CLOUDS TV KUZINDULIWA RASMI KESHO


UZINDUZI rasmi wa kituo kipya cha Televisheni cha Clouds unatarajiwa kufanyika kesho ambapo watazamaji watapata fursa ya kuangalia vipindi mbalimbali na muziki kutoka kituo cha kimataifa cha MTV Base.


Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari, hatua hiyo inafuatia Clouds Tv kupanua wigo wake wa burudani baada ya kusaini mkabataba na MTV Networks Africa, hivyo kuanzia leo watazamaji watapata nafasi ya kuburudishwa kwa masaa mawili ya vipindi vya muziki na mitindo na maisha kutoka kituo cha MTV Base.

Taarifa hiyo ilieleza kwamba burudani hiyo itakuwa ikipatikana jumatatu hadi jumapili kati ya saa 12 na saa moja usiku, pia kutakuwa na mwendelezo wa burudani kati ya saa nne na saa tano usiku katika siku za wiki ambapo vipindi hivyo vitatoa ladha mbalimbali za muziki na burudani kwa watazamaji vijana na wenye umri wa kati.

Baadhi ya vipindi hivyo ni pamoja na Run’s House, My Super Sweet 16, Pimp my Ride, African Allstars, MVP, Retrobase, The Official African Chart pamoja na 10 Bigest Tracks Right Now.
Mkurugenzi Mtendaji wa Clouds Entertainment inayomiliki Tv Clouds Joseph Kusaga alisema ushirikiano wa kibiashara baina yao na MTV Network Africa utawapa nafasi ya kuweza kupata muziki na vipindi vya burudani vilivyo na ubora wa hali ya juu.

“Tukiwa na uwezo mkubwa wa kuwafikia vijana wa Kitanzania katika burudani na sasa tunapojumuisha uwezo wa kimataifa na MTV Networks Africa ama kwa hakika Tanzania itaweza kupata burudani iliyobora kabisa na anuai toka pande zote mbili”, Alisema Kusaga.

Naye Makamu wa Rais na Mkurugenzi Mtendaji wa MTV Networks Africa Alex Okosi alisema wamefurahishwa sana na mafanikio hayo hadi kufikia kusaibniwa kwa mkataba huo wa ushirikiano baina yao na Clouds Tv ambao unawapa nafasi ya kuweza kuwafikia watazamaji wa Tanzania.

Comments