TUCHAGUE VIONGOZI BORA ILI TUPIGE HATUA MICHEZONI

Na Dina Ismail
KWA miaka mingi Tanzania imekuwa  ikifanya vibaya katika michezo mbalimbali ya kimataifa ambayo inashiriki.
Licha ya kujaliwa kuwa na wachezaji wenye vipaji vya hali ya juu lakini bado hali imekuwa si ya kuridhisha kabisa.
Hata hivyo sababu  hasa ya kutokufanya vema  na kujikuta kuwa wasindikizaji tu katika mashindanio tunayojaliwa kushiriki bado haijajulikna.
Kwani kama ni maandalizi hufanyika ya kutosha, kama ni walimu wapo wazuri sana iwe wazawa ama wale wa kigeni ambao naamini hawana tofauti na wan chi nyingine.
Ukiangalia kwa haraka haraka, kitu kikubwa kinachotukwamisha ni viongozi tulionao katika ngazi mbalimbali.
Ndio! Viongozi ndio kila kitu katika mafanikio ya kitu hivyo basi tunaweza kusema wao ndio wanachingia tufanye vibaya au vizuri katika michezo.
Sifa ya kiongozi bora ni kuhakikisha anasimamia vilivyo anachokiongoza ili mwisho wa siku kiwe kitu bora na chenye manufaa kwa Taifa.
Na viongozi wengi wa vyama vya michezo hawana sifa za viongozi kwani uwepo wao umetokana na shinikizo kutokana na sababu fulani, ushabiki na mengineyo.
Kwamba wengi wa viongozi katika michezo hawana wapo kwa manufaa yao binafsi na si katika kuendeleza michezo.
Tumesshuhudia katika kampeni kabla ya chaguzi mbalimbali, viongozi wengi wakitoa ahadi nzuri sana na za kupendeza na kuwavutia wapiga kura lakini pindi wanapochaguliwa hushindwa kutekeleza.
Hivyo basi, kushindwa kwao kutekeleza ahadi walizoweka pindi wanaomba kura ndiyo inakuja pelekeakubaki wasindikizaji katika michuano ya kimataifa.
Kiongozi anaonekana kipindi cha kuomba kura tu na baada ya hapo humuoni ofisini wala kwenye viwanja vya michezo kwa ajili ya kutoa sapoti ama neno lolote la faraja kwa wanamichezo wa eneo lake.
Kiongozi hajui hata wanamichezo ama michezo iliyopo katika eneo lake, yeye huishia kuja kutoa pongezi kwa washindi au kuzindua mashindano tu.
Kuna maeneo yamebarikiwa kuwa na hali nzuri ya hewa kwa ajili ya wanamichezo kufanya maandalizi yao lakini kutokana na kuwa na viongozi wasiokuwa na kiu ya mafanikio wanashindwa kuzitumia vema rasilimali hizo.
Ifikie mahala wapiga kura wajiongeze kwa kuchagua viongozi ambao wana lengo na dhamira ya dhati kabisa ya kuinua na kuendeleza michezo na si kuchagua viongozi ‘wauza sura tu’.
Kwamba, kiongozi anamwaga sera za kuvutia na anachaguliwa kwa kura nyingi, lakini anamaliza muda wake bila kuleta mafanikio yoyote halafu anakuja kuomba tena nafasi ya kuongoza, huyo hafai kabisa kurudi.
Kama kweli tunataka mafanikio katika michezo ni vema wapiga kura kuchagua viongozi wanaoona wana dhamira ya dhati na uchungu na maendeleo ya soka.

Pia kwa wale viongozi maslahi ifikie mahala waone aibu kwa kujiweka kando na kuwaachia wenye moyo wa dhati kuongoza.

Comments