'KIKI NI UFINYU WA MAWAZO'

Na Dina Ismail
HIVI karibuni  kumeibuka tabia inayokera na  kuchefua inayofanywa  na  baadhi ya  wasanii wa filamu au wale wa bongo fleva , ikijulikana kama Kiki.
Kitendo hicho kimekuwa kikitumika zaidi pindi wanapokaribia kutoa nyimbo zao au filamu zao.
Si  jambo baya kwao  kutafuta ‘attention’ katika kuelekea kuachia kazi zao mpya lakini njia wanazozitumia ni  mbaya na sio za kuridhisha.
Msanii kama kioo cha jamii hana budi kufanya ama kuonesha vitu vizuri ili awe mfano bora kwa wanaomzunguka lakini si kwa baadhi ya bongo.
Utakuta msanii anamtukana mwenzake matusi  mazito katika mitandao ya kijamii ama vyombo vya habari au msanii anaweza mzulia mwenzake jambo lolote la fedheha kiasi cha kuleta picha mbaya katika jamii lakini mwisho wa siku inakuja bainika kwamba ilikuwa ni Kiki ya kutoa kazi yake mpya.
Tumeshuhudia wasanii wakifanya mambo ya aibu sana katika mitandao ya kijamii kinyume na mila na desturi za Kitanzania na yote hayo wanafanya katika kutafuta umaarufu.
Kweli sasa hivi sanaa imekuwa ngumu kutokana na hali ya kiuchumi na pia uwepo wasanii wenye vipaji wanaochipukia kila kukicha kiasi cha kufanya sanaa iwe ngumu.
Na kwa hali hiyo ndipo wasanii hutafuta njia mbadala za kujiweka matawi ya juu kwa niia zisizo sahihi ambazo mwisho wa siku inakuwa ni kama dhalili kwao.
Kinachoonekana hapa ni ufinyu wa fikra na mawazo  pia katika kutayarisha hadi kupakua kazi zao kwani kama msanii yuko vizuri katika fikra hizo hawezi ‘kutafuta kiki’ ili atoe albamu ama filamu.
Usanii ni kipaji sasa kama kuna walioingia katika sanaa kwa lengo la kusaka umaarufu au kuuza sura ndio hao mwisho wa siku wanafanya mambo ya ajabu ajabu.
Mbona kuna wasanii wengi wanafanya sanaa kwa muda mrefu na majina yao yapo juu na hata siku moja huwakuti ama kuwaona wakitafuta ‘kiki’ za kijinga wao wanapata umaarufu kulingana na kazi zao.
Wasanii kama Mwana Fa, Fid Q, Lady Jaydee, Riyama Ali, Joh Makini, King Majuto ni baadhi ya wale wanaojielewa kwani hata siku moja huwezi sikia wanatafuta ‘kiki’ wakianza kutoa kazi zao.
Sana utaona matangazo ya ujio wao mpya, na pindi kazi ikitoka kama ni nzuri itachukua nafasi yake kupitia mashabiki na mwisho wa siku heshima yao inabaki kuwa juu.
Pia kuna wasanii walioibuka miaka ya hivi karibuni kama Darassa, huyu ni mmoja wao ambaye ubora wa kazi zake umeweza kumuweka katika matawi ya juu ya muziki wa kizazi kipya.
Kuna njia nyingi za maana na zenye heshima wanazoweza kupitia katika ‘kuprome’ kazi zao kama ilivyo kwa wasanii wan chi zilizoendelea badala ya hizi za aibu wanazozidumia baadhi yao hivi sasa.
Nadhani ifikie mahala wasanii wanaoishi kwa ‘kiki’ kujipanga upya  kuumiza vichwa kwa kutayarisha kazi  nzuri na zinazoendana na maadili ya kitanzania, kinyume na hapo naliona anguko la baadhi yao.

Mungu Ibariki Tanzania.