TWANGA YALIA NA HUJUMA

WANENGUAJI WA TWANGA WAKIWA KAZINI
BAADA ya kuzidi kupata mafanikio katika medani ya muziki wa dansi hapa nchini, zikiwamo tuzo mbili za wimbo bora wa Kiswahili na bendi bora ya mwaka, baadhi ya watu wanaodaiwa kuwa na uwezo wa kifedha wako kwenye mikakati ya kuibomoa African Stars ‘Twanga Pepeta’.


Habari kutoka chanzo cha kuaminika zimedai kwamba matajiri hao wamejiunga katika kikundi na kupanga mikakati hiyo, ikiwamo kuwachukua wasanii nyota ambao ni waimbaji na marapa.

Chanzo hicho kilibainisha kuwa matajiri hao wamewapa ahadi nono ikiwamo ya kuwanunulia magari nyota hao sambamba na mengineyo mengi.

Wasanii hao wanaopigiwa hesabu ni Kalala Junior, ambaye ni mwimbaji, Saulo Ferguson, rapa na mwimbaji na rapa mahiri, Khalid Chuma ‘Chokoraa’.

Alipoulizwa jijini Dar es Salaam jana, Mkurugenzi wa Kampuni ya The African Stars Entertainment (ASET), Asha Baraka ‘Iron Lady’ kuhusiana na jambo hilo, alisema hata yeye amezisikia habari hizo, lakini hana uhakika na kudai kwamba endapo kama kweli wapo watu wamepanga kuibomoa Twanga wanajidanganya.

“ASET ni kisima cha burudani, yaani unaweza kusema ‘Alfa na Omega’ hivyo wakae wakitambua kwamba sisi wasanii wetu tumewajenga kimuziki na kifikra, kama wao wanaweza waunde wa kwao, lakini yote kwa yote hakuna atakayeweza kuiua bendi hii,” alisema.

Aliongeza kuwa hao ni matajiri wa msimu ndiyo maana wanajificha nyuma, hawataki kufahamika kama wanamiliki bendi na kuhoji, kwa nini wasijitokeze hadharani wakajitangaza kama wengine?

Asha alisisitiza kuwa endapo wanataka kuboresha tasnia ya muziki wa dansi nchini, wangefanya uboreshaji katika kuwalipa mishahara wanamuziki wanaowamiliki, kwani wengi wao wana hali mbaya kifedha na maisha kwa ujumla, kiasi hata wakiumwa wengi wamekuwa wakihaha huku na kule kutafuta misaada.



Mwisho.

Comments