GOR MAHIA YA KENYA YAJA BONGO

GOR MAHIA
TIMU ya Gor Mahia ya Kenya inatarajiwa kuja nchini kwa ajili ya kuvinoa vigogo vya soka nchini, Simba na Yanga, ambavyo vipo kwenye kampeni ya kusaka ubingwa wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara iliyoanza Agosti 21.
Awali, timu ya Ulinzi ambao ni mabingwa wa Kenya ndio walipanga kuja, lakini habari zilizopatikana leo jioni zilisema timu hiyo inayomilikiwa na Jeshi la Ulinzi, wamenyimwa ruksa hivyo Gor-Mahia wanakuja badala yao.
Kwa mujibu wa mratibu wa mechi hiyo, Phil Mmari, baada ya kuwakosa Ulinzi ilibidi wafanye mazugumzo na Gor Mahia ambao wameridhia kuja nchini kwa ajili ya mechi hizo mbili dhidi ya Simba na Yanga.
Alisema Gor Mahia itaanza kwa kucheza na Simba keshokutwa kwenye Uwanja wa Taifa kabla ya kwenda Arusha kucheza na Yanga kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid.
Mechi hiyo ni sehemu ya maandalizi kwa timu hizo ambapo Septemba 11, watashuka katika viwanja tofauti kucheza mechi za Ligi Kuu ya Vodacom kwa Simba kucheza na Azam FC kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam huku Yanga ikicheza na AFC mjini Arusha.

Comments