Kilimanjaro Stars na Zanizbar हेरोएस

Timu mbili zenye upizani wa kupindukia katika soka, Kilimanjaro Stars ya Tanzania Bara na Zanizbar Heroes zinakutana jijini hapa katika mchezo wa kusaka nafasi ya tatu ya michuano ya 33 ya kombe la Chalenji inayofikia tamati leo.

Mchezo wa leo unazikutanisha timu hizo baada ya kupoteza michezo ya nusu fainali ambapo Zanzibar ilifungwa 2-1 na mabingwa watetezi Uganda Juamatano kabla Stars kufungwa na Rwanda kwa idadi hiyo hiyo ya magoli hapo Alhamis.

Awali mchezo huo ulipangwa kufanyika jana (Jumamosi) lakini uliahirishwa kutokana na uwanja wa Nyayo kutumika kwa shughuli za maadhimisho ya miaka 46 ya Uhuru na miaka 45 tangu Kenya iwe Jamhuri.

Mshindi wa mchezo huo utakaochezwa kuanzia saa 7 mchana na ambao unangojewa kwa hamu na wapenzi wa soka atajinyakulia fedha tasilim Dola za Marekani 10,000 pamoja na medali za Shaba. Baadaye utafuata mchezo wa fainali kati ya Uganda na Rwanda.

Hii itakuwa ni mara ya pili timu hizo kukutana katika michuano ya mwaka huu kwani mara ya kwanza timu hizo zilikutaa Desemba mosi katika hatua ya makundi na Stars kushinda 1-0 goli lililofungwa na Mrisho Ngasa kwenye uwanja wa kiwanda cha Sukari cha Mumias, magaharibi mwa Kenya.

Kocha wa Stars Marcio Maximo anasema anatarajia mchezo mgumu na wa ushindani wa hali juu kama ambavyo ilikuwa michezo mingine dhidi ya Zanzibar.

‘ Michezo yetu yote na Zanzibar imekuwa ni migumu na pamoja na kwamba tumekuwa tukishinda, ushindi wenyewe umekuwa ni mdogo kwa hiyo sitarajii kitu tofauti, uatkuwa mchezo mgumu ambao lazima tuwe makini na tupunguze makosa ili tyondoke na kitu kwenye mashindano haya’ alisema Maximo ambaye atakuwa anakutana na Zanzibar kwa mara ya nne, akiwa ameshinda mechi zote tatu za awali.

Maximo alianza kukabilina na chagamoto za kucheza dhidi ya Zanzibar Agosti 26, 2006 katika mchezo wa kirafiki na akafanikiwa kushinda 1-0, Said Maulid akiziona nyavu. Mapema mwaka huu huko Uganda Kilimanjaro Stars ilijipatia ushindi wa magoli 2-1, yaliyofungwa na Mrisho Ngasa na Athuman Iddi kabla ya kushinda tena huko Mumias. Goli la Zanzibar wakati huo lilifungwa na Nadir Haroub ‘Cannavaro’

Mara ya mwisho Zanzibar kuifunga Tanzania Bara katika michuano ya Challege ilikuwa mwak 2004 wakati michuano hiyo ilipoandaliwa huko Ethiopia na timu hizo kupangwa kundi moja. Zanzibar ilishinda kwa magoli 4-0. Tanzania Bara iliwahi kupata ushindi kama huo mwaka 1975 wakati mashindani hayo yalifanyika Zambia. Hiyo pia ilkuwa katika hatua ya Makundi.

Matokeo mengine yanayokumbukwa mno ni ya mwaka 1988 katika kombe la Chalenji lililoandaliwa Malawi na Zanzibar kuishinda bara kwa goli 1-0 katika hatua ya makundi huku ikiwa haina nafasi yoyote ya kufuzu kwa hatua ya nusu fainali. Kichapo hicho pia kiliikwamisha Bara kufuzu.

Zanzibar inayofunzwa na kocha Hemed Morocco itakuwa ikiwategemea zaidi wachezaji wake wazoefu wanaocheza katiika Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara. Wachezaji hao ni Cannavaro, Nahodha Abdi Kassim, kiungo Abdulhalim Humoud wa Mtibwa Sugar, Nassor Masoud wa Moro United na Aggrey Moris wa Azam FC.

Kocha Maximo anatarajiwa kufanya mabadiliko kidogo kwenye kikosi chake kutokana hali halisi ya kukosekana kwa mlinzi wa kati kevi Yondan aliyeonesha kadi nyekundu katika mchezo dhid ya Rwanda na pia mahitaji ya mchezo weyewe.

Nafasi ya Kevin inatarajiwa kuzibwa na David Naftal ambaye itakuwa mara yake ya kwanza kuwemo kwenye kikosi kwanza. Kadhalika Sahaban Nditi anatarajiwa kuanzia benchi huku kiungo Ibrahim Mwaipopo akianza kudhibiti sehemu ya kati akisaidiana na Juma Nyoso, Nurdin Bakari na Kigi Makasi.

Nahodha Salum Swed ambaye leo atakuwa nacheza mechi yake ya 60 ya kimataifa ataendeleo kuongoza safu ya ulinzi lakini bila shaka atahitajika kupanga vema safu hiyo inayoundwa pia na Shadrack Nsajigwa, na Juma Jabu na hivyo kurekebisha makosa yaliyosababisha Rwanda kujipatia magoli mawili.

Jukumu la kupachika magoli litabakia kwa mshambuliaji kijana mwenye umri wa miaka 20, John Bocco na kinara wa kuziona nyavu, Mrisho Ngasa ambaye hadi sasa amepachika magoli 5 katika mashindano haya huku akiwa amefunga magoli 9 ya kimataifa katika micheso 33 aliyocheza.
Mwamuzi wa mchezo wa leo leo Ali Kalyango wa Uganda ambaye amejipatia umaarufu kwa namna anavyodhibiti michezo ambayo huichezesha.

Comments