YANGA MDHARAU MWIBA.....

Na Dina Ismail
KUNA usemi  maarufu ‘Mdharau mwiba, mguu huota tende!
Huu msemo una maana kubwa sana na ni wajibu kuutilia maanani.
Mabingwa watetezi wa Ligi Kuu bara, Yanga Sc kwa leo ndio walengwa wa msemo huu.
Kwa miezi kadhaa sasa hali ya kiuchumi ndani ya klabu hiyo yenye maskani yake mitaa ya jangwani na Twiga imekuwa si nzuri.
Hiyo inatokana na mwenyekiti wake ambaye pia ni mfadhili wa klabu hiyo, Yussuf Manji kupata misukosuko na serikali.
Kutokana na hali hiyo kuna baadhi ya mambo na hasa yahusianayo na masuala ya kifedha ndani ya klabu hiyo yalianza kuyumba.
Mwezi Machi mwaka huu, Katibu mkuu wa Yanga, Charles Boniface Mkwassa alikiri kuwawepo kwa hali mbaya ya kiuchumi kiasi cha wachezaji kutolipwa mshahara wa mwezi mmoja.
 Mkwassa alisema  tangu Manji aingie matatani, hajawahi kufika katika ofisi za klabu hiyo hivyo wamekuwa na wakati mgumu wa kupata fedha za kuendesha klabu na hivyo walikuwa mbioni kuandaa utaratibu wa kuwataka wanachama na wapenzi wa Yanga waweze kuichangia ili iweze kutimiza malengo yake ya kutetea ubingwa wa ligi kuu.
Kama hiyo haitoshi, baada ya siku chache baadae  ilitangaza kuachana na aliyekuwa Mkurugenzi wake wa benchi la ufundi, Mholanzi Hans van der Pluijm kutokana na sababu hiyo.
Ukata huo ulipelekea pia wachezaji kugomea mazoezi kwa siku kadhaa wakishinikizwa kulipwa mishahara yao, kabla ya kuwekwa sawa na kuendelea na maandalizi yao ya ligi kuu bara na michuano ya kombe la Shirikisho.
Wiki iliyopita kumeibuka taarifa za mshambuliaji wake wa kimataifa Mzambia Obrey Chirwa kugoma kufanya kazi ndani ya klabu hiyo hadi alipwe malimbikizo yake ya mishahara ya miezi mitatu.
Chirwa pia alikataa kusafiri na wenzake kwenda Algeria kwa ajili ya mchezo wa marudiano wa mchujo wa kuwania kuingia hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya, Mouloudia Club Alger  uliofanyika Jumamosi Uwanja wa Julai 5, 1962 mjini Algiers ambapo walifungwa jumla ya mabao 4-0 hivyo kuondolewa katika michuano hiyo kwa jumla ya mabao 4-1.
Hali ya ukata ni kitu cha kawaida hasa kwa vilabu vyetu vya bongo lakini je viongozi huwa wanalichukuliaje na hasa kwa vilabu vikubwa ambavyo vinakuwa katika harakati muhimu.
Mpira ni ajira yao wachezaji kwani kuna wenye familia ambazo zinawategemea hivyo kama wasipolipwa stahiki zao ni lazima watashindwa kutimiza wajibu wao ipasavyo.
Ni bora ya chirwa ambaye ameamua kujilipua mwenywe ili kufikisha salamu kwa uongozi kuliko hao waliokaa kimya sababu hamjui wanapanga nini vichwani mwao.
Yanga inakabiliwa na mchakamchaka wa kuwania ubiongwa pamoja na michuano ya kombe la Shirikisho hivyo ni kipindi ambacho wachezaji walipaswa kulipwa vizuri ili kuwekeza nguvu katika michuano hiyo.
Lakini kwa sasa akili zao zitakuwa zikiwaza fedha tu na matokeo yake timu itajikuta inafanya vibaya katika michezo yake na kuanza kumtafuta mchawi wakati wanajiroga wenyewe.
Yanga ni timu kubwa, timu pendwa  yenye mashabiki wenye hadhi na madaraja tofauti  katika ukanda wa Afrika  mashariki na Kati ambao wakiamua wanaweza kuichangia klabua yao ili kulipa mishahara ya wachezaji na shughuli nyingine za klabu.
Kinachoonekana ni mawasiliano duni baina ya uongozi wa klabu na wadau wake kwani naamini kuna matajiri wengi sana ambao wanaweza kuokoa jahazi, lakini uongozi umeamua kumuachia mzigo huo manji pekee tu kitu ambacho sio sahihi kabisa licha ya kuwa ni mfadhili wao.
Hivyo ni wakati wa viongozi kuamka na kutafuta njia mbadala ya kukabiliana na hali hiyo ili kuhakikisha wachezaji wanapata stahiki zao na kazi ibaki kwao kutimiza wajibu wao uwanjani.
Kwa kuacha hali ibaki hivyo hivyo mwisho wa siku itawagharimu maana leo kaanza Chirwa, kesho atakuja Tambwe  (Hamis), na mwisho wa siku timu nzima, sasa ikifikia huko unadhani timu itakuwa na mafanikio tena?

Kauli mbiu ya  Yanga ‘Daima Mbele nyuma Mwiko’ nadhani ndio ifuatwe kwa kuweka sawa kasoro ndogondogo kama hilo suala la mishahara ili baadae wasije patwa na Matende!

Comments