Mansu-Li: Hip hop ni ya ukombozi si biashara

Mansu-Li

“KAMA muziki wa hip hop ungekuwa hauna faida tusingeendelea kuimba na wala wasanii wa muziki huo wasingekuwa na mafanikio,” hiyo ni kauli ya msanii wa muziki wa hip hop nchini, Mansoor Ally Mohammed maarufu kama Mansu-Li.
Kauli ya Mansu-Li imekuja kufuatia wasanii wengi kuwa na dhana hiyo akiwemo Ahmad Ally ‘Madee’ aliyetunga wimbo ‘Hip hop haiuzi’ hali iliyomjengea chuki na wasanii wa muziki huo. Baadhi yao walijibu mapigo.
Akizungumza na mwandishi wa makala hii, Mansu-Li ambaye ni mmoja wa wasanii wanaofanya vema katika muziki huo hapa nchini, anasema mtazamo kuwa hip hop haiuzi hauna mantiki yoyote kwani wengi wa wasanii wanapenda mafanikio ya haraka.
Anasema hip hop ni utamaduni na inaelezea maisha halisi yanayotokea katika jamii duniani, ndiyo maana haifi kama muziki unaopigwa kwa mitindo mingine ambayo nyimbo zake zimekuwa zikitamba kwa muda mfupi tu na kisha kutoweka.
Mansu-Li anaongeza kuwa muziki wa hip hop ulikuwepo tangu awali na haupo kimaslahi. Ni wa ukombozi tofauti na aina nyingine aliyodai kuwa ipo kibiashara zaidi.
“Muziki wa hip hop unaongoza kwa kila sekta, hata katika ‘live perfomance’ wanamuziki wa hip hop tunafanya vizuri zaidi tofauti na wengine ambao wakiimba kidogo tu pumzi zinakwisha ama wanapoteza mwelekeo, wao ni wazuri zaidi katika playback.
“Ona watu kama Profesa J, Mr. 11 na wengineo, wamekuwa wakifanya vizuri na kupata mafanikio makubwa kupitia muziki huo, hivyo hatuwezi kuacha kuimba hip hop,” anasema.
Anasema kubwa linalochangia watu kuwa na fikra kama muziki wa hip hop hauuzi ni kutokana na wizi unaofanywa na wasambazaji wa kazi hizo.
“Mtu unaingia gharama kati ya sh mil tatu mpaka tano kwa ajili ya kutayarisha albamu, matokeo yake ukiingiza sokoni unajikuta unaambulia sh 500,000, hilo ni tatizo,” anasema.
Mansu–Li anasema kwa hali hiyo hawezi kutoa albamu na ndivyo ilivyo kwa wasanii wengi wa hip hop.
“Tumekuwa tukitoa singo moja moja moja ambazo zimekuwa zikitubeba katika medani ya muziki hapa nchini,” anasema.
Akizungumzia hali ya muziki hapa nchini, anasema imekuwa na ushindani mkubwa na hilo linatokana na kuibuka kwa wasanii wapya kila kukicha ingawa wengi wao wameshindwa kuwa wabunifu hivyo wanafanya kazi kwa kuiga waliotangulia.
Anasema wengi wanasafiria nyota za wenzao, hivyo wanapata mafanikio ya haraka na matokeo yake majina na nyimbo zao zinatamba kwa muda mfupi kabla ya kupotea kwa haraka kama walivyopanda.
“Wasanii tuumize vichwa kwa kutunga nyimbo zenye maana kwa jamii, kwa kufanya hivyo nyimbo zitaweza kutamba miaka mingi kama ilivyo hip hop,” anasema.
Kama hiyo haitoshi, anasema tatizo la kushuka kwa muziki pia linachangiwa na kuibuka kwa watayarishaji wasio na uwezo sambamba na studio zenye viwango vya chini, ambao badala ya kujijenga kwanza ili kutoa vitu vilivyo bora wao wanaangalia maslahi zaidi.
“Baadhi yao wanafanya vizuri, lakini wengine bora liende. Muhimu ni kujituma zaidi na wasanii chipukizi wafanye juhudi za kutunga mashairi yenye akili na kuacha kuiga nyimbo za wenzao,” anasema akiwa na matarajio ya kujiimarisha zaidi ndani na nje ya nchi.
Mansu-Li anasema anavutiwa na wasanii wote wanaofanya vizuri hapa nchini na nje ya mipaka ya Tanzania.

Historia yake kimuziki:
Alianza kujihusisha na muziki tangu akiwa mdogo ambapo alikuwa akikariri nyimbo za wasanii mbalimbali wa nje.
Anasema msanii Saleh Jabir alibadilisha upepo wake kimuziki wakati alipokuwa anasoma katika Shule ya Msingi Mlimani mwanzoni mwa miaka ya 1990.
“Jabir alikuwa akizigeuza nyimbo za Kiingereza na kuzifanya za Kiswahili, hivyo na mimi nilivutika naye na kuanza kutunga mashairi kwa lugha ya Kiswahili,” anasema.
Mwaka 2003 alishiriki katika shindano la kumsaka bingwa wa ku-rap lililoandaliwa na Radio Magic FM katika klabu ya Aset ambapo alitinga fainali na kushika nafasi ya nne.
Kupitia shindano hilo, mtayarishaji bora wa muziki kwa sasa, Hammie B enzi hizo akiwa Magic FM pamoja na Sosthenes Ambakise ‘Sos B’ walivutiwa na kipaji chake hivyo walimwingiza studio na kumtayarishia singo ya kwanza ‘Poa’, Hata hivyo haikufanya vema.
“Niliamua kutuliza msuli darasani na Hammie aliendelea na masomo yake ya chuo, hivyo 2006 tulikutana tena na akanitayarishia ‘Kina Kirefu’ ambayo ilinitambulisha katika game,” anasema.
Kibao ‘Kina Kirefu’ kilimuingiza kuwania tuzo za muziki za Kili pamoja na kazi za kina Fid Q, Rado, Joh Makini na Chid Benz, lakini hata hivyo hakushinda.
Mwaka huo pia aliachia ‘Sina Budi’ akimshirikisha Joslin, kazi iliyotayarishwa Downtown Records.
“Juni 2007 nilitoa ‘Sura ya mchezo’ kabla ya Septemba kutoka na ‘Tupo pamoja’ ambao nao ulifanya vema. Kazi zote zilitayarishwa na Hammie B. Pia wimbo huo niliufanyia video na Kampuni ya Visual Lab,” anasema.
Mwaka 2008 haukuwa mzuri kwake. Alifanya kazi nyingi za kushirikishwa na wasanii mbalimbali likiwemo kundi la Nako 2 Nako katika remix ya ‘Mchizi wangu’, akatoka na Kikosi cha Mizinga kwenye kibao chao ‘Hip hop bila madawa’ pamoja na wakali wengine.
Anasema kazi hizo zilimbakiza katika ramani. Pia mwaka huo alitoa wimbo mmoja tu ‘Naamini’ aliomshirikisha Esther Wasira.
Machi mwaka 2009 alitoka na ‘Mengi yanatokea’ kazi iliyotayarishwa na Lamar wa Fishcrab Records, Juni akatoka na ‘Hivi ndivyo, ndivyo sivyo’ akiwashirikisha Jay Mo na Ibra Da Hustler kabla ya Julai kuachia ‘Mrembo’ akimshirikisha Makamua. Wimbo huo bado unambeba mpaka sasa.
mwisho

Comments

  1. hongera kwa kutuletea makala za burudani na michezo, tunaomba habari zaid, mdau wakudata

    ReplyDelete

Post a Comment