SERENGETI BOYS IZIKE 'BIFU' YA DIAMOND, KIBA

Na Dina Ismail
WASANII  maarufu  nchini  wa muziki wa  kizazi kipya  Nassib Abdul ‘Diamond Platnumz’  na Ali  ‘King’ Kiba  wanatarajiwa kurekodi  wimbo wa pamoja ambao ni maalum kwa ajili ya kuhamasisha kampeni za kuichangia timu ya Taifa ya Vijana wenye umei chini ya miaka 17 ‘Serengeti Boys’.
Nyota hao ambao pia ni wajumbe wa kamati  ya  Serengeti Boys  wamekuwa na msigano mkubwa kwa muda mrefu kiasi cha kusababisha mgawanyiko mkubwa baina ya mashabiki wao.
Diamond na Kiba wataungana na nyota wengine wa bongo fleva katika kuimba wimbo huo wakiwemo  Mwasiti Almasi, Darasa na Vanesa Mdee ambapo tayari kila mmoja ameshapatiwa ala kwa ajili ya kuingiza sauti.  
Chanzo cha kuwepo kwa ‘bifu’ kati yao mpaka sasa hakijajulikana, huku kila mmoja  akikana kuwepo kwa hali hiyo lakini  bado wameshindwa kufanya kazi pamoja kama ilivyo kwa wasanii wengine.
Baadhi ya wadau wa muziki wamejaribu kuwakutanisha pamoja wasanii hao ili kuondoa  ‘bifu’ walilonao lakini imeshindikana, huku tukishuhudia madongo ya kila mmoja akimrushia mwenzake katika mitandao ya kijamii.
Hilo si jambo zuri kwa wasanii wakubwa kama hawa ambao  kutokana na umahiri wao wamekuwa wakiipeperusha bendera ya Tanzania kila mara katika medani ya kimataifa kwa  nyakati tofauti.
Kwa sasa wasanii hao wanakutana katika kamati hiyo ya Serengeti  Boys ambapo kwa namna moja ama nyingine watahitaji kuwa na mawasiliano ili kuhakikisha wanatimiza wajibu  ndani ya kamati hiyo ili kufanya mambo yaende sawa.
Hivyo  ni wakati wa nyota hao kuzizika rasmi  tofauti zao kwa kufungua ukurasa mpya wa kusaidiana na kushirikiana katika kazi zao na hivyo kusaidia maendeleo ya sanaa ya Tanzania.
Itakuwa ni jambo la jema tukisikia tamko toka kwao kama wameingia studio kurekodi kazi ya pamoja, au mmoja wapo kamshirikisha mwingine katika moja ya kazi yake ama lebo ya ya Diamond na lebo ya Kiba zinashirikiana katika kuinua wasanii chipukizi.
Diamond na Kiba ni wasanii wenye vipaji vya hali ya juu hivyo naamini kama watakuwa na ushirikiano ni wazi watapata mafanikio zaidi ya ilivyo sasa, kwa jinsi wanavyokubalika pindi wakianza kuwa na uhusiano mzuri ni wazi wataliteka zaidi soka la muziki.
Ni wasanii ambao wametembea katika nchi nyingi duniania na hivyo kujifunza mengi mazuri kupitia wasanii wakubwa waliokutana nao hivyo kama watamaliza tofauti zaom wataweza kubadilishana uzoefu ili kuweza kujijenga zaidi kisanaa.
Hivyo wanatakiwa wawe mfano wa kuigwa na wasanii wengine na hasa chipukizi ambao mara nyingi wanapenda kufuata nyayo za watu waliopata mafanikio katika kazi zao sasa kama wanakuiwa na uhasama chipukizi watajifunza nini kutoka kwao?
Kwamba, Diamond anazijua njia za magharibi na Kiba anazijua za Mashariki sasa wakiwa na mahusiano mazuri ni wazi kila mmoja atamuonesha njia mwenzake watazidi kujiongezea mashabiki na hatimaye kujiongezea vipato vyao kwani watapata fursa za kutumbuiza maeneo mengi zaidi.
Kama watamaliza tofauti zao pia itasaidia kuongeza mapato yao kupitia kazi zao kwani hata wataungwa mkono na mashabiki wa kila upande   ambao watanunua kazi zao na hatab kujitokeza kwa wingi katika maonesho yao.
Kiba na Diamond wote wapo kwenye Kamati iliyoundwa na Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Nape Nnauye ya kuhamasisha na kuwaunganisha Watanzania kwa pamoja ili kuichangia Serengeti Boys iliyofuzu Fainali za Afrika  zitakazopigwa nchini Gabon  mwezi Mei mwaka huu.

Katibu wa Kamati hiyo ni Mwesigwa Selestine ambaye pia ni Katibu Mkuu wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) wakati wajumbe wengine ni pamoja na Miss Tanzania 1999 , Hoyce Temu, Mtangazaji wa EFM Radio na TV, Maulid Kitenge,  Mkurugenzi wa Mahusiano wa kampuni ya Airtel Tanzania, Beatrice Singano, Mkurugenzi wa Habari katika Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Hassan Abbas, Mkurugenzi wa Global Publishers Limited, Eric Shigongo na Mkurugenzi wa Radio Clouds, Ruge Mutahaba.