NYANDUDO KUPAMBA MIAKA 10 YA TWANGA PEPETA

MKURUGENZI WA ASET, ASHA BARAKA

MSANII wa muziki wa asili kutoka Kenya, Tonny Nyandudo anatarajiwa kupamba sherehe za kuadhimisha miaka 10 ya albamu na bendi ya African Stars ‘Twanga Pepeta’ zitakazofanyika Juni 27 kwenye viwanja vya Leaders, vilivyopo Kinondoni jijini Dar es Salaam.


Mkurugenzi Mtendaji wa African Stars Entertainment (ASET), Asha Baraka alisema kuwa maandalizi ya tamasha hilo yamekamilika na kutoa wito kwa wadau kujitokeza kwa wingi kuanzia saa mbili asubuhi ambako kutakuwa na maandamano yatakayoanza kwenye ofisi za kampuni hiyo, hadi kwenye viwanja vya Leaders Club Kinondoni.

Alisema waandamanaji watakuwa wamevaa sare maalumu kutoka kwa wadhamini wao kampuni za Vodacom Tanzania na Kampuni ya Bia Tanzania (TBL) watakuwa wamebeba mabango yenye ujumbe mbalimbali kama Malaria haikubaliki, kupiga vita ukimwi na uchaguzi wa amani.

Baada ya kufika Leaders kutakuwa na michezo mbalimbali ikiwemo utakaozikutanisha timu za Twanga FC na TASWA FC, kuvuta kamba na kufukuza kuku.

Mbali ya Nyandudo,wasanii wengine watakaokuwepo ni pamoja na Profesa Jay, ambaye ni Balozi wa Malaria nchini na Dully Sykes.

Pia wasanii waanzilishi wa bendi hiyo watakuwepo wakiwamo Mafumu Bilali ‘Bombenga’, Bob Gaddy, Adolph Mbinga, Ramadhani Masanja ‘Banza stone’, Luiza Mbutu, Abuu Semhando, Rogart Hegga na Hamisi Kayumbu ‘Amigolas’.

Burudani nyingine zitakazokuwepo siku hiyo ni kundi la mipasho la East African Melody, na bendi kongwe ya Msondo Ngoma ‘Baba ya Muziki’.

Katika tamasha hilo, wabunge wote wa majimbo ya Dar es Salaam wamealikwa, huku Mkuu wa Mkoa huo, William Lukuvi, akitarajiwa kuwa mgeni rasmi.

Bendi hiyo iliundwa kwa mara ya pili baada ya kuvunjika katika miaka ya mwishoni mwa 1980, huku ikiwa na wanamuziki 10 ambao ni Jesca Charles, Hamisi Kayumbu ‘Amigo’, Roggart Hegga, Banza Stone, Deo Mwanambilimbi, Bob Gaddy, Joseph Watuguru, Luiza Mbutu, Abuu Semhando na Adolph Mbinga.

Albamu hizo 10 ni ‘Kisa cha Mpemba’, ‘Jirani’, ‘Fainali Uzeeni’, ‘Chuki Binafsi’, ‘Ukubwa Jiwe’, ‘Mtu Pesa’, ‘Safari 2005’, ‘Password’, ‘Mtaa wa Kwanza’ na ‘Mwana Dar es Salaam’.

Comments

  1. twanga pepeta juu daima, mamapipiro mbona iron lady umemtoa vibaya?tafuta picha yake hata ya maktab
    Amina Tanga

    ReplyDelete

Post a Comment