Nafungiwa kwa chuki binafsi- Chuji




.Aamua kuwa mpole uwanjani hata akionewa
.Asema mpambano dhidi ya Simba ya kawaida


TANGU ajiunge na timu ya Yanga akitokea Simba, kiungo Athuman Idd ‘Chuji’ amekuwa akiandamwa na mabalaa mbalimbali ikiwemo kufungiwa kucheza soka kwa nyakati tofauti kwa hoja ya utovu wa nidhamu.

Mbali na kufungiwa mara kadhaa kwa sababu hiyo, Chiji pia amejikuta ‘akifungiwa vioo’ katika kikosi cha timu ya soka ya Tanzania, Taifa Stars’ chini ya kocha Mbrazil, Marcio Maximo.

Kote huko inaelezwa ni kutokana na utovu wa nidhamu pindi anapokuwa uwanjani, iwe kwa waamuzi wa mchezo ama mashabiki au timu pinzani.
Je, hali hii anaichukulia vipi kwake kama mchezaji mwenye malengo ya mafanikio katika soka?

Katika mahojiano maalum yaaliyofanyika mwishoni mwa wiki iliyopita, Chuji anasema kwa upande wake anaona kufungiwa kwake kama chuki binafsi dhidi yake zinazofanywa na watu wasiomtakia mema.

Anasema umekuwa ni mkakati maaalumu uliosukwa na kupangiliwa ipasavyo kupanga mtiririko wa visa na vituko vya kuhalalisha kuwa, Chuji si mchezaji mwenye nidhamu.

“Ni mpango mchafu dhidi yangu wa kunifanya nionekane ni mkorofi uwanjani, katika hili wabaya wangu wamekuwa wakiwatumia hata wachezaji au mashabiki wa timu pinzani kunichokoza ili kunipandisha hasira ili niadhibiwe,” anasema Chuji na kuongeza:

.“Nikiwa uwanjani, mtu unakufanyia kitendo cha ajabu ili mradi akupandishe hasira ili uonekane wewe mkorofi, matokeo yake ndio unaonekana wewe mtovu wa nidhamu,” anasema kwa masikitiko na kusema yeye si mkorofi kama alivyochafuliwa.

Anaongeza kuwa yeye ni mtu mwenye akili timamu, hivyo kamwe hawezi kufanya utovu wa nidhamu kila mara kama ambavyo amekuwa akidaiwa, isipokuwa ni ni mkakati uliosukwa kuchafua jina lake.

“Kwa sababu jina langu linaonekana limechafuka kamba mimi ni mtovu wa nidhamu, nimekuwa nikiandamwa mno hata pale kosa linapofanywa na mchezaji mwingi wa karibu yangu,” anasma Chuji.

Chuji anasema licha ya kuwa makini awapo uwanjani, dabo anaonekana ni mtukutu kumbe na kusema hiyo kwake ni changamoto ya kumfanya azidi kuwa makini kwa kuchukua tahadhari.

Aidha, Chuji anakwenda mbali zaidi akisema anashangazwa na sheria zinazotumika kumfungia kwani zimekuwa zikijichanganya zenyewe kwa Kamati husika kuzipindisha.

“Kwa kweli adhabu zinazotolewa dhidi yangu nashindwa kuzielewa zinatoka wapi kwani zinakuwa zinajichanganya …lakini kwa vile unakuwa umeadhibiwa, huwa jingine la kufanya isipokuwa kutekeleza adhabu,” anadai Chuji.

Chuji anasema katika kujiepusha na matatizo ambayo yamekuwa yakimwandama, kuanzia sasa ataongeza umakini uwanjani ikiwemo kutozungumza na mtu hata kama atamuudhi vipi.

“Yaani kwa kuonywesha ni jinsi gani ninaonewa, niwapo uwanjani hata nikifanyiwa vibaya waamuzi, hawachukui hatua, mfano mechi yetu na Azam wiki iliyopita kuna mchezaji alinitwanga ngumi ya jicho na kupata maumivu makali, lakini niliposhitaki kwa mwamuzi hakuchukua hatua yoyote,” anadai Chuji.


Vipi mechi dhidi ya Simba?

Chuji anasema licha ya wapenzi na mashabiki kuipa mechi hiyo umuhimu mkubwa, kwao wachezaji wa Yanga ni ya kawaida tu kama ilivyo kwa mechi dhidi ya timu nyingine katika ligi hiyo.

“Mechi dhidi ya Simba kwetu ni ya kawaida tu kama zilivyo nyingine ambazo tumekuwa tukicheza, hivyo hatuna hofu yoyote na ushindi tutafanya kama mwaka jana,” anasema Chuji.

Katika msimu uliopita, Simba na Yanga zilipokutana Oktoba mwaka 2008, Yanga ilishinda bao 1-0 kabla ya kutoka sare ya mabao 2-1 ziliporudiana Aprili 19, mwaka 2009.

Chuji anasema licha ya timu yao kutetereka katika ligi hiyo huku Simba ikiwa na rekodi ya kutofungwa, anasema hiyo haiwatii hofu kwani hicho si kigezo cha wao Yanga kufungwa.

Akiizungumzia ligi hiyo kwa mwaka huu, Chuji anasema imekuwa ya ushindani mkubwa hali inayochangiwa na
timu zilizopanda kutaka kuonyesha makali yao, hivyo kukamia kila mechi hasa walizozikuta ikiwemo Yanga.

“Hali hiyo imesababisha hata sisi Yanga kuwa katika nafasi hii, lakini ndiyo ushindani kwnai kuna kipindi hali inakuwa haijakaa vizuri na wakati mwingine mnakuwa sawa,” anaongeza Chuji.

Kuhusu ujio wa kocha wao mpya kutoka Serbia, Kostadian Papic ‘Clinton’, Chuji anasema licha ya baadhi ya watu kumponda kocha huyo, wa wachezaji wanamuona ni kocha mzuri mwenye mipango madhubuti.

Anasema baada ya kuonmdoka kwa Dusan Kondic, Papic anajitahidi kujenga upya kikosi hicho baada ya kudumu nacho kwa karibu wiki mbili tangu aliposaini mkataba wa kukinoa kikosi hicho kwa mwaka mmoja.

Chuji ambaye aliwahi kuzichezea timu ya taifa ya vijana na Polisi Dodoma, ameawataka mashabiki wa Yanga kutulia kwani kuteleza sio kuanguka mambo yatakuwa mazuri muda si mrefu.

mwisho

Comments