MILOVAN KUMRITHI PHIRI SIMBA


AFISA TAWALA WA SIMBA EVODIUS MTAWALA KULIA NA OFISA HABARI WA CLIFFORD NDIMBO WAKINZUNGUMZA NA WAANDISHI WA HABARI


MABINGWA wa Tanzania Bara, Simba, wameanza mchakato wa kumrejesha kocha wao wa zamani, Mserbia Milovan Curcovic, kuinoa timu hiyo, akichukua nafasi ya Mzambia, Patrick Phiri.


Kwa mujibu wa Ofisa Tawala wa Simba, Evodius Mtawala, uamuzi huo umefikiwa na Kamati ya Utendaji iliyoketi juzi kujadili suala hilo na mambo mengine ya klabu hiyo.

Mtawala alisema Milovan aliyepewa mkataba wa miaka miwili, atawasili nchini wakati wowote kuanzia sasa na baada ya kufika ataungana na timu hiyo iliyopiga kambi Zanzibar kujiandaa kwa Ligi Kuu.

Kabla ya kuripoti rasmi kwa Milovan aliyewahi kuinoa timu hiyo, Simba itaendelea kuwa chini ya Kaimu Kocha Mkuu, Syllersaid Mziray

akisaidiana na Selemani Matola na Amri Said ‘Stam’.

Kabla ya kuanza kampeni ya kutetea ubingwa wake iliyoutwaa msimu uliopita kwa rekodi ya kushinda mechi 20 na sare mbili, Agosti 14 Simba itacheza na Yanga katika mechi ya Ngao ya Jamii.

Aidha, Mtawala alisema wamemtaka aliyekuwa kocha mkuu wa timu hiyo (Phiri) kueleza sababu za kukatisha mkataba wa kuinoa Simba ili kutochafua sifa yake ya ufundishaji.

Akifafanua zaidi sababu za kuachana na Phiri, Mtawala alisema ni baada ya kukwama kwa juhudi zao wa kumtaka arejee, kwani kila walipowasiliana naye, kocha huyo alisema alikuwa akishughulikia mambo yake binafsi.

Katika hatua nyingine, bonanza la klabu hiyo litakalofanyika Agosti 8, litakwenda sambamba na uzinduzi wa jezi za timu hiyo kwa msimu mpya,

tovuti, kalenda na kikosi cha msimu ujao.

Mtawala alisema katika bonanza hilo, kikosi cha kwanza cha Simba kitamenyana na Express ya Uganda huku Simba B ikicheza na Azam FC.

Comments