VODACOM PREMIER LEAGUE KUANZA LEO

MBIO za miamba 12 ya soka nchini za kuwania ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania bara, zinaanza leo huku mabingwa watetezi, Simba wakianza na African Lyon kwenye Uwanja wa Uhuru, jijini Dar es Salaam.


Watani wao Yanga, wakiwa na furaha ya ushindi wa mabao 3-1 dhidi ya Simba kwenye mechi ya Ngao ya Jamii, watakuwa wageni wa Polisi Dodoma Uwanja wa Jamhuri, Dodoma.

Ofisa habari wa Yanga, Louis Sendeu amesema kwamba, kikosi kamili cha Yanga kiliwasili salama mjini Dodoma lakini ikiwaacha nyoya wake kadhaa kutokana kuwa majeruhi.

Hao ni nyota wake wa kimataifa wa Ghana, Kenneth Asamoh, Abdi Kassim ‘Babi’, Kiggy Makassi na Shamte Ally na kusema jana jioni timu hiyo ilifanya mazoezi.

Alisema, wembe uliotumika kuinyoa Simba, Jumatano katika mechi ya Ngao ya Jamii, ndio watautumia kwa maafande hao wa Polisi Dodoma waliorejea Ligi Kuu msimu huu.

Sendeu alisema mkakati wao ni kuwa makini zaidi uwanjani ili kutopoteza hata mechi moja, hivyo kila mechi kwao ni muhimu kushinda.

Kwa upande wa Simba ambayo itaanza kampeni ya Ligi Kuu ikiwa na machungu ya kufungwa na mtani wake, wametamba kuwa hakuna timu ya kuwazuia kutetea ubingwa.

Nahodha wa Simba, Nico Nyagawa alisema kwamba wameshasahau yaliyotokea Jumatano na akili zao zote wanazielekeza katika Ligi Kuu, hivyo habari zaidi itapatikana huko.

“Sisi hatutaki kuandikia mate wakati wino upo, mambo yote yanaanza kesho (leo) tutawaonyesha tulichokuwa tunakifanya Zanzibar na mwisho wa siku watakubali na kutuheshimu,” alisema Nyagawa

Kama ilivyo kwa Yanga, timu ya Simba nayo itamkosa kipa wake namba moja, Juma Kaseja na Mussa Hassan Mgosi.

Mbali ya mechi hizo, ligi hiyo itaendelea kwenye viwanja vingine vinne kwa wageni wengine katika Ligi hiyo, AFC Arusha ambao watakuwa wenyeji wa Azam FC kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid.

Nayo Majimaji ya Songea itaanzia kampeni yake kwenye Uwanja wake wa nyumbani dhidi ya mabingwa mara mbili wa ligi hiyo, Mtibwa Sugar ya Morogoro.

Mtibwa Sugar iliyo chini ya Kocha Mkenya, Tom Olaba, imewahi kutwaa ubingwa huo mwaka 1999 na 2000, hivyo safari hii itakuwa ikisaka ubingwa wa tatu.

Aidha, timu ya Toto African ya Mwanza nayo itakuwa kwenye Uwnaja wa CCM Kirumba mjini Mwanza kuwakaribisha Ruvu Shooting ya Pwani huku Kagera Sugar ikiwakaribisha JKT Ruvu Stars katika Uwanja wa Kaitaba.

Comments