SIMBA, YANGA ZALALAMIKIA MAPATO KIDUCHU

MAOFISA HABARI WA SIMBA NA YANGA, CLIFFORD NDIMBO KUSHOTO NA LOUIS SENDEU KULIA WAKIZUNGUMZA NA WAANDISHI WA HABARI LEO

KLABU za Simba na Yanga zimetishia kujitoa katika ligi Kuu Tanzania bara kutokana na makato makubwa ya mchezo wa kuwania ngao ya Hisani kwa Shirikisho la soka Tanzania (TFF) kuingiza makato yanayohusiana na na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).
Wakizungumza kwa nyakati tofauti jana, Ofisa Habari wa Simba Cliford Ndimbo na wa Yanga walisema klabu zinaungana kupinga makato makubwa yanayofanywa na TFF.
Ndimbi alisema mchezo wa kuwania ngao ya Jamii uliochezwa Agosti 18 katika uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam uliingiza sh mil 222 ambako klabu hizo zimepewa asilimia 18 ya mapato fedha ambazo ni ndogo kutokana na maandalizi waliyofanya kabla ya mchezo huo.
Ndimbo alisema mapato ya asilimia 18 ya fedha hizo ni sh mil 33 ambazo hazitoshi kuendeleza klabu hizo ambazo maandalizi ya mchezo huo yalikuwa ni zaidi ya fedha hizo.
Ndimbo alisema TRA inatakiwa ikate mapato ya TFF na si klabu ambazo makato yake yatokane na nembo ya timu hizo ambazo zimejipanga kusajili nembo zake na kujiendesha kibiashara.
Aidha Ndimbo alisema kilio chao kinatokana na klabu hizo kujiendesha katika mtindo wa kusaidiwa ambako pia TRA nayo imeingia kabla ya kupewa tamko la kukatwa mapato katika michezo ya Ligi Kuu.
Ndimbo alitishia kujitoa katika ligi Kuu iwapo kama suala hilo halitowekwa sawa kwa sababu klabu hazitofaidika na lolote kutokana na kwamba hakuna biashara zinazofanywa na klabu hizo.
Alisema suala hilosi la Simba na Yanga peke yake bali hata klabu nyingine za Ligi Kuu zinahusika ingawa wao wameanza kulitolea tamko tatizo hilo.
“Tukirejea maandalizi mfano ya Yanga ambao waliweka kambi Bagamoyo, Simba nayo iliweka kambi Zanzibar, fedha zilizotumika ni zaidi ya sh milioni 33, hivyo tulivyopewa zote ziliishia mikononi kwa kulipia gharama mbalimbali,” alisema Ndimbo.
Ndimbo alisema kutokana na mpangilio huo ulioanza kufanywa na TFF inatakiwa wasake miradi ambayo itafanikisha maendeleo ya Shirikisho na si kusubiri mapato ya michezo na kukata makato makubwa.
Naye Sendeu alisema baada ya hatua hiyo kufikiwa na Wenyeviti wa klabu hizo juzi, watapeleka taarifa hizo TFF ili wabadilishe mfumo wa makato.
Sendeu alisema matatizo kama hayo yanatokana na udhaifu wa Umoja wa Klabu za Ligi Kuu Tanzania Bara (UTAFOC) uliokuwa chini ya Meja Jackson Lema ambao ulitakiwa usaidie masuala kama hayo.
Aidha Sendeu alifafanua kuwa maana ya mchezo wa Ngao ya Jamii ni kwamba fedha zinazopatikana zisaidie jamii mfano kama zingepelekwa hata Hospitali ya Taifa Muhimbili na nyingine zikagaiwa klabu lakini TFF wamekata makato mengine hata hayastahili.

Comments