KOZI ZA UKOCHA ZISAIDIE KULETA MAPINDUZI KATIKA SOKA

Na Dina Ismail
KADIRI miaka inavyosonga  ndivyo  mwamko na chachu ya kusaka  mafanikio ya soka yanavyoongezeka.
Hilo halina ubishi kwani tumeshuhudia mengi  katika miaka ya karibuni  na mojawapo ni  kwa wachezaji wa Kitanzania kuitangaza nchi katika bara la Afrika na dunia kwa ujumla kupitia soka ya kulipwa.
Katika  harakati hizo za kusaka mafanikio, wiki iliyopita kumezalishwa makocha wapya 27 ambao walifuzu kozi ya  kati  iliyoratibiwa kwa kufuata miongozo ya Shirikisho la soka Tanzania (TFF) na lile la Afrika (CAF).
Kozi hiyo ambayo ilijazwa na idadi kubwa ya wachezaji  mahiri waliokuwa  wakizicheza timu kongwe za Simba na Yanga na ile ya Taifa ‘Taifa Stars’  ambapo siku ya ufungaji mgeni rasmi alikuwa  Rais wa TFF, Jamal Malinzi.
Malinzi alifurahishwa na idadi kubwa ya makocha waliohitimu  na na kusema kuwa itasaidia kukuza soka nchini , huku akisikitishwa  na ushiriki wa wanawake ambapo ni mmoja tu kati ya  27 aliyejitokeza na hivyo kutoa rai kwa wanawake kujitokeza kwenye kozi za namna hiyo.
Kujitokeza kwa nyota hao wa zamani kushiriki kozi hiyo ni jambo la  kupongezwa kwani  inaonesha  ni jinsi gani wana uchungu na maendeleo ya nchi yao hivyo wameona kufanya hivyo kutasaidia kwa namna moja ama nyingine.
Ikumbukwe, wengi wa washiriki wa kozi hiyo walipata kutoa mchango mkubwa katika soka Tanzania enzi za uchezaji wao hivyo naamini kupitia mafunzo hayo pamoja na uzoefu walionao wa kisoka kutasaidia kupatikana kwa wachezaji bora zaidi chini ya mikono yao.
Hata mwanamama pekee aliyeshiriki kozi hiyo, Doris Malyaga ambaye ni mwandishi wa habari za michezo nchini, mbali na ukufunzi huo pia ataitumia vema kalamu yake katika kuhamasisha wanawake kujitokeza kwa wingi katika kozi kama hizo.
Hii in maana kwamba, kama kutakuwa na makocha wengi wanawake wenye viwango na  utaalamu wa hali ya juu ni wazi kwamba itapunguza idadi ya makocha wa kiume katika timu za wanawake.
Hivyo basi  mafunzo waliyoyapata yasiishie kuwavimbisha vichwa, vyeti walivyoviopata visiwe mapambo katika kuta za nyumba zao bali wayatumie kuwafunza  wachezaji  wenzao na hasa timu za vijana ambazo ni muhimu sana katika mustakabali wa matunda ya baadae.
Kama hiyo haitoshi, makocha hao wapya wasibwetye na kozi hiyo  hivyo wanawajibu wa kujingeza zaidi ili kuweza kufikia katika madaraja ya juu  ili siku zijazo Tanzania itanue wigo wa kuwa na makocha wanaofundisha nje ya Tanzania.
Baada ya hatua hiyo naamini kila mshiriki wa kozi hiyo hatobweteka na hatua hiyo hivyo atakuwa na jukumu la kujiongeza zaidi ili kupanda daraja.
Kozi hiyo iliendeshwa na   mkufunzi anayetambuliwa na  CAF Wilfred Kidao,  akisaidiwa na kipa mkongwe wa zamani  Manyika Peter aliyefundisha  mtaala kwa makocha wa makipa,  Dk. Nassoro Ally Matunzya aliyefundisha  kuhusu tiba za wanamichezo/wanasoka  pamoja na mMkufunzi wa muda mrefu wa soka, Hemed Mteza.
Mbali na Malyaga , washiriki wengine walohudhuria  kozi hiyo ya siku 14 ni pamoja na  Boniface Pawasa, Fred Mbuna, Innocent Haule, Herry Morris, Ivo Mapunda, Nizar Khalfan na Mussa Hassan Mgosi.

Wengine ni Omar Kapilima, Amosi Mgisa, Uhuru Mwambungu, Yussuf Macho, George Minja, Haruna Adolf, Selemani Omari, Ally Ruvu, Masoud Selemani, Haji Mustapha, Mhasham Khatib, Issa Ndunje, Salum Kapilima, Said Salum, Julio Elieza, Hassan Mwakami, Rajab Mponda, Ally Mbonde na Evod Mchemba.

Comments