofauti ya sekunde 15 na aliyeshika nafasi ya pili na sekunde 25 na
Joseph aliyekuwa kinara wakati kwa wanawake Jacquline Juma alishika nafasi ya
pili kwa kutumia saa 1:18:09 na nafasi ya tatu ilikwenda kwa Rebeka Chacha
aliyetumia saa 1:19:05.
Katika mbio za kilometa 5, Mzungu Ndorobo alishinda na kufuatiwa na Victor
Daniel aliyekuwa wa pili na Dotto Ikangaa akishika nafasi ya tatu wakati katika
mbio za kilometa 3 ambazo zilikuwa maalumu kwa wazee, Jonas Mwangole alishika
nafasi ya kwanza akifuatiwa na Ramadhani Kinye aliyeshika nafasi ya pili.
Kwa upande wa wanawake kilometa 5 mshindi alikuwa Fazina Rashid akifuatiwa na
Saida Romanus aliyeshika nafasi ya pili huku nafasi ya tatu ikienda kwa Godriver
Michael.
Kivutio kikubwa kilikuwa katika mbio za kilometa 2 kwa watoto wa umri wa kati ya
miaka 7-10 ambapo Mary Chacha aliibuka mshindi huku nafasi ya pili ikienda kwa
Naomi Mganga na Jacquline Msese akishika nafasi ya tatu.
Mashindano haya yamedhaminiwa na Tigo Tanzania, Kampuni ya Ndege Tanzania
(ATCL), TTB, Mfuko wa Pensheni wa Taifa (PPF), Kampuni ya Executive Solutions,
Nyanza Bottlers Ltd, Hoteli ya New Africa, NSSF, Clouds FM na Isamilo Lodge ya
Mwanza.
Washindi katika mashindano hayo walizawadiwa vitu mbalimbali zikiwemo fedha
taslimu na nyinginezo kama fulana na kofia kutoka kwa wadhamini ambapo wale wa
kilometa 21 washindi walipata sh. 500,000/- wakati wa pili waliweka kibindoni
sh. 300,000/- na walioshika nafasi ya tatu walinyakua sh. 200,000/- kila mmoja.
Aidha washindi walioshika nafasi ya kwanza hadi 20 katika kila mbio walipatiwa
zawadi tofauti tofauti zikiwemo fedha tasilimu na kwamba hiyo ilifanywa
makusudi na Chama cha Riadha Tanzania (RT) kwa kushirikiana na waandaaji Kampuni
ya Capital Plus International kwa ajili ya kuongeza hamasa ya ishiriki.

Comments