PAULSEN AWAPONGEZA WACHEZAJI STARS KWA KUTOKA SARE YA 1-1 NA ALGERIA

JAN POULSEN

KOCHA timu ya soka ya Tanzania, ‘Taifa Stars,’ Jan Poulsen, amewapongeza wachezaji wake kwa kujituma na kuonyesha nidhamu ya kiwango cha juu katika mechi ya jana usiku dhidi ya Algeria.

Poulsen aliyerithi mikoba iliyoachwa na Kocha Marcio Maximo wa Brazil tangu Agosti mosi mwaka huu, alitoa pongezi hizo muda mfupi baada ya mechi hiyo iliyochezwa kwenye Uwanja wa Mustapher Tchaker, mjini Blida.
Ikicheza soka ya kuelewana, Stars ilikuwa ya kwanza kupata bao katika dakika ya 31 likifungwa na Abdi Kassim kwa mkwaju wa adhabu ya umbali wa mita 25.
Algeria iliyo chini ya Kocha Rabah Saadani, ilisawazisha bao hilo katika dakika ya 45 likifungwa na Adlene Guedioura, kwa shuti ya umbali wa zaidi ya mita 32.
Poulsen alisema matokeo hayo ya ugenini dhidi ya Algeria yenye uzoefu mkubwa wa mashindano ya kimataifa, ni mwanzo mzuri kwa kikosi chake ambacho amedumu nacho kwa mwezi mmoja.
‘Ni kama mwezi mmoja hivi tangu niitwae Stars, nawaahidi Watanzania nitajitahidi kujenga kikosi bora chenye kucheza kitimu kama ilivyocheza leo (juzi),” alisema Poulsen, raia wa Denmark na kuongeza:
“Ilikuwa ni mechi ngumu kwetu, kwani wapinzani wetu walikuwa nyumbani, achilia mbali aina ya wachezaji wao wanaocheza ligi za Ulaya, lakini vijana wamejitahidi kukabiliana nao kwa nidhamu kubwa ya kiuchezaji.
“Walitengeneza nafasi nyingi za kufunga, lakini tuliwadhibiti vizuri, hivi ndivyo tulipanga kucheza kwa sababu tulihitaji mipango mizuri ya kukabiliana nao.
Poulsen aliiwezesha Denmark kutwaa ubingwa wa Ulaya mwaka 1992, akiwa kocha msaidizi.
Katika mechi hiyo, kipa wa Stars, Shaaban Hassan ‘Kado’ alifanya kazi kubwa ya kuokoa michomo mingi ya wachezaji wa Algeria.
“Amefanya kazi kubwa katika mechi ya leo (juzi), alisema Poulsen akimsifia Kado anayedakia klabu ya Mtibwa Sugar ya Turiani, Morogoro.
Kuhusu upendeleo wa wazi wa aliyekuwa mwamuzi wa kati katika mechi hiyo, Djobi Kokou, kutoka Togo, Poulsen alisema huwa hapendi kuwazungumzia waamuzi.
Katika mechi hiyo, mwamuzi huyo alionekana wazi kutochukua hatua dhidi ya faulo zilizokuwa zikichezwa na wachezaji wa Algeria isipokuwa zile za Stars huku mechi hiyo ikichezwa kwa dakika 97.
Msafara wa Stars ukiwa na wachezaji 20 na viongozi 10, unarejea nchini kesho jioni kwa Ndege ya Shirika la Ndege la Qatar.
Baada ya mechi ya jana, katika mechi ya pili Stars itacheza na Morocco kati ya Oktoba 8 hadi 10, kabla ya kuwafuata Afrika ya Kati kati ya Machi 25 na 27, 2011.
Stars itaanza mechi za marudiano kati ya Juni 3 hadi 5 kwa kuwafuata Afrika ya Kati kabla ya kucheza na Algeria kati ya Septemba 2 hadi 4, 2011 na kumaliza kampeni dhidi ya Morocco kati ya Novemba 7 hadi 9, 2011.
Mara ya kwanza na mwisho kwa Stars kucheza fainali za CAN, ni mwaka 1980, ambazo zilifanyika mjini Lagos, Nigeria.

Comments

  1. huyo kocha ni komesha sana nakumbuka mwaka 92 waliichukua Denmark last moment lkn walifanya maajabu kwa kuchukua kombe la ulaya. kila la kheiri Poulsen.

    ReplyDelete

Post a Comment