MUNGU IBARIKI TAIFA STARS, MUNGU IBARIKI TZ

TIMU ya soka ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars, leo inaanza kampeni yake ya kusaka tiketi ya kucheza fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (CAN) za mwaka 2012 kwa kukwaana na Algeria mechi itakayopigwa kuanzia saa 7 usiku kwenye Uwanja wa Mustapha-Tchaker, mjini Algiers, Algeria.
Mechi hiyo itachezeshwa na mwamuzi Djobi Kokou kutoka Togo ambaye wiki mbili zilizopita alichezesha mechi ya Ligi ya Mabingwa Afrika kati ya JSK Al dhidi ya Ahly huko Tizi Ouzou ni mechi inayotarajiwa kuwa ngumu kwa Stars.
Stars iliyokwenda Algiers na msafara wa wachezaji 20 na viongozi 10, ilitumia saa 5: 30 angani kabla ya kuwasili Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Houari Boumedienne, mjini Algiers na kupokelewa na viongozi wa Shirikisho la Soka la Algeria.
Kwa mujibu wa Rais wa Chama cha Wanafunzi wa Tanzania nchini Algeria (ATSA), Habib Luombo, walijiandaa vilivyo kuipokea Stars kwa mbwembwe zilizopambwa na wimbo wa Kiswahili usemao ‘Karibu Stars Mjini Algiers’ ili wajisikie kama wako Tanzania.
shangwe hizo zilifunika kwa muda maeneo ya uwanja huo wa ndege huku wanafunzi wa Tanzania nchini Algeria wakishangilia kwa bendera ya Tanzania huku kocha mkuu wa Stars, Jan Poulsen, akionyesha hali ya kujiamini akitumia kauli mbiu ya ‘Yes We Can’ yaani ‘Ndiyo Tunaweza.’
Akitaraji kupata ushindani mkali kutoka kwa wenyeji wao, Poulsen amesema vijana wake watapambana ili kupata matokeo mazuri licha ya kikosi cha Algeria kuundwa na nyota mahiri wanaokipiga kwenye nchi mbalimbali ikiwemo Ulaya.
Silaha zinazompa kiburi Poulsen ni makipa Shaaban Hassan 'Kado' (Mtibwa Sugar) na Jackson Chove (Azam FC).
Mabeki: Shadrack Nsajigwa (Yanga), Salum Kanoni (Simba), Aggrey Morris (Azam FC), Erasto Nyoni (Azam FC), Nadir Haroub (Yanga), Stephano Mwasika (Yanga) na Idrisa Rajabu (Sofapaka-Kenya).
Viungo: Jabir Aziz (Azam FC), Nurdin Bakari (Yanga), Abdi Kassim (Yanga), Seleman Kassim (Azam FC), Henry Joseph (Kongsivinger Il, Norway), Nizar Khalfan (Vancouver White Caps, Canada).
Washambuliaji: Mrisho Ngassa (Azam), Mussa Hassan 'Mgosi' (Simba), John Bocco (Azam FC) na Danny Mrwanda (Vietnam).
Kwa upande wa Kocha wa Algeria, Rabah Saadan atawakosa nyota wake kadhaa akiwemo Antar Yahia anayetumikia adhabu, Medhi Lacen anayechezea Racing Santander ya Hispania, Mourad Meghni wa Lazio ya Italia na Foued Kadir wa klabu ya Valenciennes ya Ufaransa ambao ni majeruhi.
Nyota wa Algeria ni makipa: Lounes Gaouaoui (USM Blida), Rais Mbolhi (Slavia Sofia), Mohamed Amine Zemmamouche (MC Alger).
Mabeki: Mohamed Chakouri (Charleroi), Habib Bellaid (Eintracht Frankfurt), Madjid Bougherra (Glasgow, Rangers), Rafik Halliche (Benfica), Abdelkader Laïfaoui (ES Setif), Carl Medjani (AC Ajaccio), Nadir Belhadj (Al-Sadd), Djamel Mesbah (Lecce).
Viungo: Adlene Guedioura (Wolverhampton), Hassan Yebda (Benfica), Fouad Kadir (Valenciennes), Karim Ziani (VfL Wolfsburg), Chadli Amri (Kaiserslautern), Djamel Abdoun (FC Nantes), Ryad Boudebouz (FC Sochaux).
Washambuliaji: Karim Matmour (Borussia Mönchengladbach), Rafik Djebbour (AEK Athens), Abdelkader Ghezzal (AS Bari) na Abdelmalek Ziaya (Al-Ittihad).
Baada ya mechi ya kwanza, Stars itarejea nyumbani kuisubiri Morocco kati ya Oktoba 8 hadi 10 kabla ya kuifuata Afrika ya Kati kati ya Machi 25 hadi 27, 2011.
Katika mechi za marudiano, Stars itaanza kwa kuikaribisha Afrika ya Kati mechi itakayochezwa kati ya Juni 3 hadi 5, 2011 kabla ya kuikaribisha Algeria kati ya Septemba 2 hadi 4, mwaka 2011 na kumaliza kampeni dhidi ya Morocco kati ya Oktoba 7 hadi 9 mwaka 2011.

Comments

  1. Kwa kweli JK boys kama wanavyopendwa kuitwa wamejitahidi sana na kuweza kutoka droo ya 1-1 hayo ni matokeo mazuri sana ugenini. Ukizingatia kauli ya kocha wa Algeria kabla ya mechi alisema nitaivunja vunja Tanzania. Lkn vijana wamemjibu kiwanjani, na wangetuli kidogo wangeweza kurudi na mzigo mzima wa pointa 3. Hongera TZ.

    ReplyDelete

Post a Comment