LIPULI FC IRUDI NA MOTO WA ZAMANI LIGI KUU

Na  Dina Ismail
BAADA ya kutoshiriki Ligi Kuu soka Tanzania Bara kwa takribani miaka 17, hatimaye timu ya Lipuli ya Iringa imekata tiketi ya kucheza ligi hiyo msimu wa 2017/18.
Lipuli  iliyokuwa tishio katika miaka ya nyuma kwenye soka, imekata tiketi hiyo baada ya kufikisha pointi 29 ambazo haziwezi kufikiwa na timu yoyote katika kundi A huku ikibakiwa na michezo miwili.
Chini ya kocha wake mkuu, Richard Amatre ambaye ni raia wa Uganda, timu hiyo ilianza kuonesha dalili za kupanda daraja tangu kuanza kwa ligi hiyo ambapo iliweza kufanya vema katika michezo yake.
Amatre ambaye alipata kuwa kocha msaidizi wa Simba, amekuwa akijigamba kwa timu yake kufanya vema na kweli ndicho kilichotokea na hivyo kuifanya timu yake kupanda daraja.
Kocha Amatre ambaye amedumu na timu hiyo kwa miaka mitatu pamoja na kuwapongeza wachezaji wake kwa hatua hiyo anasema haikuwa rahisi kwao kuibuka vinara katika kundi lao.
Lipuli ambayo miaka ya nyuma ilipokuwa ikishiriki Ligi Kuu Bara ilikuwa ni moja ya timu tishio sana, haijapanda kirahisi kwani kabla ya mwaka huu ilikuwa ikiishia nafasi ya pili na tatu.
Ni moja ya timu iliyokuwa na heshima kubwa Tanzania; mkoa wa Iringa una matajiri wengi ambao kama wakiamua wanaweza kuihudumia timu hiyo na kuepuka vishawishi hivyo vya timu kubwa na kutoa upinzani mkubwa kwa Yanga na Simba zinapokwenda kwenye uwanja wa Samora pale Iringa.

Enzi hizo, hakuna mshabiki wa soka aliyekosa kuifahamu Lipuli kwani haikuwa timu ya kawaida kwa kutandaza kabumbu safi kupitia kwa nyota wake waliokuwa na uwezo wa hali ya juu.
Kama hiyo haitoshi, Lipuli ilikuwa ni roho ya Wana Iringa kwani ni timu pekee iliyokuwa ikiuwakilisha vema mkoa huo, hivyo ni wazi kwamba wakali hao wa zamani wataendeleza makali yao ya zamani.
Kwamba, lengo lao la kufanya mapinduzi ya soka kwa mkoa wa Iringa liendane sambamba na kufanya vema katika Ligi Kuu Bara kwani kinyume na hapo itakuwa ni kazi bure.
Kupanda kwa Lipuli ni nafasi pekee kwa wakazi wa mkoa wa iringa pamoja na wadau wa soka kuhakikisha wanaiunga mkoni na kuipa sapoti timu hiyo ili iweze kudumu na siyo kupanda na kushuka.
Matajiri wa Iringa wanatakiwa kujitolea kuisaidia timu hiyo iweze kujimudu na kuondokana na ukata ambao unaweza kuitia timu hiyo majaribuni kwa wachezaji kupokea rusha na kupeleke timu hiyo kupoteza mwelekeo kwenye ligi ya msimu ujao.
Lakini kitu kingine ambacho ni chamuhimu zaidi kwa timu hiyo ni kuepuka kufungamana na upande mmoja katika ya timu mbili kubwa za Simba na Yanga na kujenga timu isiyofungamana na upande wowote kati ya hizo mbili.

Timu nyingi kwenye ligi ya Vodacom zimekuwa zikiathirika kwa jambo hilo la kufungamana na upande mmoja kati ya timu hizo mbili, na hali huwa mbaya na wakati mwingine kushuka daraja pindi timu kubwa inapohitaji pointi tatu ili kutwaa ubingwa au nafasi fulani kwenye msimamo .