DAR ES SALAAM ALL SCHOOLS CONCERT JUMAMOSI

WANAFUNZI kutoka shule mbalimbali za msingi na sekondari za jiji la Dar es Salaam keshokutwa wanatarajiwa kushiriki katika tamasha maalum lijulikanalo kama ‘Dar All Schools’ lenye lengo la kusaka vipaji vya mpira wa kikapu na kucheza muziki litakalofanyika katika viwanja vya Posta, Kijitonyama jijini Dar es Salaam.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na mratibu wa tamasha hilo, Camillo Mhando kutoka kampuni ya A+Communications alisema kwamba lengo la tamasha hilo ni kuwakutanisha pamoja wanafunzi hao ili kuweza kuvumbua vipaji vipya, pia kuhamasisha wanafunzi wenye vipaji kuvitumia badala ya kukaa navyo.
"Hii ni maalum kwa ajili ya wanafunzi kutoka shule zote za Sekondari na msingi jijini Dar es Salaam na maeneo ya jirani. Tunajua siku kuu wanafunzi wangependa kuburudika, lakini burudani nyingi zinafanyika usiku. Kwa kutambua umuhimu wa wao pia kufurahi, ndiyo maana tumeona tuwape siku hii kwa burudani ya mchana," alisema Mhando.
Alisema mbali ya muziki na mpira wa kikapu, tamasha litakaloanza saa nne asubuhi hadi saa 12 jioni pia litaambatana na maonyesho maalum ya mavazi yatakayofanywa na wanafunzi na zawadi mbalimbali zitatolewa kwa wale watakaofanya vizuri.
Aliongeza kuwa wasanii mbalimbali wakiwemo Maunda Zorro, Steve R & B, Baby Boy, Kala Jeremiah na Niki wa Pili wanatarajiwa kupamba tamasha hilo ambalo limedhaminiwa na Sprite, PSI na TACAIDS ambapo kiingilio kitakuwa sh.2,000.

Comments