Yanga waifuata Fc Lupopo

kikosi cha Yanga
TIMU ya soka ya Yanga ilitarajiwa kuondoka usiku wa kuamkia ijumaa kwenda Lubumbashi, DRC kwa ajili ya mechi ya marudiano ya Ligi ya Mabingwa wa Afrika baina ya Yanga na FC Lupopo ya DRC itakayopigwa keshokutwa.


Akizungumza kwa njia ya simu jana, Afisa habari wa Yanga, Louis Sendeu alisema kwamba msafara wa watu 26 ukiongozwa na mwakilishi wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Kitwana Manara, kilitarajiwa kuondoka ndege ya shirika la Kenya (KQ).

Sendeu alisema kikosi chao kimejiandaa vema na mchezo huo ili kuahikisha kinaibuka na ushindi mnono ambao utaiwezesha timu hiyo kusonga mbele.

Hata hivyo Yanga inahitaji ushindi wa zaidi ya mabao 2-0 ili kusonga mbele kwani katika mechi ya awali iliyopigwa hapa nchini walifungwa mabao 3-2.

Aliwataja wachezaji walioondoka , Yaw Berko, Obren Curcovic, Shadrack Nsajigwa ‘Fuso’, George Owino, Athuman Idd ‘Chuji’,Nadir Haroub ‘Cannavaro’, Nurdin Bakari na Abdi Kassim ‘Babi’, Kigi Makasi, Jerry Tegete, Mrisho Ngasa, Wisdom Ndhlovu, Godfrey Bonny, Shamte Ally, Steven Bengo, Boniface Ambani.

Viongozi ni pamoja Mwenyekiti, Iman Madega, Katibu Mtendaji, Lawrance Mwalusako, Godfrey Mwenje (Katibu Mipango), Emmanuel Mpangala(Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili), Kocha Mkuu, Kostadin ‘Clinton’Papic, Kocha Msaidizi, Kenneth Mkapa na Daktari, Sheki Mngazija.

Comments