ROSE JOHN NDIYE MISS DAR INTERCOLLEGE 2010

                                                                   
                    MISS DAR INTERCOLLEGE 2010 ROSE JOHN KATIKATI AKIWA NA MSHINDI WA PILI CASSIANA MILINGA KULIANA NA MARYLIDYA BONIFACE KUSHOTO ALIYETWAA NAFASI YA TATU
 
MAJAJI TUKIWA KAZINI
                                                               
AMINI NA BARNABA WAKITUMBUIZA
                                                        


ROSE JOHN

NYOTA ya jaha usiku ilimmulika Rose John (22) pale alipoweza kutwaa taji la Miss Dar Inter College lililofanyika kwenye klabu ya kimataifa ya Bilicanas baada ya kuwashinda wenzake 14.

Ushindi wa Rose haukuja kirahisi kutokana na ushindani mkubwa baina ya washiriki wa shindano hilo ambao karibu wote walikuwa na vigezo vinavyostahili hivyo kuwapa wakati mgumu majaji wa kuchagua nani zaidi.

MSHINDI WA PILI CASSIANA MILINGA

Kupitia shindano hilo warembo walipanda jukwaani kwa nyakati tofauti wakiwa katika mavazi ya ubunifu, kuogelea na jioni ambayo yalitanguliwa na shoo safi ya ufunguzi waliyoicheza.

Baada ya hatua hizo jopo la majaji likiongozwa na mwandaaji wa Miss Kinondoni ambaye alipanda jukwaani na kuwatangaza Aghatha Kilala, Joyce Baluhi, Rose, Cassiana Milinga na Marylidya Boniface, na kisha mchakato wa maswali ulianza.

MSHINDI WA TATU MARYLIDYA BONIFACE


Kila mrembo aliulizwa swali alilolichagua na kujibu kwa ufasaha kabla George kupanda tena jukwaa na kutangaza washindi ambapo nafasi ya pili ilinyakuliwa na Cassiana, nafasi ya tatu (Marylidya), huku Joyce akishika nafasi ya nne na Agatha akiwa wa tano.

Kwa ushindi huo Rose alizawadiwa sh mil.1.5, huku mshindi wa pili akipatiwa mil. moja, mshindi wa tatu alipewa 500,000, mshinmdi wa nne alipatiwa 400, 000 na mshindi wa tano (300,000), huku washiriki waliosalia wakipata sh 200,000 kila mmoja.

Aidha, Club ya Bilicanas iliyokuwa mmoja wa wadhamini wa shindano hilo nayo ilitoa ofa ya kuingia bure mwaka mmoja kwa mshindi wa kwanza hadi wa tatu, huku mshindi wa nne na wa tano wakipata ofa ya kuingia bure miezi sita na washiriki waliobaki walipata ofa ya kuingia bure katika klabu hiyo kwa miezi mitatu.

Akizungumza mara baada ya kutwaa taji hilo, Rose alisema haikuwa rahisi kwake kuamini kama angetwaa taji hilo kutokana na ushindani mkubwa uliokuwepo baina yake na washiriki wenzake ambao walikuwa na vigezo vinavyostahili kutwaa taji.

“Namshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuniwezesha kutwaa taji la Miss Dar Inter College, upinzani ulikuwa mkali na hasa ikizingatiwa washiriki wengi walikidhi vigezo vya kutwaa taji,” alisema Rose.

Mrembo huyo aliwashukuru waandaaji pamoja na wadhamini wa shindano hilo kutokana na zawadi aliyoipata ambapo alisema itamsaidia katika masuala yake ya kielimu.

Aidha, Rose aliwashauri wasichana wenye sifa za kushiriki mashindano mbalimbali ya urembo na hasa wasomi wa vyuo vya elimu ya juu kujitosa kushiriki katika mashindano hayo ambayo yanaweza kuwasaidia pia kuwapatia fedha za masomo pia kuiasa jamii kuachana na fikra ya kuona kwamba mashindano hayo ni uhuni.

Shindano hilo lilipambwa na burudani kutoka kwa Amin na Barnaba wa Tanzania House of Talent (THT) ambapo waliimba vibao vyao mbalimbali vikiwemo ‘Mbalamwezi’, ‘Robo Saa’, ‘Wrong Number’, pamoja na kuigiza nyimbo za msanii wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Papa Wemba.

Shindano hilo lilidhaminiwa na kampuni ya RBP Oil & Industrial Tz Technology, Gazeti la Tanzania Daima, Bilicanas, Redio Clouds, Vodacom Tanzania, Ndege Insurance, Fabak Fashion, Redd’s Original, Condy Bureau, Dotnata Decoration, Shear Illusion pamoja na blogu za Michuzi, Full Shangwe, Mtaa kwa Mtaa na Jane John5.

Comments