RICHARD TUNDA:KIFAA KINGINE TIP TOP CONNECTION, NI MDOGO WA MKALI WA BONGO FLEVA TUNDAMAN



RICHARD

MOJA ya singo zinazotesa kwenye medani ya muziki wa bongo fleva kwa sasa ni ‘Far Away’ ulioimbwa na Richard akimshirikisha Big Jahman.


Kukubalika kwa wimbo huo kunatokana na ujumbe ulimo kwenye wimbo huo pamoja na sauti tamu toka kwa wasanii walioimba hivyo kumfanya anayeusikiliza kutaka kuusikiliza tena na tena.

Hata hivyo wasanii walioimba wimbo huo si maarufu sana licha ya kuwahi kutoa nyimbo zilizowahi kufanya vema kwani Big Jahman amekuwa akifanya kazi pamoja na Akili the Brain anayemiliki Akili Records.

Leo namzunngumzia hasa Richard, msaniii wa mwanzo kujifunza katika kituo cha Tanzania House Of Talent (THT) ambaye anaendeleza ujuzi wake katika kundi linalofanya vema kwa sasa katika medani ya bongo fleva,Tip Top Connection.




Ni nani asiyekubali kwamba Tip Top Connection inazalisha, inaendeleza na kukuza wasanii wenye vipaji vya muziki vya kuzaliwa na si kujifunza?, basi amini tambua kwamba Richard anakipaji cha hali ya juu na ndiyo maana ameingia katika kundi hilo.

Kwa asiyefahamu, Tip Top inaundwa na wasanii mahiri na wasiochuja kwenye fani akiwemo Harid Tunda ‘Tundaman’, Kassim Mganga ‘Cassim’,Ahmed Ally ‘Madee’, Deso na ‘first lady’ wao Khadija Shaban ‘Keysha’.



RICHARD NI NANI?



Richard Ramadhan Tunda ni mdogo wa damu wa mmoja ya nyota wa kundi la Tip Top, Tundaman ambaye kwa wanaofuatilia muziki wa bongo fleva mwaka 2007 aliwahi kutamba na kibao cha ‘Marionse’.

Kabla ya kutoa ‘Marionse’ alitoka na ‘Limekushuka aliomshirikisha Mandojo na kurekodiwa studio za Baucha chini ya mtayarishaji Maneke, wimbo huo ulifanya vena na hata kutinga ‘Top 10’ katika vituo mbalimbali vya redio hapa nchini, hiyo ilikuwa mwaka 2005.

Richard ni msanii aliyepata kujifunza THT akiwa ni mmoja ya wasanii wa mwanzo kabisa kwani hata kina Mwasiti, Buibui walimkuta na hiyo ilikuwa mwaka 2004 na 2008 ambapo anasema anashukuru kazi zake zilikuwa zikikubalika na wakubwa wake wa kazi akiwemo mkurugenzi wao, Ruge Mutahaba.

Akiwa na THT mwaka 2006 walifika maofisa toka shirika la umoja wa mataifa la kuhudumia watoto (UNICEF) ambao walikuwa wanasaka wasanii wa Tanzania ambao wangeshiriki kuimba kwenye tamasha la kumuaga aliyekuwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa (UN), Koffi Annan lililotarajiwa kufanyika nchini Ethiopia.

“Liliendeshwa shindano pale THT na bahati nzuri mimi na Mwasiti tulifanya vizuri na hivyo kuunganishwa na Professa Jay na tulikwenda Ethiopia kutumbuiza katika tamasha hilo kubwa na la aina yake.

Anakumbuka tamasha hilo liliwashirikisha nyota wakali wa Afrika Angelique Kidjo na msanii toka Afrika Kusini Zola ambapo kwa kiasi kikubwa kazi yao ilikubalika na kupendwa na wasanii wenzao na hata watu mbalimbali.

Anasema katika tamasha hilo waliimba kibao kiitwacho ‘Taifa la kesho’ ,,pia kabla na baada ya tamasha hilo waliweza kutembelea sehemu mbalimbali za jiji la Ethiopia pia walipata wasaaa wa kuingia studio na kufanya kazi kadhaa.

Akielezea zaidi ziara hiyo anasema ilimpa uzoefu mkubwa pia alipata kuwaielezea Tanzania kwa wenyeji wao ambao wengi walimfahamu baba wa Taifa Mwalimu JK Nyerere.

“Lakini katika pitapita na stori zangu na watu wa huko kuna mmoja aliniulizia kuhusu Mwalim Nyerere nikamwambia alishafariki tamgu mwaka 1999...kwa kweli alilia sana”, Anasema.

Richard anasema waliporudi nchini hakukaa sana THT aliachana nako na kuendelea na shule huku akifanya muziki kama msanii wa kujitegemea.

Anasema kipindi hicho alikuwa anafanya muziki huku akisoma sekondari ya Mtakatifu Laurante ya jijini Dar es Salaam alipokomea kidato cha tatu mwaka 2008, kisa kuambatana na kaka yake nchini Afrika Kusini.

Anasema mwaka 2009 ilikuwa afanye mtihani wa kidato cha nne lakini aliona muziki ni muhimu kuliko masomo na kuamua kwenda Afrika Kusini kumsindikiza Tundaman aliyealikwa kwa ajili ya shoo pamoja na Madee.

“Sijui ni utoto au ujinga wangu...niliamua kuacha hata kufafanya mtihani ili niende Afrika Kusini si unajua tena?, kweli nilienda nao na nikaungana nao katika shoo, matokeo yake niliporudi Bongo shule ikawa basi tena”, Anaongeza.

Hata hivyo Richard anajutia kitendo cha kukacha masomo kwa kipindi kifupi alichokuwa amebakiza na kusema panapo majaliwa ya mwenyezi mungu atarejea darasani muda si mrefu.

“Unajua kila kitu ni elimu siku hizi hata huu muziki hauwezi kuufanya ukawa bora zaidi bila ya elimu...nipo katika hatua za mwishoni za kujipanga ili nirudi shule na mambo mengine yatakuja baadaye”, Anaongeza.

Kwa sasa msanii huyo yupo jikoni akipika albamu yake ya kwanza aliyopanga kuipa jina la ‘Fire’ atakayowashirikisha wasanii kama Big Jahman, Tundaman, Cassim, Madee na Sheta na bado vibao viwili ili kuikamilisha.

“Nitaiita jina la Fire (Moto) kutokana na nyimbo zote zitakazokuwemo zitakuwa kali kupita maelezo, huku zikipambwa na ladha tofauti kutoka studio za Sharobaro, Baucha na nyinginezo.

Mbali na kufanya albamu yake binafsi, Richard pia anashiriki katika kuandaa albamu ya kundi la Tip Top ‘Bado Tunapanda’ ambapo ameshiriki kuimba baadhi ya nyimbo zinazofuata baada ya uliobeba jina la albamu ambao hakushiriki.

Kuiva kwake katika muziki kunamfanya aambatane na kundi hilo lenye wasanii wenye sauti zenye mvuto wa aina yake katika ziara zake za kimuziki inazofanya sasa hivi ikiwemo ile ya utambulisho wa singo ya ‘Bado Tunapanda’ na tamasha la Fiesta. Pia ameshawahi kushirikishwa katika kazi za wasanii kadhaa



ALIPOTOKEA:

Kama kawaida msanii unapoanza lazima ukumbane na adha za kuingia studio, kudhulumiwea na mambo mengine yanaytokatisha tamaa, lakini kutokana na kudhamiria kwake kufanya muziki na pia kuwa na kipaji, hakuvunjika moyo.

Anasema, alikuwa akipata nguvu ya kujituma zaidi baada ya kluona makali na mafanikio ya kimuziki aliyonayo kaka yake Tundaman na kutaka afike na ikiwezekana kuzidi kiwango alichofikia.

Kwa hali hiyo Richard anasema hatarajii kuwa msanii mwenye mafanikio yatakayoisjhia hapa bongo tu bali anataka kuvuka mipaka ya bara la Afrika na Ulaya kwa ujumla.

Anamaliza kwa kuwashukuru Ruge, Tundaman, Meneja wa Tip Top Babu Tale na wasanii wote wa Tip Top, huku akiwaasha wasanii hapa nchini kuangalia mbele zaidi kwa kutovimba vichwa kwa mafanikio wanayoyapata.

Alizaliwa wilaya ya Kinonondi mnamo Februari 3, 1989 kwa baba Ramadhan Tunda afisa mstaafu wa serikalini na Mama Juliana Herman aliyekuwa daktari katika chuo kikuu cha Dar es Salaam (wazazi wake wote ni marehemu).

Alianza kupenda muziki tangu akiwa mdogo huku akivutiwa zaid na msanii wa marekani Craig David, Dully Sykes na Cassim kwa hapa bongo, huku shule ya msingi akiipata Karume alipomaliza darasa la saba mwaka 2004 na kisha kusoma sekondari ya mtakatifu Laurenti alipokomea kidato cha tatu.



WASIFU WAKE:

JINA: Richard Ramadhan Tunda

KUZALIWA: Februari 3, 1989 (Miaka 21)

ALIPOZALIWA: Kinondoni, Dar es Salaam

SANAA: Muziki wa Bongo Fleva

KUNDI: Tip Top Connection

Comments

Post a Comment