BUNDI AANZA YANGA SC


HAKUNA tafsiri nyingine, zaidi ya kusema baadhi ya wanachama wa klabu ya Yanga wameanzisha chokochoko ya kuleta vurugu katika klabu hiyo wakitaka kurudiwa kwa uchaguzi mkuu ulifanyika Julai 18 na kuusimika madarakani uongozi wa Lloyd Nchunga.


Kwa niaba ya wenzao, wanachama George ‘Castro’ Mpondela na Ibrahim Akilimali, wanataka kurudiwa kwa uchaguzi huo kwa madai kuwa, serikali iliingilia mchakato wake, kitu ambacho ni kinyume cha taratibu za kanuni za Shirikisho la soka la Kimataifa (FIFA).

Kwa mujibu wa barua ya Mpondela (kadi 000020) na Akilimali (kadi 000073), kwenda kwa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), wametaka pia Francis Kifukwe aliyekuwa mgombea wa nafasi ya uenyekiti, aombwe radhi dhidi ya shutuma za maneno ambazo zimemvunjia hadhi.

“Serikali imeingilia uchaguzi wa Yanga kinyume cha taratibu wa FIFA ( Shirikisho la Soka la Kimataifa), kwa hivyo uchaguzi urudiwe.

“Kauli za kushutumu mgombea kwa maneno ya majungu, ni kumvunjia heshima mgombea, hivyo ambwe radhi,” ilisema sehemu ya barua hiyo ambayo nakala yake imekwenda pia kwa Mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi ya Yanga, Jaji John Mkwawa.



Mpondela na wenzake wamebeza hata uteuzi wa Kifukwe kwenye Bodi ya Udhamini kwa kusema ni unafiki mtupu kwa sababu bado wanachama wa Yanga hawajatendewa haki ya kidemokrasia wana-Yanga na kusema kitendo hicho hakipaswi kupewa nafasi.

Kwa misingi hiyo, Mpondela na wenzake wanataka uchaguzi huo urudiwe chini ya usimamizi wa TFF huku serikali ikilipa gharama zake kwa sababu yenyewe ndiyo ilivuruga uchaguzi huo, hivyo kutokuwa wa huru na haki.

TFF imetakiwa kutoa ufumbuzi wa suala hilo, vinginevyo azma yao ya kwenda mahakamani, itabaki palepale hadi haki ipatikane na kusisitiza utezi wa Kifukwe kwenye Bodi ya wadhamini si suluhu.

“Tunaomba TFF itoe ufumbuzi wa jambo hili haraka, vinginevyo uamuzi wetu wa kwenda mahakamani utaendelea ili haki yetu ipatikane. Kuteuliwa kwa Kifukwe kama mdhamini wa Yanga siyo suluhu,” ilisisitiza sehemu mojawapo ya barua hiyo.

Kupitia barua hiyo, Mpondela na Akilimali waliokuwa kwenye kambi ya Kifukwe katika harakati za kusaka madaraka Yanga, wamesema wamefikia hatua hiyo kwa sababu uchaguzi huo uligubikwa na mizengwe, hivyo kutokuwa wa uhuru na haki.

Wazee hao wameshutumu pia kitendo cha Mfadhili wa klabu hiyo, Yusuph Manji kuagiza sharti la kiongozi ambaye angeshinda kumteua Kifukwe kuwa mdhamini na kusema hiyo ni kinyume cha utaratibu wa kuendesha soka kwa sababu huko ni sawa na kutaka serikali ya mseto.

“Kwenye uongozi wa mpira hakuna uongozi wa mseto kwani taratibu hizi hutumika kwenye nchi zilizogubikwa na utata wa uchaguzi, hivyo huundwa ili kukwepa gharama na machafuko zaidi, sisi tunataka uchaguzi urudiwe kwa sababu gharama si kubwa ikilinganisha na athari ya wanachama kuporaji wa haki.”

Mpondela na Akilimali wanakwenda mbali zaidi na kuhoji uhalali wa aliyekuwa Kaimu Mwenyekiti katika uchaguzi huo wa Julai 18, Ridhiwani Kikwete kumchukulia fomu Nchunga na kusema wakiwa kwenye kampeni, walielezwa Ridhiwani alikuwa akijinadi kuwa alitumwa na serikali.

“Siku ya uchaguzi, Ridhiwani aliingia ukumbini akiwa na Joel Bendera( Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni na Michezo).

“Katika ufunguzi wake (Ridhiwani) alisoma taarifa ya maandishi ya kumchafua mgombea (Kifukwe) na taarifa hiyo kuungwa mkono na Bendera, hivyo ni wazi serikali ilijihusisha.”

Wengine waliochaguliwa siku hiyo ni Makamu Devis Mosha na wajumbe zee Yusuph, Ally Mayay, Sarah Ramadhani, Salum Rupia, Tito Ossoro, Godfrey Mgondo na Theonest Rutashoborwa.

Mbali ya Kifukwe, uongozi huo mpya umewateua wajumbe watatu wa Kamati ya Utendaji ambao ni Mbaraka Igangula, Seif Ahmed Seif na Pascal Kihanga.

Comments