SIMBA KUVUNJA MKATABA NA PHIRI?


RAGE, MWENYEKITI WA SIMBA

KLABU ya Simba imepanga kumchukulia hatua za kisheria Kocha Mkuu wa timu hiyo, Mzambia Patrick Phiri ambaye ameshindwa kurejea kwa wakati na kuiandaa timu hiyo kwa ajili ya Ligi Kuu ya Bara iliyopangwa kuanza Agosti 21.


Kwa mujibu wa Mwenyekiti wa klabu hiyo, Ismail Aden Rage, watachukua hatua dhidi ya Phiri kwa sababu kukawia kwake bila sababu ya msingi, kunatibua maandalizi ya timu.

“Phiri amekuwa na matatizo ya kurejea kwa wakati pale anapokwenda kwao Zambia, tumevumilia vya kutosha, lakini akiendelea kuwa kimya, tutaangalia hatua za kuchukua kwa mujibu wa mkataba,” alisema Rage.


KIKOSI CHA SIMBA


Rage alisema Phiri akiwa Kocha wa kimataifa, alipaswa kuheshimu taratibu za mkataba, lakini amekuwa mwenye matatizo pale anapokwenda kwao Zambia hali ambayo inasikitisha.

“Inasikitisha kuona kocha wa kimataifa akishindwa kuheshimu mkataba, kama ataendelea kuwa kimya, tutafanya maamuzi mengine kwa mujibu wa mkataba,” alisema.

Rage alikwenda mbali na kusema wataketi na wanasheria kuangalia na ikiwezekana, watauvunja mkataba wa kocha huyo na kuelekeza nguvu upande mwingine.

Alisema katika kipindi hiki, timu hiyo itaendelea kuwa chini ya Kaimu Kocha Mkuu, Sillersaidi Mziray akisaidiwa na Selemani Matola na Amri Said.

Katika kujiandaa na ligi kuu, timu hiyo jana jioni ilikwenda Zanzibar kwa kambi ya muda kabla ya kurejea kwa mechi ya Ngao ya Hisani dhidi ya Yanga, itakayocheza Agosti 14.

Kwa mujibu wa Ofisa Habari wa klabu hiyo, Clifford Ndimbo, wachezaji wote wameondoka isipokuwa nyota watatu kutokana na sababu mbalimbali.

Nyota walioshindwa kwenda Zanzibar, ni George Owino George mwenye matatizo ya kifamilia na Emmanuel Okwi ambaye yu majeruhi.

Mwingine ni nyota wa kimataifa wa Uganda, Patric Ochan ambaye naye anakabiliwa na matatizo ya kifamilia.

Simba, mabingwa wa Bara mara 17 wa Bara, wamekwenda Zanzibar kujipanga kabla ya kuanza kwa Ligi Kuu kwa lengo la kutetea ubingwa wao waliotwaa msimu uliopita kwa rekodi ya aina yake.

Chini ya Kocha Phiri, Simba ilishinda mechi zote isipokuwa mbili ambazo ilitoka sare, hivyo kumaliza ligi hiyo ikiwa na pointi 62.

Comments