SAA ILIVYOPANIA KUJIKWAMUA KIUCHUMI

WANACHAMA WA SAA WAKIWA KATIKA PICHA YA PAMOJA NA MENEJA MKUU WA KAMPUNI YA KONYAGI, DAVID MGWASA (WA TATU KUTOKA KUSHOTO WALIOKAAWE) WAKATI WA MKUTANO WAO MKUU WA MWAKA.

WAHENGA walisema umoja ni nguvu na utengano ni udhaifu. Hii inatokana na ukweli kuwa, chini ya umoja na mshikamano wa dhati katika harakati za kutafuta mafamafanikio, hakuna kinachoshindikana.
Kwa kulitambua hilo, wahusika wa fani ya ushehereshaji (MC’s), Upambaji, Upishi, Upigaji Muziki (Djs) wapigaji wa matarumbeta, wapigaji wa picha za mnato, picha za video na waoka keki, waliamua kuunda chama chao kiitwacho Sherehe Arts Association (SAA).
Lengo ni kuwa na sauti ya pamoja katika kusaka maendeleo ya shughuli zao kwa maslahi yao, chama na taifa kwani fani hiyo ni kama zilivyo nyingine.
Mwaka 2001 wadau wa fani hii, waliunda umoja wao na kusajiliwa rasmi mwaka 2003 chini ya Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) kwa mujibu wa sheria namba 23 ya mwaka 1984.
Lengo la kuundwa kwa SAA, ni kutoa elimu kwa wanachama wake katika nyanja kadha wa kadha kama za kijamii, ustadi endelevu wa fani zao.
MC Mackie Mdachi ambaye ni kati ya wakongwe wa fani hiyo nchini na mmoja wa Baraza la Walezi wa SAA, anasema semina hiyo itafanyika kwenye Hoteli ya Lunch Time.
Anasema tangu kuanzishwa kwa chama hicho, kimejikusanyia zaidi ya wanachama 70 ambao Jumapili wameandaliwa semina ya mwaka itakayotanguliwa na Mkutano Mkuu wa pili wa chama hicho.
Kwa mujibu wa Mdachi, semina hiyo itahusu masuala ya SACCOS kwa lengo la kuwaelimisha wanachama namna ya kujikwamua kiuchumi kwa maslahi yao na chama.
Mdachi anasema, mgeni rasmi katika mkutano huo utakaofuatiwa na semina, atakuwa ni Katibu Mtendaji wa BASATA, Ghonche Materego ambaye atafungua mkutano na kufungwa na wakili, Mose Kalua.
Kwa upande wa madhumuni ya SAA, Mdachi anasema ni kuinua, kustawisha na kuboresha hali ya wanachama wake katika kukidhi mahitaji yao ya kiuchumi, kijamii na kimazingira kwa misingi, kanuni na sheria za vyama vya ushirika.
Anasema pamoja na mambo mengine, kikubwa katika semika na mkutano wa Jumapili, ni kuwahamasisha wanachama wake kujenga tabia ya kujiwekea akiba kwa maslahi yao na chama.
Kwa lengo la kwenda na wakati, Mdachi anasema semina zao nyingi zimekuwa zikiongozwa na wahadhiri wa vyuo mbalimbali wakiwamo wa taaluma za itifaki, diplomasia, Sosholojia, Lugha/Kiswahili fasihi kutoka Baraza la Kiswahili Tanzania (BAKITA), Bara za la Kiswahili Tanzania na wataalamu wengine.
Kwa upande wa muundo wa uongozi, Mdachi anasema Mwenyekiti wa SAA ni MC Guydon Lukuwi ‘Zuma,’ Makamu ni MC Arcardo Nchinga na Katibu Mkuu ni Dj Emmanuel Urembo akisaidiwa na MC Elly Ngwalla huku Mweka Hazina akiwa ni Juliana Mtei.
Mdachi anasema, pia kuna kamati nyingine za ufanikishi kama Kamati ya masuala ya dharura iliyo chini ya Bi. Ahobokela Kalinga.
Aidha, kuna Kamati ya burudani inaongozwa na MC Tumaini Mwendembwa huku kamati ya Katiba ikiongozwa na MC Bryceson Makena.
Mdachi anasema pia kuna Baraza la Walezi wa chama linaloongozwana Jaji Mkuu wa Tanzania, Augustino Ramadhani, MC William Chitanda, MC Ahmad Chombo na yeye Mdachi.
Kwa upande wa ofisi, Mdachi anasema wanapatikana katika Hoteli ya Legho, Barabara ya Shekilango, Sinza wilayani Kinondoni.
Kuhusu malengo ya siku za usoni, Mdachi ansema ni kujenga kituo maalumu ambacho kitajumuisha ofisi za chama hicho, maduka, kliniki ya akina mama na watoto.
Mdachi anasema kama mipango yao itakwenda vizuri, jengo hilo litakuwa na ukumbi wa kisasa wa mikutano na kusema kwa sasa wapo kwenye harakati za kupatiwa uwanja kupitia ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni.
Mdachi anasema SAA ni chama kinachoendesha shughuli na majukumu yake kwa umakini mkubwa kwa mujibu wa katiba na kanuni zake ikiwemo kufanya chaguzi kila inapotakiwa.
Ukija kwa upande wa masuala ya kijamii, SAA imekuwa ikisaidia vituo mbalimbali vya watoto wanaoishi katika mazingira magumu na kusema wamekuwa wakifanya hivyo kila mwaka.
Mdachi anasema wanafanya hivyo kutokana na kuona umuhimu wa kufanya hivyo katika kusaidia kundi hilo kwani nao wana haki ya kupata mahitaji muhimu kama wengine watoto wengine.
Anasema kwa kutimiza wajibu huo wa masuala ya kijamii, SAA imekuwa ikipongezwa na BASATA kwani wamekuwa mfano wa kuigwa na wengine.

Comments