JKT RUVU YASHIKA USUKANI LIGI KUU YA VODACOM


TIMU ya JKT Ruvu ya Pwani, jana ilivuna ushindi wa pili tangu kuanza kwa Ligi Kuu ya Vodacom baada ya kuitandika Toto African ya Mwanza mabao 2-1, mechi iliyopigwa kwenye Uwanja wa CCM- Kirumba jijini Mwanza.
JKT Ruvu sasa inaongoza ligi hiyo ikiwa na pointi sita kwani katika mechi ya kwanza dhidi ya Kagera Sugar, ilishinda bao 1-0 kwenye Uwanja wa Kaitaba, mjini Bukoba.
Mabao yote ya JKT Ruvu jana yaliwekwa kimiani na Pius Kisambale katika dakika ya 40 na 76 huku lile la wenyeji Toto African likifungwa na Hussein Swedi.
Mbali ya mchezo huo, mechi nyingine ilikuwa kwenye Uwanja wa Majimaji mjini Songea ambapo wenyeji Majimaji walifungwa bao 1-0, ikiwa kipigo cha pili, kwani katika mechi ya kwanza, walifungwa 1-0 na Mtibwa Sugar.
Nayo Kagera Sugar ambayo ilianza kwa kipigo cha bao 1-0 kutoka kwa JKT Ruvu, ikicheza nyumbani jana ilizinduka na kushinda bao 1-0 dhidi ya Ruvu Shooting.
Aidha, maafande wa Polisi Dodoma wakicheza kwenye Uwanja wa Jamhuri, jana walitoka sare ya bila kufungana na Mtibwa Sugar.

Comments