SHY ROSE ATIA NIA KINONDONI

SHYROSE
MENEJA Uhusiano wa benki ya NMB, Shyrose Sadruddin Bhanji amejitosa kuwania nafasi ya ubunge jimbo la Kinondoni jijini Dar es Salaam kwa tiketi ya Chama cha Mapinduzi (CCM) kwa lengo la kuwa kiungo katika jamii ya Wana Kinondoni.


Akitangaza azma yake ya kuomba ridhaa kwa wanachama wa CCM katika taarifa yake kwa vyombo vya habari jana, Bhanji alisema kwa mtazamo wake neno ubunge kwa mwaka 2010 linahitaji tafsiri mpya kwani kwa sasa mbunge anatakiwa kuwa ni kiungo cha jamii badala ya kuwa mwakilishi wa jimbo.

Bhanji alibainisha mambo makubwa ambayo atayapigania kwa ari zaidi, nguvu zaidi na kasi zaidi ni elimu, afya, ajira kwa vijana, kupiga vita utumiaji wa madawa ya kuleta kwa vijana, kupigania haki za wasanii, kusaidia wajane katika kujikwamua kiuchumi na kuleta msukumo mpya kabisa katika masuala ya mahusiano na jamii ambayo kwa mtazamo wake eneo hili linahitaji msukumo.

Alisema sababu ingine iliyompa ujasiri wa kujitokeza katika nafasi hiyo ni kutokana na kauli mbalimbali ambazo zimekuwa zikitolewa na viongozi akiwemo Rais Jakaya Kikwete, za kuwataka wanawake kujitokeza katika kuwania nafasi za uongozi ili Tanzania iweze kufikia hatua ya kuwa na wabunge asilimia 50 wakiwa ni wanawake.

Shy-Rose amepata kuwa mwandishi wa habari wa magazeti ya Serikali ya Daily News, mtangazaji Televisheni ya Taifa (sasa TBC1), Meneja Uhusiano Shirika la Majisafi na Majitaka jijini Dar es Salaam (DAWASCO) na Mkuu wa Kitengo cha Mahusiano Benki ya NMB, nafasi anayoshikilia hadi sasa tangu mwaka 2006.

“Mwaka 2010 ni mwaka wa mabadiliko na ndio maana nimeona kwamba ili kila mwananchi kuweza kuwajibika, nafasi ya mbunge inahitaji kutafsiriwa upya ili iendane na wakati na matatizo ambayo yanayotukakabili wananch” alisema.

Comments