YANGA TULIENI VINGINEVYO MTAZIDI KUPOTEA


Na Dina Ismail
KUMEKUWA na sintofahamu katika klabu ya soka ya Yanga kufuatia taarifa za kuwepo kwa hali ya ukata unayoikabili.
Hali hiyo inafuatia mwenyekiti na mdhamini wa timu hiyo, Yussuf Manji kuwa katika misukosuko baada ya akaunti zake kufungwa na serikali.
Kwamba, Manji baada ya kukumbwa na misukosuko hiyo klabu imekuwa katika hali mbaya ya kifedha  ambapo Katibu mkuu wa Yanga   Charles Boniface Mkwassa akithibitisha hali hiyo.
Kama hiyo haitoshi, ukata huo umepelekea Yanga kusitisha ajira ya Mkurugenzi wake wa ufundi, Hans Van Pluijim.
Pia kuna taarifa ya baadhi ya wachezaji kwamba wapo mbioni kuikimbia klabu hiyo kutokana na hali mbaya ya kiuchumi iliyonayo.
Hizi dalili mbaya kwa klabu ya Yanga na isipochukuliwa tahadhari ni wazi kwamba itapoteza hata matumaini yake ya kutetea ubingwa wake wa Ligi Kuu soka Tanzania Bara na hata michezo yake ya Ligi ya Mabingwa Afrika.
Yanga ni mali ya wanachama hivyo basi ni wajibu kwa kila mwanachama  mwenye mapenzi ya kweli kujitoa kwa hali na mali kuhakikisha wanaiokoa klabu yao ili iweze kurudi katika mstari.
Kuendelea kuacha jukumu la kuiendesha pekee kwa uongozi itakuwa ni kuwatwika mzigo ambao hawawezi kuubeba.
Pia ni wakati kwa viongozi kuamka katika usingizi wa muda mrefu iliokuwa imelala kwa kutegemea mtu mmoja katika kuindesha kwenye masuala ya kiuchumi.
Yaangi, viongozi wapigane kufa kupona ili kuhakikisha wanapatikana wafadhili ama wadhamini ambao watamwaga fedha kwa ajili ya kuindeshe klabu hiyo.
Soka la sasa lipo kibiashara zaidi, hivyo bila ya kuwa na fedha itakuwa gumu kwa klabu kubwa kama Yanga kuishi kwa kutegemea mapato ya mlangoni tu.
Kwamba , tahadhari zisipochukuliwa ni mengi tutayasikia na kuyaona kwani Yanga imesheheni wachezaji wa kigeni ambao wanahitaji kulipwa mishahara na stahiki zao nyingine, hata wale wazawa pia wanahitaji kulipwa hivyo bila pesa kuna kitakachochezwa hapo?
Tukirejea historia ya soka la bongo inaonesha kwamba, dalili za namna hii na hasa kwa vilabu vikubwa kama Yanga ni mbaya na zisipofanyiwa kazi zitawagharimu sana na itawachukua muda mpaka kukaa katika mstari ulionyooka.
Yanga ambayo pia inashiriki Ligi ya Mabingwa Afrika inahitaji kujiaandaa vema ili kuweza kushinda michezo yake na kusonga mbele na maandalizi hayawezi kuwa bora bila ya kuwepo kwa fedha.
Ni kipindi ambacho ‘vivuruge’ watakitumia kwa lengo la kuhakikisha Yanga inaparaganyika hivyo kushindwa kutimiza harakati zake za kutetea ubingwa.
Katika kipindi hiki cha mpito ni vema kukawepo na amani na mshikamano ili mwisho wa siku lolote litakalotokea libaki kuwa limetokana na umoja huo.
Bila mshikamano ni wazi kwamba mtavuruga hadi akili za wachezaji wenu na hivyo kupelekea kupoteza mwelekeo kabisa katika kutimiza wajibu wao .
Shime kwa wanaYanga kuchukua tahadhari mapema kabla ya hatari kubwa inayioweza kuja kutokea katika siku zijazo.

Comments