Moracka:Mr Dar Handsome mwenye vipaji kibao



KIHISTORIA alianza muziki miaka nane iliyopita, lakini jina lake limekuwa maarufu zaidi katika miaka ya hivi karibuni baada ya kuanza kuimba kama msanii wa kujitegemea.Huyo si mwingine bali ni Mohammed Hassan maarufu kama ‘Moracka’.


Ni mshindi wa mwanaume mwenye mvuto wa jiji la Dar es Salaam kwa mwaka 2009, huku wimbo wa ‘Kisa me nashaini’ alioutoa mwaka 2005 ndio ulimtambulisha zaidi katika medani ya muziki wa bongo fleva.
Moraka ni mmoja ya wasanii waliokuwa wanaunda kundi la Rocka’s akiwa na wenzake kama Quick Racka, Dau Racka na Chief Racka, kabla ya kujitoa rasmi mwishoni mwa mwaka jana na kuamua kufanya kazi kivyake.

Kundi hilo aliloliasisi mwanzoni mwa miaka ya 2000 wakati akisoma shule ya msingi Olympio kabla ya kuhamia Upanga alikomalizia elimu yake ya msingi na baadaye kujiunga na sekondari ya Al Haramain ambapo mwaka 2007 waliachia kibao cha ‘Rocka’s Anthem’, kabla ya 2009 kuachia ‘Gamble’.

Katika mahojiano na mwandishi wa makala hii, Moracka anasema “nilijitoa Rocka’s siku chache kabla ya kufanyika kwa tamasha la fiesta mwaka 2009 na hatua hiyo nilifikia baada ya kuona hakuna ushirikiano baina yetu…nilikuwa nikiwashirikisha wenzangu katika mambo mengi lakini wao walikuwa wapo wawpo tu”, Anasema.

Anaongeza kuwa pamoja na kujitoa huko hana ugomvi na wanachama wenzake, wana maelewano mazuri tu a kwa kudhihirisha hilo anatarajia kuwashirikisha katika baadhi ya kazi zake zitakazokuwemo kwenye albamu yake ya kwanza ambayo bado anaendelea kuifanyia maandalizi.

Moraka anasema mpaka sasa amesharekodi nyimbo zaidi ya sita ambapo pia ndani ya albamu hiyo amepanga kuwashirikisha wasanii kama Geez Mabovu, Loveness, Fatma, Rocka’s na wengine na ili kuipa ladha tofauti albamu hiyo atarekodi nyimbo zake katika studio tofauti.

Kwa sasa Moracka anatamba na ngoma iitwayo ‘She Got It’ aliourekodi katika studio za Fishcrab chini ya mtayarishaji Lamar na video yake iliyotengenezwa Kalaghe Picture’s inatarajiwa kutoka wakati wowote kwani zoezi la upigaji picha limeshamilika.

“Mbali na huo nimeshakalisha vibao kama ‘How u feel’, niliomshirikisha Fatma, ‘Nijue Moja’ , ‘Unapopita’, pia nyimbo zangu za awali kama ‘demu mjanja’, ‘kisa me nashine’ na roka’s anthem zitakuwemo”, aliongeza.

Msanii huyo ambaye ana vipaji mbalimbali vya sanaa ikiwemo kuigiza, anasema ana uwezo wa kuimba lakini anapenda zaidi kurap kwani huwa ajiona yuko huru zaidi kutumia mtindo huo unaodaiwa kuwa ni wa ‘wagumu zaidi’.

Akizungumzia hali ya muziki hapa nchini, Moracka anasema “unaenda na wakati lakini unaisha hamu haraka, akimaanisha kuwa nyimbo nyingi zinazotolewa kwa sasa zinadumu kwa kipindi kifupi tu na kupotea kabisa tofauti na nyimbo za zamani na sijui nini kinasababisha hali hiyo”, anasema.

Hata hivyo msanii huyo anasema kwa upande mwingine anaona ni sawa kutokana na kuwa muziki huo unakubalika zaidi na hata wazee waliokuwa wakiupinga zamani kwa kuona kuwa ni wa kihuni siku hizi wanaukubali.

Pamoja na hilo, msanii huyo anaungana na wenzake katika suala la wizi la kazi zao na kusema kuwa hali hiyo inamtia hofu ya kutoa albamu, “sijui itakuwaje katika siku za usoni, hata hivyo kwa kuanzia ni msanii kufanya jitihada binafsi za kukabiliana na hali hiyokwa kuandaa albamu katika mazingira mazuri ili faida ipatikane”, Anaongeza.

Akiwa na matarajio ya kuwa msanii mkubwa ambaye ataitangaza Tanzania nje ya mipaka kwa kiwango cha hali ya juu, Moracka pia ana mpango wa kuwa muigizaji wa kimataifa, pia mwanamitindo wa kimataifa akiwa na imani kuwa linawezekana kutokana na kuwa na viopaji vya hali ya juu.

Anawashauri wasanii hapa nchini kufanya kazi kwa bidii pia kutouchukulia muziki kama ni uhuni, “tujiheshimu kwa kuandika mashairi bora na yenye maana ambayo kila mtu atayakubali na kututfanya tuzidi kuheshimika”, Anasema.

Comments