SAJNA - KICHWA KIPYA KWENYE MEDANI YA BONGO FLEVA

SAJNA

NI ukweli usiopingika kuwa wasanii wanochipukia kwenye muziki wa bongo fleva hivi sasa wameweza kuliteka soko la muziki huo kwa kiasi kikubwa kiasi cha kuwatia hofu nguli katika fani hiyo.


Diamond, Belle 9, Baby Boy, Roma, Wyfill Dav, pamoja na vijana toka kituo cha Tanzania House of Talent (THT) Amini, Barnaba, Buibui na Mataluma ni baadhi ya mfano huo.

Hata hivyo orodha hiyo haitakamilika bila kumtaja chipukizi mwingine anayekuja kwa kasi ya ajabu Faraji Twaha maarufu kama ‘Sajna’ ambaye singo yake ya ‘Iveta’ inakamata vilivyo katika chati za muziki hapa nchini.
Msanii huyo mwenye makazi yake jijini Mwanza, licha ya kuwa ni mwanafunzi wa kidato cha pili katika shule ya Sekondari Mlimani, Sajna anasema amejipanga vema kuwatumikia mabwana wawili kwa upande mmoja na atahakikisha anatenda haki kwa kila upande.

“Nimeamaua kufanya muziki huku nikiwa bado nasoma kwa sababu ninaamini ninao uwezo wa kufanya mambo yote kwa wakati mmoja, muziki una muda wake na masomo yana muda wake hivyo sioni kama kuna tatizo”, Anasema.



SAJNA

ALIPOANZIA:
Kabla ya kufika hapo Sajna alikutana na milima na mabonde ambavyo anaamini vyote ni sehemu ya maisha na hasa ikizingatiwa kuwa hakuna mafanikio bila ya kupata misukosuko.

Akiwa ameanza muziki miaka ya nyuma kwa kuigiza nyimbo za wasanii mbalimbali, Sajna alipojiona amekomaa kiasi cha kuingia studio alianza harakati zake hizo mwishowe alibahatika kuingia studio za A2P na kukutana na mtayarishaji wake Sam Timba aliyemrekodia kibao cha ‘Nadhifa’ uliotoka Desemba 2009.

Kibao hicho kilimtambulisha kiasi kidogo kwenye medani ya muziki wa kizazi kipya na katika Sandu George ‘Kid Bwoy’ ambaye ni mmiliki na mtayarishaji katika studio ya Tetemesha jitihada zake za kusaka kutoka zaidi alikutana na meneja wake ambaye baada ya kuridhishwa na kipaji alichonacho aliamua kusaini mkataba wa kusimamia kazi zake.

“Nilianza safari yangu ya kimuziki mwaka 2004 lakini mwaka 2010 ndiyo nimeona njia ya mafanikio yangu katika muziki hivyo naamini makubwa zaidi ambayo yatawafaa mashabiki wangu yanakuja”, Anasema.

Anaongeza kuwa baada ya kumwaga wino Tetemesha Records ndipo aliporekodi singo yake inayotamba sasa ‘Iveta’ na kisha kazi nyingine zitakazokuwemo katika albamu yake itakayojulikana kwa jina la ‘Iveta’ zikiendelea huku akipanga kuwashirikisha chipukizi wenzake Belle 9, Linah na Josefly.

Anazitaja baadhi ya nyimbo zitakazokuwemo kwenye albamu hiyo itakayokuwa tayari kabla ya kumalizika kwa mwaka nhuu ni pamoja ‘Iveta’ ‘Binadamu’, ‘Mbalamwezi’, ‘Subira’, ‘Roho Mbaya’, ‘Nadhifa’ na nyinginezo akiwashirikisha wasanii kama Belle 9, Linnah na Josefly.

Kama hiyo haitoshi Sajna anasema ili kuipa ladha na vionjo tofauti albamu yake atazitumia studio za Tetemesha (Kid bwoy), AB (Amba), Music Lab (Duke), Immortal Music Tris), A2P (Sam Timba), na MJ (Marco Chali)


SAJNA




KWA NINI IVETA:
Sajna anasema ‘Iveta’ ni hadithi ya kweli, iliyomtokea jamaa mmoja wa toka mkoani Kagera ambaye kwa sasa yupo jijini Mwanza akijihusisha na biashara ndogondogo ajulikanaye kwa jina la Elly, aliyekuwa na mpenzi anaeitwa Iveta.
Anasema jamaa huyo alikwenda jijini Mwanza kwa lengo la kutafuta maisha hivyo akapata mtaji kidogo na kuanza kufanya biashara ya kuuza miwa katika maeneo mbalimbali ya jiji hilo.

“Kutokana na pitapita alininifahamu hivyo siku moja alinifuata na kunihadithia kisa chake na kuniomba nimwandikie wimbo ambao aliamini utasaidia kumfikishia ujumbe mpenzi wake aliyemuacha Bukoba” Anasema Sajna.

Anaongeza kuwa, bila hiyana nilimuandikia mashairi papo hapo tena wakiwa wamesima tu njiani pia alimtengeneza kiitikio ambacho kinatumika katika wimbo huo.

“Kwa kweli alifurahi sana na hivyo alikuwa na shauku ya kuusikiliza wimbo wote pindi utakapokamiilika…niliongeza beti tatu na kisha kuingia studio, mwisho wa siku kitu Iveta kikatoka na ndio hivyo unasikia kinafanya vema”, Anasema.
Kiitikio cha wimbo huo kinasema hivi " Iveta kijijini ningojee mama, ningojee dia, huku mjini nakutaftia mama, nakutaftia dia".



MIKAKATI:

Kutokana na fani hiyo kuwa na ushindani mkubwa, Sajna anasema amejiandaa kikamilifu kwani kabala ya kujitosa katika medani hiyo alikuwa anajifunza kutoka kwa wengine na baada ya kuingia bado anaendelea kujifunza akiamini kuwa itasaidia kukabiliana na hali ya ushindani.
Anaongeza kuwa kipaji alichonacho, uwezo wa kutunga mashairi pamoja usimamizi mzuri wa meneja wake vinamfanya aamini kuwa ataweza kukabana koo na chipukizi nwenzake wanaofanya vema sasa na hilo limeanza kuonekana.
Akiwa na matarajio ya kuusomea zaidi muziki, msanii huyo anawashauri wasanii wenzake ambapo wanatafuta namana ya kutoka kutovunjika moyo katika safari yao hiyo kwani ipo siku watafanikiwa.
Msanii huyo ambaye shoo yake ya kwanza ilikuwa ni shindano la Miss Mwanza mwaka 2010 lililofanyika kwenye ukumbi wa Yatch Club mkoani humo anasema hakuopata woga wowote kupanda jukwaani na badala yake alipandwa na mzuka ambao ulimtia nguvu.

Comments