HUYU NDIYE JACKSON GEORGE WA BSS 2009

“TANO BORA (Top Five) ya Bongo Star Search 2009 itakuwa moto wa kuotea mbali katika medani ya muziki hapa nchini”.

Hiyo ni kauli ya mshindi wa nne wa shindano la kusaka nyota wa muziki (BSS) kwa mwaka jana, Jackson Geoge aliyoitoa hivi karibuni katika mahojiano maalum na Mnyamwezi Halisi.
Jackson ametoa kauli hiyo kufuatia dhana iliyojengeka vichwani mwa watu kuwa washiriki wa shindano hilo na hasa washindi wa nafasi za juu wa shindano hilo hushindwa kuendeleza ama kuendelzwa vipaji vyao.

Hali hiyo imedhihirika katika misimu miwili iliyopita yaani tangu kuanza kwa mashindano hayo yaliyojizolea umaarufu ambapo washindi hao wameishia kufanya mambo mengine zaidi ya sanaa.

Hata hivyo ni wachache miongoni mwao wametutumua kwa kujaribu bahati zao kwenye ‘game’ lakini hata hivyo wameshindwa kufurukuta kwa kiasi kikubwa katika medani hiyo iliyojaa ushindani mkubwa nchini.

Jackson anasema washiriki wa BSS 2009 watafuta dhana hiyo kwani wamedhamiria kuushangaza umma kwa kutayarisha kazi nzuri na zenye ujumbe ambazo ziatadhihirisha uwezo wao.

Kwa kudhihirisha hilo nadhani umeona ama kusikia kazi zetu tulizoziacghia hewani ambazo ni sehemu ya ujio wetu katika ‘game’ la bongo fleva”, Anasema Jackson.

Kwa kuanzia tayari nyota wanne kati ya walioshika nafasi tano za juu katika shindano hilo wameshakamilisha albamu ya pamoja ambayo inatartajiwa kuingia sokoni Machi 15.

Nyota hao ni pamoja na Pascal Cassian (mshindi), Peter Msechu (mshindi wa pili), Jackson (wa nne) na Beatruce William alitekuwa watano.

Kazi ya kutayarisha albamu hiyo imefanywa na kusimamiwa na studio za Master J huku kila mmoja akiingiza nyimbo mbili ambapo tayari kila mmoja ameachia kazi moja hewani na kazi hizo zimeonekana kufanya vema.

Baadhi ya nyimbo hizo ni pamoja na Nimechoshwa, kuagana (Jackson), Hasira Hasara,Maneno (Msechu),’Usinichoke (Cassian) na ‘tunajituma (Beatrice).

Jackson anakwenda mbali zaidi na kusema kuwa mbali na kazi hiyo ya pamoja tayari ameshandaa nyimbo nyingi ambazo ataziweka katika albamu yake binafsi na ameshaanza kuifanyia matayarisho.

Anasema, licha ya kuwa muziki wa bongo fleva kwa sasa upo katika ushindani wa hali ya juu anaamini anakipaji kikubwa cha kuweza kukabiliana na changamoto hizo ili kuweza kufanya vyema.

Anajiridhisha kwa hilo kwa kusema kuwa ametunga nyimbo ambazo zina ujumbe mahususi kwa jamii, zisizochuja masikioni mwa watu hivyo anaamini hiyo ni moja ya nyenzo ya kumfanya msanii adumu katika medani hiyo.

“Nashukuru kupitia shindano la BSS nimeweza kutambulika vizuri na hata mashabiki walitambua kipaji changu ndio maana walinifikisha hapo nilipokuwa…hivyo nataka kuwaonyesha kuwa nina kipaji si kulazimisha”, Anasema.
Aizungumzia shindano lilivyokuwa, Jackson ambaye aliuwakilisha mkoa wa Arusha anasema lilikuwa na ushindani mkubwa kutokana na washiriki wengi kuwa na vipaji vya hali ya juu.
“Kadiri siku zilivyosonga nilizidi kuona ushindani ukiongezeka huku na mimi nikijibidiisha katika mazoezi…namshukuru mwenyezi mungu kwa kuniwezesha kufika nafasi ile”, Anaongeza.
Licha ya mshindi wa pili (Msechu) kudai kuwa hamkubali mshindi (Cassian) huku akiapa kumfunika katika ‘game’, Jackson yupo tofauti kwania nasema “nilikuwa nikimkubali Cassian tangu tunaanza masjhindano na hata alipotangazwa kuwa ndio mshindi nilifurahi”, Anaongeza.

Jackson kwa sasa anaendelea na kuatayarisha kazi zake huku akisubiri majibu yake ya kidato cha sita baada ya kufanya mtihani mwezi februari mwaka 2010 kwani alishiriki akiwa kidato cha sita.

Kihistoria, alizaliwa Februari 14 mwaka 1990 huku Moshi, Kilimanjaro na alipata elimu yake ya msingi katika shule ya Kijenge, kabla ya kujiunga na Sekondari ya Lemara mwaka 2004-2007 na kisha alijiunga na sekondari ya Edmund Rice aliposoma kidato cha tano na sita mwaka 2008-2010 akichukua mchepuo wa HGL.

Comments