MUSTAFA HASSANALI ALIVYOKIMBIWA NA MCHUMBA SABABU YA KUJIPUNGUZA MWILI

MUSTAFA HASSANALI
“WATU wanazungumza tu Mustafa kafanya hivi, kafanya vile wakati mimi sijamzungumza jambo lolote, wache waseme lakini ukweli naujua mwenyewe”, Hiyo ni kauli ya Mbunifu maarufu wa mitindo na mavazi Mustafa Hassanali.
Unajua ni kwanini ametoa kauli hiyo?, ni kutokana na kupingua kwake uzito kutoka kilo zaidi ya 120 hadi kufikia kilo 70 hali ambayo imesababisha minong’ono miongoni mwa watu huku kila mmoja akizungumza vyake na hata magazeti kuandika.
Katika mahojiano na maalum ofisini kwake juzi, Mustafa hakupenda kuweka wazi njia alizozifanya ili kutoka kwenye uzito mkubwa ‘Ubwanyenye’ mpaka kuwa na uzito wa kati zaidi ya kusema ni siri yake moyoni haina haja ya watu kufahamu alichokifanya.
Anasema awali alikubaliana na hali ya ‘ubwanyenye’ aliyokuwa nayo lakini kuna vitu vilikuwa vinamkweza katika sehemu ya maisha yake hivyo akaona kwa namna yoyote ni lazima ajipunguze ili kuweza kuishi kwa amani nha usalama.
Akifafanua anasema, alikuwa akipata tabu pindi anaposafiri kwenye ndege, anapokuwa katika hoteli migahawa ambapo alikuwa akipata tabu ya kupata kiti kinachomtosha,pia suala la kupata mavazi yanayokwenda na wakati yanayotosha umbo lake ili kuwa tabu sana hali ambayo ilimkosesha raha kabisa.
Pia alikuwa akikabiliwa na usingizi mara kwa mara,pia kutokana na kazi yake ya ubunifu haikuwa sahihi pia kuwa na umbo lile kwani hata anapopita jukwaani kutambulishwa baada ya kazi zake kupita jukwaani inamuwia vigumu kupita kwa uharaka kama wafanyavyo wenzake.
“Unajua kipindi kile cha unene wakati mwingine nilikuwa najiona kama mgonjwa na kuna wakati nilikuwa naenda hospitali na ninapofanyiwa vipimo nakutwa sina tatizo lolote, kumbe chanzo ilikuwa ni uzito mkubwa niliokuwa nao”, Anasema.
“Hivyo vyote nilivifikiria na kwa mara moja nikaamua kujitoa katika hali hile na kuja katika mwonekano mwingine, nashukuru mungu nimekuwa katika hali ya wastani ambayo inanifanya nimudu mambo ambayo nilikuwa nashindwa kuyamudu nilipokuwa bonge”, Anasema Hassanali.
Baada ya kufanikisha mchakato wa kujipunguza mwili wake Mustafa anasema anafurahia jinsi alivyobadilika, pia ameona kuna tofauti kubwa katika maisha na kaZi zake za kila siku zimekuwa kwani amekuwa na wepesi mkubwa unaomfanya amudu kufanya mambo mengi aliyokuwa akishindwa kufanya awali.
Hata hivyo, kupungua kwake kumemfanya aachwe na mpenzi wake ambaye alikasirika mabadiliko hayo na kwani alimpenda kutokana na jinsi alivyokuwa mnene, lakini hatoweza kuendelea na Mustafa aliyejibadilisha.
“Kwa kweli moja ya mikasa niliyokumbana nayo baada ya kujupunguza ni kukataliwa na mpenzi wangu ambaye kwa kweli hakupenda kabisa nilichokifanya kwani alinipenda kwa unene niliokuwa nao, iweje nijipunguze…yote kwa yote namshukuru mungu”, Aliongeza.

HISTORIA YAKE:
Alizaliwa jijini Dar es Salaam Juni 9, 1980 na kusoma katika shule tofauti za msingi na sekondari lakini elimu yake ya juu zaidi ni shahada ya udaktari aliyoipata mwaka 2003 katika chuo cha International Medical and Technological University (IMTU) kilichopo Mbezi beach jijini Dar es Salaam.
Hata hivyo Mustafa hakuwahi kufanya kazi aliyoisomea zaidi ya mazoezi na hilo lilitokana na kupenda kwake masuala ya ubunifu wa mavazi tangu alipokuwa mdogo, hivyo baada ya kumaliza kusomea udaktari aliipa kisogo fani aliyosomea na kuanza kufanya kitu ambacho roho yake inapenda.
Alianza rasmi kufanya kazi ya ubunifu wakati akiwa mwanafunzi wa (IMTU) ambapo alianza kujipatia umaarufu kabla hata ya kuingia rasmi katika medani ya ushindani ya fani hiyo, kuanzia mwishoni mwa miaka ya 1990 alikuwa ni mmoja ya wabunifgu ambao walikuwa wakishona nguo za baadhi ya watu maarufu kwa kipindi hicho.
Kwa uchache kazi za awali alizozifanya enzi hizo ni pamoja na kubuni baadhi ya nguo za mke wa rais wa awamu ya tatu Benjamin Mkapa, Mama Anna Mkapa, Nguo aliyoivaa kwenye fainali za Miss Tanzania 1999 na kisha kutwaa taji hilo, Hoyce Temu, Miss Tanzania mwaka 2000 Jackline Ntuyabaliowe na wengineo ambapo aliwafanyia hivyo mpaka walipiokwenda kushiriki fainali za Miss World.
Kama hiyo haitoshi, Mustafa pia amekuwa akiwabunia watu wengine wenye nafasi za juu za uongozi Serikalini, watu wa kati, warembo wanaoshiriki mashindano ya kanda mbalimbali iwe ndani na nje ya nchi, maharusi, mabalozi na wengine wengi nikiwataja kwa uchache.
Anasema alipenda kuwa mbunifu wa mavazi kutokana na kutaka kuwaona watu wanakuwa katika hali ya unadhifu na umaridadi zaidi bila kujali mamlaka walizonazo katika jamii lakini si kwa watu wa hapa nchini bali hata nje ya nchi ambapo kazi yake inakubalika.
Mustafa anaweza kuwa anaongoza kwa sasa kati ya wabunifua wa Tanzania ambao wamefanya maonyesho mengi ya mavazi na kukubalika kwa kiasi kikubwa nje ya nchi kwani kila mwaka hupata fursa ya kuonyesha kazi zake zaidi ya nchi kumi duniani.
Baadhi ya nchi ambazo amewahi kushiriki katika kuonysha kazi zake ni pamoja na Kenya, Uganda, Ethiopia, Msumbiji, Afrika Kusini, India, Cameroon, Italia na nyinginezo, huku baadhi ya kazi zake alizozitambulisha ni pamoja na Perfume D’ Amour , Mduara , Africa Collection, Kangalicious, Harusi, Namaste, Mama Afrika na nyinginezo.
Pia amekuwa akishiriki katika wiki za mavazi sehemu mbalimbali, India International Fashion Week , Arise Africa Fashion week 2009, Durban & Cape Town Fashion Weeks, Uganda & Kenya Fashion Weeks, Naomi Campbell’s Fashion for Relief 2009, Vukani Fashion Awards in Pretoria, Miss Ethopia Beauty Pageant, Mediterranean Fashion Festival in Sicily, Italy; M’Net Face of Africa, Msumbiji na nyinginezo.
Mustafa amekuwa na moyo wa kujitolea kwa kusaidia jamii za aina mbalimbali kwani ameweza kushiriki katika maonyesho ya kuchangia jamii hiyo kama wagonjwa wenye kansa ambapo hufanya hivyo kila mwaka, pia hospitali ya wagonjwa wenye akili visiwani Zanzibar ambapo mwaka huu ameshiriki kwa mara ya tatu.

WASIFU WAKE:
JINA:MUSTAFA HASSANALI
KUZALIWA : JUNI 9, 1980
KAZI:MBUNIFU WA MAVAZI
ELIMU:SHAHADA YA UDAKTARI

Comments