K'NAAN :Msomali aliyekula shavu World Cup 2010


WAVIN FLAG’ ni wimbo maalumu (official song ) utakaotumika katika fainali za Kombe la Dunia mwaka 2010, zitakazoanza kurindima Juni 11, nchini Afrika Kusini.


Licha ya kuwa wimbo huo kuwaingia vichwani mashabiki na hata wasiokuwa mashabiki wa soka duniani kutokana na mvuto wa aina yake, ni mwimbaji wa wimbo huo ambaye si mwimbaji maarufu sana kama ilivyozoeleka katika matukio makubwa, kutumia wanamuziki wenye majina makubwa na wanaofahamika.

Anajulikana kama K’Naan, ndiye aliyepewa shavu la kuimba wimbo huo ambao pia unatumika katika matangazo ya wadhamini wa kombe hilo, Kampuni ya vinywaji baridi ya Coca -Cola.

Keinan (Msafiri) Abdi Warsame, ndilo jina lake halisi. Alizaliwa Mei 30 mwaka 1978 mjini Mogadishu, nchini Somalia ambako alikulia mpaka mwaka 1991 alipoihama nchi yake kutokana na vita ya wenyewe kwa wenyewe na kukimbilia katika Jiji la Toronto, Canada anakoishi hadi hivi sasa.

Ni miongoni mwa wanamuziki wenye asili ya Afrika wanaofanya vema katika medani ya muziki, babu yake Haji Mohamed alikuwa mshairi huku shangazi yake, Magool alikuwa ni mmoja wa waimbaji maarufu nchini Somalia.

Katika maisha yake ya utotoni ili kujiepusha na mabalaa alikuwa akisikiliza tungo za hip hop alizotumiwa na baba yake kutoka nchini Marekani, ambaye alitimkia huko akimuacha akiwa bado kinda. Akiwa na miaka 13 K'naan, mama yake, kaka yake mkubwa Libann na mdogo wake wa kike, Sagal waliondoka Somalia na kwenda kuungana na ndugu zao wengine huko Harlem, walipokaa kwa muda mfupi kabla ya kuhamia Toronto.
Muziki
K'naan alianza kujifunza lugha ya Kiingereza kupitia nyimbo za wasanii wa hip hop kama Nas na Rakim, licha ya kutoifahamu ipasavyo lugha hiyo, aliweza kukariri mashairi ya nyimbo hizo kwa lugha yake kabla ya kuanza kufokafoka (kurap)
Mwaka 2006 alishinda tuzo za Juno kama rekodi bora ya rap, pia aliteuliwa kuwania tuzo za Polaris Music Prize kabla ya mwaka 2007 aliposhinda tuzo za BBC Radio 3 kama mwanamuziki anayechipukia.
Mwaka 2008 alijikita katika ziara ya kutangaza albamu yake sambamba na kutangaza albamu yake iliyokuwa mbioni kutoka, iliyokwenda kwa jina la ‘Troubadour’, ambayo ilikuwa chini ya lebo ya A&M/Octone, ambayo inafanya kazi na wasani kama Nelly Furtado, Mos Def, The Roots, Dead Prez na Pharoahe Monch.
Albamu
My Life Is A Movie (2004), The Dusty Foot Philosopher (2005) na Troubadour (2009), ambapo amewashirikisha wasanii mbalimbali katika kazi zake.

Comments