Kocha: Kwa staili hii Zakia ni ndoto Madola, Bayi: Asipotia mguu India, RT kuwajibika


Na Tullo Chambo
KOCHA wa klabu ya Team 100 ya jijini Arusha inayommiliki mwanariadha mahiri wa Tanzania Zakia Mrisho, Zakaria Gwandu amebainisha kuwa licha ya mchezaji wake kuwa mzalendo na anayelipenda Taifa lake, itakuwa ndoto kushiriki michezo ya Jumuiya ya Madola huko India kama serikali haitamgharamia.

Mwanariadha huyo ambaye hivi sasa yuko nchini Italia chini ya Meneja wake, Gian Demadona, ushiriki wake katika mashindano hayo umezua utata, kutokana na pande kadhaa zinazohusika kutofautiana kimisimamo.
Akizungumza kwa simu kutoka Arusha jana, Gwandu alisema, riadha kwa Zakia ndio ajira yake na anamkataba nchini Italia, hivyo hataweza kurejea nchini Septemba 26 kuondoka na wenzake, kwani siku hiyo atakuwa akikabiliwa na mashindano mengine huko Italia.
“Zakia ni haki yake kushiriki Madola kwani amefikia viwango, pia ni mzalendo na analipenda Taifa lake, lakini kumbuka riadha ndio maisha yake, hivyo lazima aiheshimu, lakini hiyo Septemba 26 atakuwa na mchezo Italia, hivyo tumewaomba wahusika wafanye taratibu za kumtoa Italia hadi India, ikishindikana sidhani kama mimi au Zakia mwenyewe ataweza kujigharamia,” alisema Gwandu.
Kocha huyo aliongeza kuwa, haoni tatizo kwa Zakia kutumiwa tiketi huko alipo na kuhoji kitu kinachosababisha kuwahi India Septemba 26 ili hali ufunguzi rasmi ni Oktoba 3 na michezo ya riadha itaanza Oktoba 6.
“Mimi napenda nchi yangu, Zakia kabla ya Madola alikuwa na majukumu yake na baada ya Madola ataendelea na majukumu yake, nataka aende India kwa sababu ni haki yake, lakini ni baada ya Septemba 26,” alisisitiza Gwandu.
Kocha huyo aliongeza kuwa, kuhusiana na suala la mwanariadha huyo, aliwataarifu viongozi wa Chama cha Riadha Tanzania (RT), na kumkubalia lakini anasikitishwa na hali hii inayojitokeza sasa ya kumlazimisha arejee nchini na kuacha majukumu yake ya kimaisha.
‘Kimsingi nasisitiza na sitaki malumbano, Zakia hana tatizo kushiriki Madola lakini si kwa siku hiyo, kama ni mzuri wasimsumbue kwa hayo mambo, hana haja ya kuwahi, anawahi nini huko, aheshimiwe ajira yake,” alisema.
Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Kamati ya Olimpiki Tanzania (TOC), Meja mstaafu Filbert Bayi, alisema kuwa, haiwezekani kumtumia tiketi mwanariadha huyo huko aliko, kwani zimekatwa mojamoja kutoka India zikionyesha safari inaanzia Tanzania.
Bayi alifafanua kuwa, kama mchezaji huyo alikuwa na programu hiyo wangejulishwa tangu Juni mwaka huu ili taarifa zake ziweze kutumwa India kwa wandaaji kuonyesha hilo.
“Hawa jamaa walishindwa kutupa taarifa mapema, maana tumegundua kuwa hayuko nchini tulipoanza kambi Septemba Mosi, wakati tayari tulikuwa tumeaishafanya taratibu zote kuhusu safari hiyo,” alisema Bayi.Katibu huyo aliongeza kuwa, endapo mchezaji huyo atashindwa kurejea nchini kabla ya keshokutwa, Meneja wake Demadona itabidi amtafutie tiketi kumfikisha India na akigoma, RT itabidi iwajibike kwa kujibu hilo.
Kwa upande wake Rais wa RT, Francis John alisema, wao walimruhusu Zakia kwenda kwenye timu ya Afrika, ambayo ilishiriki mashindano ya mabara huko Croatia, lakini alipomaliza badala ya kurejea nyumbani akaunganisha Italia.
Rais huyo aliongeza kuwa, hawana ufafanuzi wa kutosha juu ya suala hilo, lakini ikishindikana mchezaji huyo kushiriki Madola watarejea na kukaa chini kuona cha kufanya.

Comments