JK AMFARIJI DA SILVA NI BAADA YA BRAZIL KUTOLEWA WOZA


RAIS WA BRAZIL LUIZ INACIO LULA DA SILVA

RAIS Jakaya Kikwete amemfariji mwenzake wa Brazil, Luiz Inacio Lula da Silva, kuwa asivunjike moyo kwa timu yake kutolewa mapema katika fainali za Kombe la Dunia zinazoendelea nchini Afrika Kusini.


Kikwete alitoa pole hizo katika mkutano uliowakutanisha wajasiriamali wa Tanzania na Brazil, uliofanyika Hoteli ya Kilimanjaro Kempinski, jijini Dar es Salaam jana.

Kikwete hakusita kumweleza rais huyo wa Brazil kuwa Tanzania ni miongoni mwa nchi zinazoishabikia timu hiyo.

“Tanzania ni nchi mojawapo inayoshabikia timu ya Brazil katika mchezo wa mpira wa miguu, lakini kwa kutolewa mapema msikate tamaa,” alisema Rais Kikwete.

Alisisitiza kuwa Brazil kutolewa mapema katika mashindano hayo ni suala la kimichezo, hivyo wasikate tamaa kwa kuwa ajali hutokea wakati wowote na hivyo kufungwa kwa nchi hiyo ni kama ajali.

Barazil iliondolewa hatua ya robo fainali baada ya kukubali kipigo cha mabao 2-1 kutoka kwa Uholanzi.

Katika hatua nyingine, rais huyo wa Brazil alikabidhi vyeti na mataji kwa washindi wa jumla katika Maonyesho ya 34 ya Sabasaba ya Kimataifa.

Mshindi wa kwanza katika mashindano hayo ni Mfuko wa Hifadhi ya Jamii (NSSF), wa pili ni Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) na wa tatu ni Shirika la Viwanda Vidogo Vidogo (SIDO).

Comments