SIMBA WALIVYOKAMIA KUTWAA KOMBE LA KAGAME KWA MARA YA SABA

BAADHI YA WACHEZAJI WA SIMBA
WAWAKILISHI wa Tanzania Bara kwenye michuano ya Kombe la Kagame mwaka 2010, Simba ya Dar es Salaam, leo wanatarajia kuanza kampeni ya kuwania ubingwa wa michuano hiyo inayofanyika Kigali Rwanda kwa kukipiga na mabingwa watetezi, Atraco ya huko.

Simba iliyowasili katika jiji la Kigali Ijumaa ikiwa na matumaini makubwa ya kufanya vema, hasa wakichochewa na hasira za kutolewa kwenye Kombe la Shirikisho la Soka Afrika (CAF) wiki iliyopita na Haras El Hodoud ya Misri, watakuwa wakipambana vilivyo kutwaa ubingwa..

Licha ya kutolewa kwa kuchapwa jumla ya mabao 6-3; wakifungwa mabao 5-1 katika mechi ya marudiano mjini Alexandria wakati huo wakitoka kushinda 2-1 kwenye mechi ya kwanza ya jijini Dar es Salaam, Simba wamejipanga vilivyo kusawazisha makosa.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti kabla ya kuondoka nchini, wachezaji wa timu hiyo walisema wanakwenda Rwanda wakitaka kutwaa ubingwa walau kuwafuta machozi wapenzi na mashabiki wa Simba na watanzania kwa ujumla.

Nahodha wa Simba Nicholaus Menard Nyagawa kwa upande wake alisema, wanakwenda Kigali kushindana na si kushiriki, hivyo watacheza kufa kupona kuhakikisha wanashinda mechi zao zote ili watwae ubingwa.

Alisema kutokana na kazi kubwa iliyofanywa na benchi la ufundi chini ya Kocha Mkuu, Patrick Phiri, kazi iliyobaki kwao ni kuyafanyia kazi mafunzo na maelekezo hayo waliyopewa wakiwa Misri baada ya kung’olewa kwenye michuano ya CAF akiamini wote watazingatia mafunzo hayo.

Kama hiyo haitoshi, Nyagawa anasema wanataka kurejea na ubingwa wa michuano hiyo kwa mara ya kwanza kutoka nje ya Tanzania kwani licha ya kulitwaa mara tatu, wamekuwa wakifanya hivyo michuano hiyo inapopigwa katika ardhi ya bara au Zanzibar.

“Mwaka huu tumejipanga kufanya vema, tumechukua ubingwa wa Tanzania Bara, bahati mbaya tukatolewa kombe la shirikisho sasa tumejipanga kuchukua Kombe la Kagame ili kuendekleza dhamira yetu,” alisema.

Naye mshambuliaji wakutumainiwa katika timu hiyo, Musa Mgosi ambaye ndiye mfungaji bora wa Ligi Kuu kwa msimu wa 2009/10, alisema kamwe hawatafanya makosa kwenye michuano hiyo ambapo pamoja na kuhakikisha wanatwaa ubingwa, Mungu akijalia atatwaa kiatu cha dhahabu.

“Tupo kamili kwa michuano ya Kagame tena morali ipo kwa hali ya juu baada ya maandalizi makubwa tuliyoyafanya kambini Misri, tunaomba Watanzania na Wanasimba kutuombea dua,” alisema.

Kwa upande wake kocha mkuu wa Simba anasema hana wasiwasi na kikosi chake, kwani maandalizi na ushiriki wao wa Kombe la Shirikisho umekisaidia kwa kiasi kikubwa kikosi hicho kufanya maandalizi ya michuano hiyo.

Phiri anasema kuondolewa kwenye michuano ya shirikisho, ni chachu ya wao kujipanga vizuri ikiwemo kusawazisha makosa yaliyojitokeza hata kufanya vibaya na anaamini yatawasaidia kufanya vema kwenye Kombe la Kagame.

Katika michuano hiyo, Simba imewaongeza wachezaji wapya iliowasajili kutoka klabu zinazoshiriki Ligi Kuu Tanzania Bara, Abdulhalim Humoud, kutoka Mtibwa Sugar ya Morogoro na Robert SSentongo kutoka African Lyon.

Wachezaji wengine ni Juma Kaseja, Deo Munishi, Salum Kanoni, Haruna Shamte, Juma Jabu, Kelvin Yondan, Joseph Owino, Jerry Santos, Juma Nyoso, Nicodemus Nyagawa, Ramadhan Chombo, Uhuru Suleiman, Mohamed Banka, Mohamed Kijuso, Musa Mgosi, Emmanuel Okwi, Mike Baraza, David Naftari na Jabir Aziz.

Katika michuano hiyo, Simba imepangwa kundi C pamoja na timu za Atraco, URA ya Uganda na Sofapaka ya Kenya huku APR ya Rwanda, TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Vital’o ya Burundi na Telkom ya Djibout zikipangwa kundi B.

Kundi jingine la C, litakuwa na timu za Rayon Sports ya Rwanda, St George ya Ethiopia na Mafunzo ya Zanzibar.

Kwa mujibu wa ratiba ya michuano hiyo inayosimamiwa na Baraza la Vyama vya Soka Afrika Mashariki na Kati (CECAFA), baada ya mechi yao ya leo itakayopigwa kwenye dimba la Amahoro, Simba itashuka dimbani tena Mei 20 kukipiga na Sofapaka kabla ya kuwakabili URA hapo Mei 23.

Aidha, wawakilishi wa Zanzibar timu ya Mafunzo ambao walianza kutupa karata yao ya kwanza jana jioni, mechi ya pili kwao itakuwa Mei 20 dhidi ya Rayon Sports kabla ya kuwakabili St. George ya Ethiopia.

Timu mbili za juu kwa kila kundi, ndizo zitacheza hatua ya robo fainali ya michuano hiyo ambapo bingwa atanyakua dola 30,000 za Marekani; mshindi wa pili dola 20,000 za Marekani na mshindi wa tatu dola 10,000 za Marekani.

Michuano hiyo ilianzishwa mwaka 1974 ikijulikana kama michuano ya Afrika Mashariki na Kati kabla ya mwaka 2002 kuanza kutambulika kama michuano ya Kagame kutokanana kufanyika chini ya udhamini wa Rais wa Rwanda Paul Kagame kuamua kuyadhamini mashindano hayo.

Aidha, michuano hiyo ambayo kwa mara ya kwanza ilifanyika nchini Tanzania huku ubingwa ukitwaliwa na Simba ambapo pia inaongoza kwa kunyakua ubingwa kwa kufanya hivyo mara sita, ikifika fainali mara 10.

Mwaka 1974 michuano hiyo ilifanyika nchini na Simba ikatwaa ubingwa kwa kuifunga Abaluhya ya Kenya kabla ya kufanya hivyo tena mwaka 1991 kwa kuifunga Villa ya Uganda mabao 3-0. Mwaka 1992, Simba ilitwaa ubingwa kwa kuifunga Yanga kwa penati 5-4 baada ya sare ya bao 1-1.

Mwaka 1996, ilitwaa ubingwa kwa kuifunga Express ya Uganda kwa mikwaju ya penati 5-3 baada ya sare ya bao 1-1 kisha kutwaa ubingwa huo mwaka 2002 kwa kuifunga Prince Louis ya Burundi bao 1-0.



UBINGWA TANGU 1974
1974 - Simba SC ( Tanzania)

1975 - Young Africans ( Tanzania)

1976 – Luo Union ( Kenya)

1977- Luo Union (Kenya)

1978 - Kampala City Council FC (Uganda)

1979 - Abaluhya FC ( Kenya )

1980 - Gor Mahia (Kenya )

1981 - Gor Mahia ( Kenya )

1982- AFC Leopards (Kenya)

1983- AFC Leopards (Kenya)

1984 - AFC Leopards (Kenya)

1985- Gor Mahia (Kenya)

1986 - Al-Merrikh

1987 - Villa SC (Uganda)

1988 - Kenya Breweries (Kenya)

1989 - Kenya Breweries (Kenya)

1990 - Haikuchezwa

1991- Simba SC (Tanzania)

1992- Simba SC (Tanzania)

1993- Young Africans (Tanzania)

1994 - Al-Merrikh (Sudan)

1995 - Simba SC (Tanzania)

1996- Simba SC (Tanzania)

1997- AFC Leopards (Kenya)

1998 - Rayon Sport ( Rwanda)

1999 - Young Africans (Tanzania)

2000 - Tusker FC (Kenya)

2001- Tusker FC (Kenya)

2002- Simba SC (Tanzania)

2003- Villa SC (Uganda)

2004 - APR FC ( Rwanda )

2005- Villa SC (Uganda)

2006- Police FC (Uganda)2

2007- APR FC (Rwanda)

2008-Tusker FC (Kenya) Uganda Tanzania

2009- ATRACO FC (Rwanda)

KWA HABARI ZAIDI SOMA TANZANIA DAIMA

Comments