WANACHAMA YANGA KUISHITAKI KAMATI YA UCHAGUZI



HAMKANI hali ya mambo ndani ya klabu ya Yanga huenda isiwe shwari baada ya baadhi ya wanachama kupanga kwenda Mahakama Kuu leo kufungua kesi dhidi ya Kamati ya uchaguzi na kupinga matokeo ya uchaguzi mkuu wa Jumapili.


Hiyo inatokana na wanachama hao kutoridhishwa na mwenendo wa kamati hiyo siku ya uchaguzi wa viongozi wa klabu hiyo uliofanyika Julai 18 katika ukumbi wa PTA ambapo Lloyd Nchunga alichaguliwa kuwa mwenyekiti.

Akizungumza jana, mmoja wa wanachama wa Yanga, Nombo Hamis ‘Mzee wa Mpunga’, alisema wapo katika hatua za mwisho tayari kwa kufungua kesi hiyo katika Mahakama Kuu.

Alisema kamati hiyo ilishindwa kuratibu zoezi ipasavyo kiasi ambacho ilibidi mgeni rasmi, Naibu Waziri wa Habari na Utamaduni, Joel Bendera, kuamua kusimamia zoezi hilo badala ya kubariki na kuondoka.

Aliongeza kuwa kamati hiyo pia ilikiuka taratibu kwa kuamua kumpigia debe mmoja wa wagombea huku ikimkandamiza mgombea mwingine.

“Hata usimamizi wa upigaji kura haukuwa mzuri, kwani kuna watu walipiga kura zaidi ya mara mbili, wengine waliondoka na karatasi za kupigia kura na kwenda nazo mahala walipojisikia, pia wengine walielekezwa kuwapigia baadhi ya wagombea ambao hata hawakuwa chaguo lao,” alisema.

Comments

  1. Mimi sina la kusema kuhusu Yanga. Ila nakupongeza Dina kwa blogspot hii. Umeanza vizuri. Keep it up.

    ReplyDelete
  2. Nakubaliana na Anon wa kwanza, blogu yako ni nzuri. Ila naongeza SIMBA SC OYEEEE!!!!! Msechu.

    ReplyDelete

Post a Comment