Boban: Watu wanavyonichulia sivyo

KIUNGO mshambuliaji wa vinara wa Ligi Kuu ya Bara, Simba aliyepata ulaji wa kukipiga katika klabu ya Gefle Fc ya Sweeden, Haruna Moshi ‘Boban’ amesema atawashangaza wote waliokuwa na fikra potofu juu nidhamu yake.

Boban ametoa kauli hiyo kufuatia wadau wa soka nchini kumtilia shaka kama ataweza kufanya vizuri na timu hiyo kutokana na kuzoeleka kuwa na tabia ya utovu wa nidhamu ulikithiri.

Utovu huo ulisababisha kufungiwa kucheza mechi za ligi kuu bara kwa nyakatio tofauti, pia kuenguliwa kwenye kikosi cha timu ya Taifa ‘Taifa Stars’.

Akizungumza katikamahojiano na Tanzania Daima, Haruna anasema, mara nyingi jamii imekuwa ikimwona ni mtovu wa nidhamu, kitu ambacho hakina ukweli wowote.

“Mimi mbona niko safi tu…unajua watu wanavyonichukulia sivyo…kwa vile wameamua kunichukulia hivyo, mimi naona sawa tu kwani huwezi kumkataza mtu kukufikiria au kukuelezea anavyojisikia,” anasema Boban aliyeachwa kikosi cha timu ya soka ya Tanzania, Taifa Stars na Bara kwa sababu za kinidhamu.

Haruna anasema kupitia nafasi yake katika klabu hiyo ya daraja la kwanza, ataonyesha ni jinsi gani nidhamu yake ilivyo na hivyo kila mtu atapata jibu la jinsi alivyokuwa akimchukulia.

Akiguzia tofauti ya wachezaji wa huko na wa hapa nchini, Haruna anasema kuna tofauti kubwa sana kuanzia ndani na nje ya uwanja kwani wachezaji wa huko wanaithamini sana kazi yao.

Boban aliyetokea katika familia ya soka, anasema wachezaji wa huko wako makini na wanachokifanya nduio maana wamepiga hatua kubwa katika medani hiyo tofauti na wachezaji wa hapa nchini ambao wanaifanya ajira hiyo kama mzaha.

Mbali ya Boban, nyota waliowahi kung’ara katika soka ya Tanzania kutoka katika famili ya mzee Shaaban Moshi, ni Shaaban, Mrisho, Iddy na Ally.

Anasema, alipokwenda Sweden kwa majaribio, aliweza kuwasoma haraka wachezaji wenzake, hivyo kuchukua muda mfupi kujua mahitaji yatakayomfanya aweze kufaulu majaribio yake.

Haruna anasema, kutokana na uzoerfu na uwezo alionao, hakupata tabu katika majaribio yake hayo ambayo hata hivyo anamshukuru mwenyezi Mungu.

“Namshukuru mungu kwa kuniwezesha kufaulu majaribio yangu ambapo nimetimiza ndoto zangu za muda mrefu za kucheza soka la kulipwa katika nchi zilizoendelea,” anasema Haruna.

Aidha, nyota huyo anaongeza kwamba kutokana na nafasi hiyo aliyoipata ataitumikia vema klabu yake sambamba hivyo kuipeperusha vema bendera ya Tanzania.

Haruna ambaye ataanza kuitumikia klabu hiyo januari mwaka 2010, kabla ya kwenda huko alikuwa akiichezea Simba ya Dar es Salaam ambayo amejiunga nayo mwaka 2004.

Hivi sasa yupo nchini, akisubiri kwenda kuanza kibarua chake kipya mwakani ambapo atawaaga mashabiki wa Simba na wadau wa soka akiwa na timu yake ya Simba kwenye michuano ya kuwania kombe la Tusker itakayoanza Desemba 14.

Mbali ya kuichezea Simba, aliwahi pia kwenda nchini Oman na kukipiga Muscat FC, pia aliwahi kuichezea Moro United mwaka 2003 aliposhiriki nayo kwenye Ligi Kuu Bara.

Mchezaji huyo ambaye anatoka kwenye familia ya wacheza soka, aliibuliwa na mkuu wa shule ya Makongo, Idd Kipingu ambaye kwa sasa, ni Mwenyekiti wa Baraza la Michezo Tanzania -BMT), kupitia michuano ya shule za msingi (UMITASHUMTA).

Akiwa Makongo na kujiendeleza katika soka, aliwahi kuzichezea kwa nyakati tofauti timu za vijana chini ya miaka 17 na 20 akiwa na nyota wengine kama Juma Kaseja, Nico Nyagawa, Musa Mgosi na wengine.

Umahiri alionao dimbani uliiwezesha timu yake ya Simba kutwaa mataji ya Ligi Kuu Bara, Kombe la Tusker na kufika raundi ya pili ya Ligi ya mabingwa wa Afrika kwa nyakati tofauti.

Mwaka 2007, Haruna alichaguliwa kuwa mchezaji bora kupitia tuzo zinazotolewa na chama cha waandishi wa habari za michezo Tanzania (TASWA).

Comments