Peter Msechu:Nilistahili kuwa mshindi BSS 2009

.hakubaliani na ushindi wa Cassian
.asema atamfunika sokoni
.‘hasira hasara’ kumpaisha
“Mimi ndiye mshindi wa BSS mwaka 2009, hilo halina ubishi na wala siwezi kubatilisha kauli yangu daima”, hayo ni maneno ya mshindi wa pili wa shindano hilo”.

Hayo ni maneno yaliyotolewa na mshindi wa pili wa shindano hilo, Peter Msechu alipozungumza na mwandishi wa makala haya mapema wiki hii.

Msechu akizungumza kwa kujiamini alisema kuwa baada ya kutangazwa kwa matokeo siku ya fainali alibaini kwamba mashabiki walitumia upepo kuchagua mshindi na si kipaji.

Alisema aliamini angekuwa mshindi mapema baada ya kuwasoma wenzake katika hatua zote walizopita kwenye mchakato wa kumsaka mshindi.

“Pamoja na yote majaji ndio walitoa uamuzi wao ya kufuata upepo wa mashabiki ambao walishindwa kubaini vipaji, hata hivyo naamini nilistahili kuwa mshindi”, alisema Msechu.

Alisema anataka kudhihirisha kuwa yeye ni bora na ana kipaji kupitia kazi zake ambazo ameanza kuzitayarisha hivi sasa, huku akiwa tayari ameachia wimbo wake unaojulikana kama ‘hasira hasara’ ambayo imeanza kufanya vizuri katika vituo vya redio.

Alisema mbali na singo hiyo pia ameshakamilisha singo yake ya pili ‘Maneno’ ikiwa ni mpango yake ya kukamilisha albamu yake ya kwanza kabla ya kumalizika kwa mwaka huu.

Anasema kwa hatua hiyo tu, inadhihirisha kuwa yeye ni zaidi ya Cassin kwani mshindi huyo mpaka sasa hajaweza kuibuka na singo yoyote tangu kumalizika kwa shindano hilo.

“Pascal hawezi kunifikia kwa hatua yoyote katika fani hii, labda muziki huu ufe”, anasema.

Anaongeza kuwa anataka kuondoa dhana ya kuwa washiriki wa BSS huwa wanaishia siku ya shindano yaani pindi wanapomaliza shindano hilo wanashindwa kutamba katika medani ya muziki hapa nchini.

“Nitafuta dhana hiyo...na nimeanza harakati kwa kutumia fedha zangu za zawadi kuingia studio ili kutayarisha kazi zangu ambazo naamini mashabiki watazipokea vema”, anasema.

Akielezea sababu za kuingia studio mapema ilitokana na kutowapoteza mashabiki wake waliokuwa wanampa sapoti katika kinyang’anyiro hicho ili waendelee kuwa pamoja kupitia kazi atakazoziachia.

Kuhusiana na ushindani uliopo kwenye gemu na maslahi yake, Msechu anasema kuwa muhimu ni kujipanga kwa kutayarisha kazi nzuri na zenye ujumbe kwa jamii.

“Muziki una maslahi kama ukijipanga vizuri, wengi wanashindwa kuumudu kutokana na kukurupuka kwa kutoa nyimbo bila mpangilio matokeo yake zinabaki zikielea”, anasema.

Msechu anasema hali hiyo inachangiwa na kuwepo kwa studio nyingi ambapo watayarishaji wake wamekuwa wakiangalia zaidi pesa badala ya viwango na kwa mwendo huo muziki huo unaweza kufa muda si mrefu.

Kwa mantiki hiyo, Msechu anawashauri wasanii kutayarisha kazi zao kwa umakini na kujiandaa vizuri pia watayarishaji wa muziki kuzipenda kazi zao kwa kutengeneza nyimbo zenye viwango bora.

“Wasifanye bora liende bali watengeneze kazi ambazo zitakuwa bora na zenye kuvutia kwa yeyete hivyo hata shabiki ashawishike kuzinunua”, anasema.

Akizungumzia matarajio yake, Msechu anasema amejipanga kuwa msanii bora mwenye ujuzi wa nyanja tofauti za fani hiyo kwa kujiendeleza zaidi kielimu ambapo amepanga kwenda nje ya nchi kusomea mambo ya muziki.

Anasema hivi sasa yupo katika mchakato wa kutafuta wafadhili ili kumuwezesha kwenda kujiendeleza ambapo anaamini baada ya elimu hiyo ataweza kutayarisha muziki, video za muziki ikiwa ni pamoja na matamasha makubwa ya muziki.

“Nawaomba wadau na mashabiki wangu mniwezeshe kwenda kujiendeleza kipaji niliochonacho ili niweze kufanya kazi hii kisomo zaidi”, anasema Msechu.

Msechu ambaye ni mtoto wa pili kati ya wanne wa Mzee Joram Msechu na mama Pendezael Eliakundi ambaye ni marehemu alizaliwa Machi 3, 1988, huko Buzebazeba Kigoma na kupata elimu ya Msingi Kahabuka Kigoma, kisha Sekondari Nianjema ya Bagamoyo kabla ya kujiunga na Sekondari ya Galanosi, Tanga kwa masomo ya kidato cha tano na sita alipohitimu mwaka huu.

Ametokea kwenye familia ya waimbaji ambapo Marehemu mama yake, baba yake na ndugu zake wote ni waimbaji wazuri wa kwaya kanisani.

Akiwa na kipaji cha kuimba mitindo yote ya muziki, Msechu anavutiwa na wasanii Banana Zorro, Marlaw na R.Kelly anawashukuru mashabiki wote waliomfikisha hapo alipo na anawaomba kuendelea kuwa naye sokoni.

Kwa sasa washiriki walioingia tano bora ya BSS 2009 wapo studio wakiandaa albamu ya pamoja chini ya usimamizi wa mtayarishaji, Master J kupitia studio zake za Mj.

Katika shindano hilo lililofanyika oktoba 13 kwenye ukumbi wa Diamondi Jubilee, Cassian aliibuka na ushindi na Msuchu kushika nafasi ya pili huku nafasi ya tatu ikienda kwa Kelvin Mbati, Jackson George alikuwa wa tano na Beatrice alikuwa wa tano.

Comments