KOCHA WA ALGERIA AJIUZURU BAADA YA TIMU YAKE KUTOKA SARE NA STARS

KOCHA wa timu ya soka ya taifa ya Algeria, Rabah Saadane, amejiuzulu wadhifa huo ikiwa ni siku moja tangu timu hiyo itoke sare ya bao 1-1 dhidi ya Tanzania katika mechi ya kwanza ya kampeni ya kucheza Fainali za Kombe la Mataifa Afrika mwaka 2012 nchini Benin na Equatorial Guinea.


Katika mechi hiyo iliyochezwa Uwanja wa Mustapher Tchaker, mjini Blida, Stars iliyo nafasi ya 111 kwa ubora wa soka duniani ilianza kupata bao katika dakika ya 33 likifungwa na Abdi Kassim ‘Babi’ kwa mkwaju wa adhabu kabla ya Adlene Guedioura kuisawazishia Algeria katika dakika ya 45.
Kwa mujibu wa taarifa zilizopatikana leo usiku kupitia mtandao wa BBC, tayari Shirikisho la Soka la Algeria nalo limethibitisha kujiuluzu kwa Saadane na kusema sababu ni sare dhidi ya Stars.
Shirikisho hilo limeridhia uamuzi wa kocha huyo aliyeiongoza timu hiyo kucheza fainali za Kombe la Dunia kwa mara ya kwanza baada ya miaka 24 nchini Afrika Kusini.
Licha ya Saadane kuipeleka timu hiyo nchini Afrika Kusini, ikiwa katika kundi la C, Algeria iliishia hatua ya makundi baada ya kumaliza ya mwisho ikiwa na pointi moja, hivyo kuwa nyuma ya Marekani, England na Slovenia.
Viongozi wa Shirikisho la soka bado hawajasema nani atachukua nafasi hiyo kwa ajili ya kampeni hiyo ya kuwania tiketi ya CAN mbele ya Stars, Afrika ya Kati na Morocco.
Awali, kocha huyo mwenye umri wa miaka 64, alitaka kujiuzulu baada ya kutolewa mapema kwenye fainali za Kombe la Dunia, lakini aliamua kubaki baada ya kuongezewa mkataba wa miaka miwili.
Kabla ya kwenda nchini Afrika Kusini, Saadane ndiye aliiwezesha Algeria iliyo nafasi ya 33 kwa ubora duniani, kufika hatua ya nusu fainali katika fainali za Kombe la Mataifa Afrika zilizopigwa Januari mwaka huu nchini Angola.

Comments