SIMBA ISIKILIZWE JUU YA WAAMUZI



Na Dina Ismail
HIVI  karibuni  uongozi  wa Klabu ya Simba, ulidai kutokuwa  tayari  kwa  timu  yao  kucheza  mechi yoyote  na  mahasimu  wa  jadi  Yanga iwapo watatumika  waamuzi  wa hapa nchini.
Mkuu wa Kitengo cha Habari na Mawasiliano wa Simba, Haji Manara  amesema kwamba  wamefikia uamuzi huo baada ya kuchoshwa na  uonevu  wa dhahiri wanaofanyiwa na waamuzi hao kila  wanapokutana.
Simba wameliomba Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kutumia waamuzi kutoka nje ya nchi katika mechi zao na Yanga, ili haki itendeke, huku wakitarajia kumuandikia barua rasmi  Rais wa TFF, Jamal Malinzi juu wa uamuzi wao.
Manara aliweka wazi kuwa kila wanapocheza na Yanga waamuzi wamekuwa wakiwaonea kwa makusudi  huku wakionesha dhari kwamba wametumwa.
“Kuna matukio mengi ya kustaajabisha yamekuwa yakitolewa na waamuzi pindi tunapocheza na mahasimu wetu, wachezaji wanapewa kadi bila kosa la kueleweka, magoli  yetu halali yanakataliwa, wenzetu wanafunga magoli ya utata yanakubaliwa na mengine mengi”, alisema
Akienda mbali zaidi, Manara alisema wachezaji wao wamekuwa wakifanyiwa vitendo vingi visivyo vya kimichezo na wapinzani wao lakini waamuzi hao wanaishia kuwaadhibu wachezaji wao tu.
“Tumechoshwa na hii hali kwa kweli, hatutokuwa tayari kuingiza timu uwanjani iwapo waamuzi watakuwa ni wale wale”, aliongeza Manara
Manara alisema watakuwa tayari hata mapato yao yote  ya mchezo wao kutumika kwa ajili ya kugharamia waamuzi kutoka nje  kuweza kuchezesha mechi yao ili kuwepo na haki.
Ukiangalia kauli ya Simba ina mashiko makubwa na hasa ikizingatiwa kuwapo kwa malalamiko  ya kuboronga kwa waamuzi si katika mechi za Simba na Yanga tu hata katika mechi mbaloimbali za Ligi Kuu Kuu Bara.
Mfano hivi karibuni katika  mchezo baina yao katika duru la kwanza la Ligi Kuu Bara uliopigwa Oktoba Mosi kwenye Uwanja wa  Taifa jijini Dar es Salaam na kumalizika kwa sare ya bao 1-1, mwamuzi Martin Saanya alilikataa bao halali la Simba na kulikubali bao la Yanga ambalo mfungaji aliukumbatia mpira kabla ya kufunga.
Katika mchezo huo pia Saanya alimtoa nje kwa kadi nyekundu  Nahodha wa Simba, Jonas Mkude kwa kadi nyekundu kabla ya kamati ya Saa 72 ya Uendeshaji na Usimazi wa Ligi kuifuta baada ya kuona hakufanya kosa.
Kama hiyo haitoshi, kamati hiyo baada ya kupitia kwa kina ripoti ya mchezo huo,  iliamua kumfungia  kuchezesha soka kwa miaka miwili  Saanya  pamoja na Msaidizi wake, namba moja, Samu Mpenzu ambaye anadaiwa kukataa  la Simba lililofungwa na Ibrahim Hajib mapema kipindi cha kwanza akidai aliotea.
Katika mchezo huo, maamuzi ya utata ya Saanya yalisababisha vurugu baada ya Yanga kupata bao la kuongoza lililofungwa na mshambuliaji Mrundi, Amissi Tambwe katika  dakika ya 26, akimalizia pasi ndefu ya beki Mbuyu Twite.
Bao la Tambwe lilizua kizaazaa  ndipo wachezaji wa Simba wakamvaa Saanya wakidai  Tambwe aliushika mpira kabla ya kufunga. Na katika vurugu hizo, Saanya alimtoa kwa kadi nyekundu Mkude dakika ya 29 kwa sababu ndiye aliyekuwa mstari wa mbele.
Hali hiyo ilipelekea mchezo kusimama  kwa takriban dakika tano baada ya mashabiki wa Simba kuanza kufanya vurugu waking’oa viti na kutupa uwanjani kabla ya Polisi kuanza kutumia  milipuko ya gesi za kutoa machozi kuwatuliza kabla ya mchezo kuendelea na  Simba kusawazisha dakika ya 87 kwa bao la Shizza Kichuya.
Kilio kwa waamuzi haliko kwa Simba peke yao kwani hata Yanga imekuwa ikilalamikia baadhi ya waamuzi wanaopangwa katika mechi zao na Simba kwa nyakati tofauti huku Simba ikionekana kuwa muhanga zaidi wa maamuzi tata.

Kwa hali hiyo, TFF  inapaswa kuzingatia na kulichukulia  kwa malalamiko ya  Simba ili kuweza kupatikana nusura  kwa  soka la Tanzania.

Comments