NCHUNGA, KIFUKWE WAMWAGA SERA YANGA


LLYOD NCHUNGA

WAKATI wagombea wa nafasi mbalimbali za uongozi katika klabu ya Yanga wakiendelea na kampeni zao wagombea nafasi ya mwenyekiti Lloyd Nchunga na Francis Kifukwe wamemwaga sera zao kwa wanayanga ili kuweza kuchaguliwa katika uchaguzi uliopangwa kufanyika Julai 18 kwenye ukumbi wa PTA.


Akizungumza na ofisini kwake leo, Nchunga ambaye ni mwanasheria alisema moja ya mikakati yake iwapo atachaguliwa ni kuunganisha makundi yote ya Yanga ili kujenga umoja, pia kutumia kamati mbalimbali kuratibu shughuli za Yanga.

Alisema anakusudia kuunganisha wanachama kupitia matawi ya Yanga na kurekebisha katiba ili kuwe na mtiririko wa mawasiliano toka matawi hadi kamati ya utendaji, pia kupeana zamu ya kushughulikia mechi za Yanga miongoni mwa matawi.

Kama hiyo haitoshi, Nchunga alkisema iwapo atachaguliwa ataanzisha SACCOS ya Yanga na hatimaye iwe benki, pia kuendelea kushirikiana na mfadhili wao Yusuf Manji na wadhamini wengine watakaojitokeza, sambamba na kulitumia eneo la klabu kiuchumi zaidi.


NCHUNGA

“Kauli mbiu yangu ni Umoja, ushindi na mafanikio kwa maslahi ya Yanga hivyo nawaomba wanayanga wenzangu kunichagua ili kuhakikisha Yanga inapiga hatua kubwa baada ya kuwa nyuma kwa muda mrefu”, Aliongeza Nchunga ambaye pia ni mjumbe wa Kamati ya nidhamu ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF).

Kwa upande wake Kifukwe aliyezungumza na waandishi kwenye hoteli ya Courtyard alisema iwapo atachaguliwa atawafanya wana Yanga wajivunie zaidi klabu yao kwa mambo mbalimbali pia kupanua wigo wa taasisi yetu, kwa kuanzisha mfuko wa akiba na mikopo kwa wanachama (SACCOS), ambao utakuwa ukitoa mikopo kwa wanachama wake, kupitia matawi.


FRANCIS KIFUKWE

Alisema kama atachaguliwa yeye pamoja na viongozi wenzake watasimamia kwa umakini, ukaribu na uadilifu
zoezi la uuzaji hisa za klabu, ili kuiongezea klabu uwezo wa kujitegemea, pia kuboresha mfumo wa uendeshaji wa klabu kwa kuunda Idara za kitaalamu kama Uhasibu, Utawala, Masoko, Ufundi, Sheria, Habari na Mawasiliano.

Kifukwe aliongeza kuwa katika uongozi wake kama atachaguliwa wataipitia upya Katiba na kuifanyia marekebisho ili kuwepo na Katiba imara, yenye nguvu itakayoletea tija kwani kwa sasa Yanga haina dira wala mwelekeo.

Pia kuleta umoja na mshikamano ndani ya klabu kwa kuondoa makundi na kuhakikisha Yanga inakuwa moja, upendo ili kuimarisha nguvu za kupambana na wapinzani.
“Haiwezekani mwanayanga adui yake, awe mwana Yanga, Umefika wakati tuiondoe hali hii, katika hili lazima tuyatazame upya matawi yetu na tuyaboreshe, ili kuyapa nguvu yawe matawi hai, si matawi mradi matawi”, Aliongeza.

KIFUKWE

Mbali na hao nafasi hiyo pia inawaniwa na Abeid Abeid, Mbaraka Igangula na Edger Chibura huku nafasi ya makamu mwenyekiti ikiwaniwa na Davis Mosha, Ayub Nyenzi na Costante Maligo, wakati wanachama 28 watawania nafasi nane za uju7mbe wa kamati ya utendaji.

Comments