LUCY:MTOTO WA MAAFANDE, NYOTA WA FILAMU BONGO

LUCY
WIGO wa tasnia ya filamu za kibongo umekuwa ukitanuka kila kukicha kwa kuibuka kwa wasanii wenye uwezo wa hali ya juu cha kuleta ushindani mkubwa kwa wahusika ili kuweza kuliteka soko hilo.


Kama hiyo haitoshi, baadhi ya wahusika katika kuigiza filamu hizo wameamua kutayarisha wenyewe filamu zao na kwa hakika wamefanikiwa kwa kiasi kikubwa katika sekta hiyo wakiwemo kina Kanumba, Raymond Kigosi ‘Ray’ na mwanadada Lucy Komba.

Kwa leo tutamzungumzia Lucy Komba mwanadada alionyesha kuwa ‘wanawake tunaweza’ kwa kuamua kutayarisha mwenyewe filamu sambamba na kuinua vipaji vingine ambavyo kwa sasa vimekuwa gumzo katika tasnia hiyo.

Mbali na kuigiza na kutayarisha filamu Lucy pia anavipaji vya utunzi, sarakasi, kuimba ambavyo vinazidi kumuongezea maksi za kumfanmya awe mmoja ya wasanii wenye vipaji vya kipekee.

Katika mahojiano mwishoni mwa wiki iliyopita, Lucy anasema hakuingia katika fani hiyo kwa kubahatisha bali amedhamiria kufanya makubwa na ndiyo maana ameamua kufungua kampuni yake binafsi ya Poyaga Production ili kuzidi kutanua wigo wa dhamira yake.

Anasema kwa kudhihirisha hilo ameweza kuwaingiza katika ulimwengu wa filamu nyota mahiri wa wanaotamba sasa wakiwemo muigizaji wa vichekesho Mkwele, Ahmed Olotu ‘Mzee Chilo’, Irene Uwoya, Jacqueline Wolper, Dino, Godliver Vedasto, Mohammed Sultan na Hemed Kavu na wengineo.


LUCY


ALIANZA VIPI SANAA
Lucy anasema mwaka 2002 alipohitimu kidato cha nne alikuwa akivutiwa na tamthlia ya Mambo hayo iliyokuwa inarushwa na kituo cha Televisheni cha ITV na hasa mmoja ya wasanii wa kike aliyekuwemo katika kundi hilo Anne Constatine maarufu kama Waridi ndiye aliyemfanya atamani siku moja afikie kiwango kama si kuzidi.

Anasema kuna siku alikuwa anamsindikiza saluni rafiki yake akakutana na Tuesday Kihangala ‘Mr. Tues’ ambaye alimwambia kuwa anasifa za kuwa muigizaji lakini kutokana na woga alimwambia asingeweza na baada ya ushawishi wa muda mrefu alifanikiwa kunipeleka kuangalia wanaporekodia kazi zao kule Kinondoni na ndipo alipojiona anaweza.

Anaongeza pia alijitosa katika tasnia ya uigizaji baada ya kubaini uwepo wa mambo mengi yaliyopo katika jamii yanayokwenda mrama ambayo aliamini ili kuyaweka sawa yalihitaji kufanyiwa kazi kupitia njia hiyo.

“Pia niliamini kupitia fani hiyo ningeweza kubadilisha mwelekeo wa watu kuwa fani hiyo sio tu pekee inaweza kuwaletea ajira wahusika, pia inaweza kusaidia kuingiza mapato ya serikali, pamoja na kutangaza utalii wa nchi”, Anasema.

Anasema akiwa chini ya Mr. Chuz alikuwa ni mmoja ya wasanii waliounda kundi la Fukuto Arts na kazi ya kwanza ilikuwa ni igizo la ‘Valentine’s Day’ ambalo aliigiza pamoja na wenzake kama ‘Ndende’ na ‘Semolina’ na baada ya hilo ukafuata mchezo wa “Rangi ya Chungwa’.

“Kwa kweli siku nilipojiona kwenye runinga nikiigiza nilijisikia furaha sana sambamba na kujawa nguvu za kufanya makubwa zaidi katika fani hiyo na hii imeshaanza kuonekana kupitia kazi ninazofanya sasa”, Anasema.

Kutokana na kutopata maslahi ya kuridhisha Lucy na baadhi ya wasanii wenzake walijiengua Fukuto Arts na kuanzisha kundi la Dar Talents ambapo wakiwa katika harakati za kurekodi moja ya kazi zao za awali walikutana na Chrisant Mhenga ambaye aliwashauri wahamie Kaole.

“Kwa kweli nyota yangu ilianza kung’ara kutokana na umahiri niouonyesha katika kazi nilizofanya ikiwemo ‘Jahazi’, ‘Dira’ na mingineyo ambayo nashukuru kwa kiasi kikubwa vimeniwezesha kunipatia umaarufu ingawa anasema umaarufu huo haukumsaidia kumpatia maendeleo yoyopte”Anasema.

Huku akifanya kazi ya usanii alikuwa akisoma katika Chuo Cha Utumishi wa Umma kilichopo Magogoni, jijini Dar es Salaam na baada ya kuhitimu mwaka 2003 alipoajiriwa kama Katibu Muhtasi katika Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam.

Anasema katika kuweka kumbukumbu zaidi na mapitio yake alipiokuwa Kaole alijiwekea akiba ya kidogo alichokuwa akikipata na hivyo kuamua kujiendeleza kimasomo katika teknolojia ya habari na mawasiliano (IT) na baada ya kuhitimu aliaachana kabisa na Kaole na kujiajiri mwenyewe.



SANAA YAKE BINAFSI:

‘UTATA’ hii ni filamu yake ya kwanza kuitengeneza na hadithi aliiandika akiwa chuoni alipoipeleka kwa William Mtitu na alipoiangalia aliisifia kuwa ni nzuri hivyo kumshauri aiandikie script, alifanya hivyo na alipokamilisha alimpelekea na hadithi yake ya ujasiriamali ilianzia hapo.

“Mtitu alliniuliza kama nina fungu la kutosa, nami nikamwambia ninalo, hivyo kutokana na kuwa ndio nilikuwa naanza niliamua kuwatumia wasanii wazoefu kama Nurdin Mohamed ‘Chekibudi’, Ndumbangwe Misayo ‘Thea’ na msanii ambaye ilikuwa ni mara yake ya kwanza kuingia kwenye filamu Ahmed Olotu ‘Mzee Chilo’, Anasema.

Anasema anashukuru filamu hiyo ilipata mapokeo mazuri tangu ilipotoka mwaka huo 2006 mpaka sasa bado inaendelea kufanya vema katika soko la filamu hali ambayo anasema imechangiwa na ubunifu wake katika uongozaji ambao hulenga zaidi katika kuwafanya waigizaji wauvai uhusika ipasavyo na hasa kufuata mila na desturi za Mtanzania.

Mwaka 2007 alitupa sokoni kazi yake ya ‘Yolanda’ iliyokuwa na sehemu ya 1&2 ambapo filamu hiyo iliyokuwa ikihusu manyanyaso wanayopata wanawake wajane baada ya kufiwa na waume zao iliweza kukubalika ipasavyo kutokana na kugusa jamii.

“Filamu hii ndiyo ilimtoa Irene Uwoya na baada ya hapo nilitoa komedi ya’Vice Versa’, kabla ya mwaka 2008 kutoka na filamu ya ‘Zako Ama Zangu’ ambayo iliwaibua wasanii Jacqueline Wolper na Home Joshi.Pia nilitoa ‘Kipenzi Changu’ iliyowashirikisha Jacqueline Wolper na OM, Joshi na Tito , kisha mwaka 2009 nikatoa ‘Cleopatra’ sehemu ya 1&2”, Anaongeza.

Anaongeza kazi nyingine alizoziteneneza ni filamu ya Fedheha sehemu 1&2, huku akiendelea na matayarisho ya filamu mbili ‘Zaidi ya Rafiki’na ‘Twiniter Show’ambapo amewashirikisha wasanii chipukizi .



NJE YA SANAA
Mbali na sanaa Lucy akiwa ni muajiriwa wa Wizara ya Kazi na Katiba akiwa katibu Muhtasi , pia ni mama wa mtoto mmoja hivyo anaweza kujipanga vema ili kuhakisha anatimiza majukumu yake ipasavyo bila kulega upande wowote.

Alizaliwa Oktoba 24, mwaka 1980 jijini Dar es Salaam, akiwa mmoja ya watoto wa marehemu Francis Komba aliyekuwa mwajiriwa wa Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ) na mkewe, Marietha ambaye ni mwajiriwa wa Jeshi la Polisi.

Alipata elimu ya awali katika Shule ya St. Peter’s, Oysterbay na baadaye kujiunga na elimu ya msingi Shule ya Oysterbay. Na baadaye alimaliza elimu ya kidato cha nne na sita huko Olaleni na kisha sekondari ya Kibosho.



WASIFU:
JINA: Lucy Francis Komba
KUZALIWA: Oktoba 24, 1980
MAHALA: Dar es Salaam
KAZI: Wizara ya Kazi na Katiba
SANAA: Uigizaji

Comments