Uchaguzi mkuu kuwatoa Wagosi wa Kaya

KIMYA kingi kina mshindo, hiyo ni kauli iliyozoeleka masikioni mwa watu ikimaanisha kwamba kukaa kimya kunamaanisha mambo makubwa yanakuja.

Msemo huo umedhihirishwa na moja ya makundi yaliyoasisi muziki wa kizazi kipya nchini, Wagosi wa Kaya ambalo tangu lijikite katika medani hiyo limekuwa likitoa vibao vinavyoigusa jamii kwa namna moja ama nyingine.

Kundi hilo ambalo liliasisiwa miaka kumi iliyopita mjini Tanga, linaundwa na wasanii wawili, John Simba ‘Dk John’ na Fred Maliki ‘Mkoloni’ ambapo vibao vyao vya awali kama ‘Tanga Kunani’, ‘Wauguzi’ na vinginevyo walivyovitoa mwaka 2001 viliwaweka katika medani ya muziki.

Lakini kama ilivyo mazoea baada ya mafanikio wanayoyapata wasanii wanaokuwa kwenye makundi, hutokea msigano ama kutengana kimaeneo hivyo hupelekea kundi kuvunjika kabisa ama kutengana kwa muda, hali iliyolikumba pia kundi la Wagosi wa Kaya.

Kwa karibu miaka mitatu wasanii wa kundi hilo kila mmoja amekuwa akifanya kazi nje ya kundi, lakini kutokana na mwaka huu kuwepo kwa uchaguzi mkuu wa rais na wabunge, wasanii hao wameamua kuungana tena na kutoa albamu maalum inayozungumzia uchaguzi huo.

Katika mahojiano na mwandishi wa makala hii hivi karibuni, mmoja wa wasanii wa kundi hilo, Mkoloni alisema kuwa wanaandaa albamu maalumu inayohusiana na uchaguzi ambapo wanatarajia kuitambulisha siku zitakapozinduliwa rasmi kampeni za uchaguzi 2010.

Anasema tayari wamekamilisha kibao walichokiita ‘miaka kumi ya maumivu’ wakimshirikisha msanii toka kundi la TMK Wanaume, Chegge na kurekodiwa katika studio za Fish Crab chini ya mtayarishaji, Lamar na unatarajiwa kutoka wakati wowote kuanzia.

Aliongeza kwa kusema tayari wametayarisha singo nyingine iitwayo ‘mjumbe hauawi’ ambayo watawashirikisha Mrisho Mpoto na Kalapina kutoka kundi la Kikosi cha Mizinga.

Mkoloni anasema pamoja na kurejea kwa ajili ya uchaguzi huo, pia kundi lao limeamua kuzinduka kwa ajili ya kuokoa hali ya muziki hapa nchini ambayo imekuwa ikizorota kila kukicha na hiyo inatokana na matabaka yaliyomo baina ya wasanii wenyewe.

Anasema matabaka hayo yamechangia hata waandaaji wanaotoa tuzo za wasanii kushindwa kutofautisha aina ya muziki ama mtindo wanaotumia kiasi cha kuwachanganya wadau na kuwafanya wasanii kuonekana hawana maana.

“Tumerudi tena ili tuitoe hali hii na ni lazima mashabiki waungane katika kuondoa matabaka haya…hebu ona imefikia watayarishaji wa tuzo wanampatia tuzo Mpoto (Mrisho) kama msanii bora wa bongo fleva wakati haimbi wala kurap”, anasema.

Kuhusiana na kuibuka kwa studio za kutayarisha muziki kila kukicha, Mkoloni anasema hali hiyo haisaidii kukuza muziki kwa sababu si yo kila mtu anaweza kutengeneza sauti nzuri, lakini wapo baadhi wenye vipaji ambao wanaweza kutayarisha nyimbo nzuri.

Kwa ushauri wake Mkoloni anasema “Hakuna anayekatazwa kufanya muziki lakini ni kweli mtu ana kipaji alichobarikiwa na Mwenyezi Mungu, unajifunza au unaiga? Kuna watu wanatengenezwa hivyo ukiwaacha matokeo yake wanapotea kabisa kwenye fani,” anaongeza.

Kundi la Wagosi wa Kaya lilianzishwa mwaka 1999 Tanga, ambapo walianza kurekodi mwaka 2000 lakini walianza kusikika mwaka 2001, ambapo vibao vya ‘Tanga Kunani’, ‘Wauguzi’, ‘Wakulima’ na vinginevyo vilikuwemo katika albamu yao ya kwanza waliyoipa jina la ‘Tanga Kunani’ waliyoitoa mwaka 2001.

Mwaka 2003 walifyatua albamu ya pili ‘Ripoti Kamili’ iliyobeba vibao kama ‘Trafiki’ ‘Soka la Bongo’, ‘Safari Zetu’ na nyinginezo, huku mwaka 2005 walitoka na albamu waliyoipa jina la ‘Nyeti’ iliyobeba nyimbo kama ‘Nyeti’, ‘Kiinua Mgongo’, ‘Ushauri wa Bure na nyinginezo.

‘Tizauye Kaye’ (Tumerudi Nyumbani) ilikuwa ni albamu ya nne ya kundi hilo waliyoitoa mwaka 2007 ikiwa na nyimbo kama ‘Kibaka’, ‘Hotuba’, ‘Hamna Shida’. Hata hivyo albamu hiyo haikufanikiwa kuingia sokoni kutokana na kutokea msigano baina yao na mtayarishaji wao, P. Punk.

Baada ya hapo kila mmoja alikuwa akifanya kazi binafsi. Kundi hilo lina matarajio ya kujijengea heshima zaidi ya liliyonayo hivi sasa katika jamii.

Comments