ZIUNDWE NA KAMATI ZA KUISAIDIA MICHEZO MINGINE SIO SOKA TU

Na Dina Ismail
TANZANIA imebahatika kuwa na wachezaji wenye vipaji mbalimbali kiasi cha kuweza kuiletea sifa nje ya nchi kwa kutwaa ubingwa ama kushika nafasi za juu katika mashindano mbalimbali.
Michezo kama riadha, masumbwi, mpira wa kikapu, mbio za nyika, mpira wa wavu, kuogelea ni baadhi tu ambayo tunaweza kujivunia wachezaji wake.
Licha ya kutuletea sifa lakini michezo hiyo bado imekuwa haipewi kipaumbele kwa namna moja ama nyingine kama ilivyo kwa mpira wa miguu.
Sote tunaamini na kujiridhisha kwamba, mpira wa miguu ni mchezo unaopendwa sana kiasi cha kujizolea mashabiki wengi katika nchini nyingi duniani.
Kimafanikio,  hapa Tanzania hatuwezi jivunia mpira wa miguu  ukilinganisha na riadha au ndondi ambayo mara kwa mara imekuwa ikituletea medali.
Lakini cha ajabu soka ni mchezo ambao unathaminiwa zaidi na kupewa sapoti ya kutosha katika kila sekta kila kukicha.
Kuna makampuni, taasisi na hata watu binafsi hujitokeza kusapoti ama kudhamini mchezo mpira wa miguu iwe katika ligi, mashindano ya ndani au nje, lakini si kwa michezo nyingine.
Timu za michezo kama ngumi au riadha hujikuta katika maandalizi duni kutokana na ukata lakini hufanya maandalizi kufa kupona na hatimaye hushiriki na kushinda.
Mfano mwezi uliopita, timu ya Taifa ya Tenisi kwa watu wenye ulemavu iliitoa kimasomamso Tanzania baada ya kufuzu kucheza  mashindano ya kombe la dunia kwa mchezo huo yanayotarajiwa kufanyika mwezi Mei mwaka huu nchini Italia.
Timu hiyo ilifuzu hatua hiyo bada ya kushika nafasi ya kwanza  katika michuano ya Afrika iliyofanyika Nairobi, lakini ilifanya maandalizi yake ikiwa na hali ngumu kutokana na kutopata sapoti yoyote kama tulivyozoea katika timu za soka.
Kama hiyo haitoshi, mpaka sasa hakuna kiongozi wala taasisi yoyote aliyejitokeza kuendesha kampeni ya kuisaidia timu hiyo ambayo itaiwakilisha Tanzania katika mashindanio ya dunia.
Lakini kila mara tumekuwa tukishuhudia zikiundwa kamati mbalimbali za kuzisaidia timu  za soka ambazo zinashiriki mashindano nje ya nchi, lakini hatujawahi kusikia kuna kamati ya kusaidia timu ya riadha ishinde au timu ya ndondi.
Kwa mfano sasa hivi Serikali pamoja na Shirikishola Soka Tanzania (TFF) wameunda kamati ya kuicchangia timu ya Taifa ya Vijana chini ya mkiaka 17 (Serengeti Boys) inayoshiriki fainali zxa Mataifa ya Afrika (AFCON) mwezi Aprili kule Gabon.
Siyo mbaya kwa kitu kama hicho kufanywa na serikali,  lakini Serikali wadau inapaswa kutambua kuwa Tanzania sio ya soka pekee kuna michezo kingine pia inahitaji kusapotiwa kwani inaweza kuiletea sifa Taifa.

Ni jambo la kusikitisha na kuvunja moyo kwa sababu michezo hiyo hiyo isiyothaminiwa ndiyo inayoliletea sifa Tanzania katika medani ya kimataifa.
Nchi nyingi zilizoendelea zinathaimini michezo yote na ndio maana zinafanya vema zaidi, lakini sisi tunathamini soka tu kwa sababu unaonekana ndio unamaslahi ndani yake.

Ifikie mahala watanzania tubadilike  kwa kuachana na kasumba ya kuuthamini mpira wa miguu tu badala yake kutoa  usawa kwa michezo mingine ili tuweze kupiga hatua zaidi. 

Comments