SERIKALI YAUTAKA UONGOZI WA YANGA KUFANYA UCHAGUZI

SERIKALI kupitia Ofisi ya Msajili wa Vyama na Klabu za Michezo wilaya ya Ilala, imeiamuru klabu ya Yanga chini ya mwenyekiti wake Imani Madega kufanya uchaguzi haraka iwezekanavyo kwa mujibu wa katiba.


Kupitia barua namba IMC/UT/Y.I/Vol.V/29 ya Machi 24 kwenda kwa Katibu Mkuu wa Yanga, Laurance Mwalusako, uongozi unakumbushwa kwamba muda wa uongozi wa Madega ni Mei 30, hivyo hauna budi kutekeleza hilo.

Barua hiyo iliyosainiwa na Msajili Msaidizi, Shani Kitogo, inautaka uongozi wa Madega kuanza mchakato wa uchaguzi kwa mujibu wa katiba ya klabu hiyo.

“Naukumbusha uongozi kuwa muda wa mwisho wa kuwa madarakani ni 30/05/2010,” ilisema sehemu ya barua hiyo na kuongeza:

“Mnaombwa muanze kufanya mchakato wa uchaguzi kwa mujibu wa katiba yenye ridhaa yenu ili mpate viongozi wapya kuanzia Juni mosi,” aliongeza.

Agizo hilo limekuja huku baadhi ya wanachama wa klabu hiyo wakiushinikiza uongozi huo kuitisha Mkutano Mkuu kwa ajili ya kupatiwa taarifa mbalimbali ikiwemo ya mapato na matumizi.

Wanachama hao wakiongozwa na Kaisi Edwin wamelalamikia kitendo cha uongozi kutoitisha Mkutano Mkuu tangu uingie madarakani Mei 30, 2007.

Hoja ya wanachama hao ni kuwa uongozi huo haujawahi kuitisha Mkutano wa Mkuu isipokuwa mikutano ya marekebisho ya katiba.

Comments