HUYU NDIYE NDUMBAGWE MISAYO 'THEA'


THEA

MVUMILIVU hula mbivu, walisema wahenga na unapotamka maneno haya mbele ya Ngumbagwe Misayo, maarufu kwa jina la utani Thea hakika atakupa ‘5’.


Kwa nini atakupa 5? Binti huyo amesota mno kabla ya kufanikiwa kutoka na kuwa msanii nyota na mashuhuri nchini katika sanaa ya uigizaji.

Katika mahojiano na Sayari, Thea anasema kwamba ilikuwa vigumu mno kwake kupata nafasi ya kutoka kisanaa, hadi ikafikia wakati akakata tamaa, lakini anamshukuru Mungu, mwishowe njjia ilifunguka.

Anasema ugumu ulitokana na mizengwe na hila zilizopo kwenye sanaa, kwa mfano ruishwa ya ngono na hata fedha wakati mwingine. “Katika vikundi vya sanaa ya magizo, kuna mambo mengi mabaya, ngono yaani usiseme, imetawala sana. Hata kuingia kwangu Kaole kwa kweli haikuwa kazi nyepesi, nilipambana na vitu kama hivi,”anasema Thea ambaye alijiunga na Kaole, Juni mwaka 2003 akitokea kundi la Mambo Hayo.

Anasema baada ya msoto wa mwaka mmoja, Thea anasema alifanikiwa kupata nafasi ya kucheza tamthiliya yake ya kwanza katika kundi la Kaole, iliyokuwa ikijulikana kama Sayari.

Kwa kupata kwake nafasi Kaole, kundi lililoasisiwa na wakongwe wa sanaa ya uigizaji Tanzania akina Mzee Kipara, Mzee Pwagu na Mama Haambiliki (sasa marehemu), anamshukuru sana Vincent Kigosi ‘Ray’. “Ray alipambana sana ajili yangu, alivutiwa na kipaji changu, alikuwa ananitetea nipewe nafasi, alikuwa anawaambia kabisa huyu dada anajua sana kucheza, mpeni nafasi, aliendelea hivyo, hadi ikafika siku nikapewa nafasi,”anasema.

Lakini Thea hakudumu kwenye kundi hilo, mwishowe alifukuzwa na kuhusu kutupiwa kwake virago anasema; “Mara tu baada ya kutoka kuonyesha michezo yetu kuopitia televisheni ya ITV na kuhamia TVT (sasa TBC1), ndio mimi nikafukuzwa na kiongozi mmoja wa Kaole kwa sababu zake binafsi, lakini nashukuru, walijitokeza watu kunitetea kwa mfano Bi Hindu na Kanumba, walinitetea na kushinikiza nirudishwe. Na kweli, siku moja nimekaa nyumbani nikapigiwa simu nirudi,”anasema.



Thea anasema maishani mwake akina Ray, Kanumba, Bi Hindu na Chiki ni watu wenye thamani kubwa, kwa sababu pengine bila wao asingefika popote.

Lakini kwa sasa Thea ameipa kisogo michezo ya kuigiza ya vikundi na kuelekeza nguvu zake kwenye uchezaji wa filamu- hivi sasa akiwa anatamba na filamu ya One By One, iliyotayarishwa na Mahsein Awadh ‘Dk Cheni’, msanii mwingine aliyekuwa naye Kaole.

“One By One, mimi ninakuwa mke wa Cheni, nakutana na misukosuko mingi, wazazi wake yaani mama yake anakuwa hanipendi, ananifanyia visa. Mdogo wangu naye anakuja kutembea na mume wangu hadi ananivurugia ndoa. Inakuwa balaa tupu, nisikumalize uhondo, itafute uinunue, tamu sana hii filamu,”anasema Thea.

Mbali na filamu hiyo, Thea anasema kwamba yuko kwenye matayarisho ya filamu mpya iitwayo Bed Rest ambayo amecheza na kaka yaike mwingine aliyeibuka naye Kaole, Ray sambamba na wadada wengine wawili aliokuwa nao kundi hilo pia, Mainda na Johari.

“Hii picha itakuwa nzuri sana na itawakumbusha watu mbali sana. Kwa sababu wewe hebu fikiria, mimi, Johari na Mainda halafu na Ray. Ni zaidi ya sinema hiyo. Yaani hii si ya kukosa, kwa wale wapenzi wetu tangu tupo Kaole, wajiandae kukipokea kitu hiki,”anasema Thea.



ALIPOTOKEA:

Thea, mtoto wa kwanza katika familia ya Matilda Misayo na Gaudence Urassa, alizaliwa miaka 27 iliyopita Shinyanga, kabla ya kuhamia Dar es Salaam na wazazi wake, ambako alipata elimu ya Msingi katika shule ya Mapambano, Sinza na baadaye kujiunga na sekondari ya Zanaki, alikosoma hadi Kidato cha Tatu kabla ya kuhamia Greens Victoria, alikohitimu kidato cha Nne mwaka 2001.

The anasema sanaa ya uigizaji ilikuwa kwenye damu yake tangu angali binti mdogo anasoma darasa la tano, alipokuwa akishiriki kwenye kikundi mcha sanaa cha shule na pia katika Kanisa Katoliki la Mwananyamala.

Akiwa kidato cha kwanza tu, Thea anasema alikwenda kujiunga na kikundi cha Mambo Hayo ambako hata hivyo baada ya kundi kusambaratika, akahamia Kaole.

Anawataja wasanii waliomvutia zaidi siku za mwanzoni kwamba walikuwa ni Suzanne Lewis anayejulikana kwa jina la sanaa kama Natasha, Jacob Steven au JB ambaye siku hizi anataka aitwe Amitabh Buchan wa Tanzania na wengineo.

Anakumbuka igizo lake la mwisho kucheza kundi la Kaole lilikuwa ni Baragumu mwaka 2005, alipoigiza kama mke wa mwanasiasa Mzee Magari, ambaye baadaye ankutana na kijana mkimbizi, Kanumba. “Yaani humo na mimi historia yangu inakuwa kama ni mkimbizi pia, kwa sababu naye Kanumba alikuwa mkimbizi mimi nikaamua kumsaidia, lakini mume wangu sasa, Mzee Magari akawa hapendi. akawa anafanya njama za kumfunga bila kujua kwamba alikuwa ni mtoto wake,”anasema.

Anataja baadhi ya filamu alizocheza hadi sasa ukiondoa By One na Bed Rest, kuwa ni Dadaz, Ukungu, Dunia Yangu, Revenge, Sigito, Tone la Damu, Why Me, Solemba, Born To Suffer, Simanzi ya Moyo, Trip To America na Out of Love.

Mshindi huyo wa tuzo ya Vinara mwaka 2008 kama mwigizaji bora wa kike, ni mama wa motto aitwaye Marlow Mpera, anayesoma darasa la pili katika shule ya msingi Diamond, Dar es Salaam.

Anazungumzia kupanuka kwa soko la filamu nchini kwa kusema kwamba, wasanii wanapaswa kuitumia vizuri fursa hiyo kwa kufanyaq kazi nzuri, ili waweze kuvutia wapenzi wengi. “Tukifanya kazi ili mradi tu iingie sokoni tupate fedha kwa sababu tuna majina makubwa, tutaharibu mambo,”anasema.



WASIFU WAKE:
JINA: Ndumbagwe Misayo
JINA LA UTANI: Thea
KUZALIWA: 1982
ALIPOZALIWA: Shinyanga
SANAA: Uigizaji

Comments